Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Serikali imesema itaongeza udhibiti dhidi ya watu wanye virusi vya ugonjwa hatari wa ebola, ili wasiweze kupenya na kuingia nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, baada ya kuulizwa na gazeti hili juzi kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuzuia ugonjwa huo usipenye nchini kufuatia Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa tahadhari kwa nchi za Afrika juu ya kusambaa kwake.
Waziri huyo alisema kuwa serikali inaendelea kuweka uangalizi kwenye maeneo ya mipakani kwa lengo la kuwabaini watu wenye ugonjwa huo wasiweze kuruhusiwa kuingia nchini.
Alisema mbali na kuweka uangalizi kwenye mipaka, pale watakapogundua mgonjwa watachukua taarifa zake alikotokea zikiwa ni njia za kuongeza udhibiti.
Alisisitiza kuwa jitihada za serikali zipo palepale ndiyo maana hata ugonjwa huo ulipoibukia nchini Uganda miaka iliyopita, uliweza kudhibitiwa usiingie nchini.
Kwa mujibu wa Dk. Rashid, ugonjwa huo unaotokana na maambukizi ya virusi utaweza kudhibitiwa kama ilivyokuwa kwa ule wa dengue ambao uliingia takribani miezi mitatu iliyopita na kusababisha vifo vya watu wanne.
Ugonjwa wa ebola ambao unaweza kuambukizwa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mwingine kwa kugusana, hadi sasa umeshaua zaidi ya watu 400 katika baadhi ya nchi za Afrika Magharibi ikiwamo Guinea Bissau.
Kutokana na hali hiyo, WHO, limetoa tahadhari kwa nchi za Afrika hasa zilizojirani na nchi hiyo dhidi ya ugonjwa huo hasa baada ya wagonjwa wa ebola kukimbilia Siera Leone.
Ebola ni ugonjwa hatari kutokana na kutokuwa na tiba wala kinga na ni ugonjwa unaoua haraka.Hilo linatosha kuwa fundisho kwetu kwamba serikali na wananchi wenyewe wanatakiwa kuchukua hatua za tahadhari ili homa hiyo isiingie nchini.
Kama alivyosema Waziri Rashid, tahadhari inayotakiwa kuchukuliwa na mamlaka mbalimbali ni kudhibiti wageni wanaoingia nchini katika maeneo ya mipaka kwa kuwachunguza kuhakikisha kwamba hakuna aliyeambukizwa ebola.
Pamoja na hatua hizo, upo umuhimu kwa mamlaka mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huo lengo likiwa ni kwenda hospitali na katika vituo vya afya ikiwa wataona dalili hizo.
Wataalam wanasema kwamba pamoja na kutokuwapo na tiba wala kinga dhidi ya ebola, kuna uwezekano wa muathirika kupona ikiwa atapata uangalizi na huduma bora kutoka kwa madaktari, wauguzi na watoa huduma wengine wa sekta ya afya.
Ebola huhesabiwa moja kati ya magonjwa ya mlipuko na wagonjwa wake hutengenishwa na wagonjwa wengine ili wasipate kuambukizwa. Wataalamu wa afya wanasema kuwa huambukizwa kwa kugusa damu ya mtu aliyeembukizwa ugonjwa huo.
Pale mtu anapopata ebola, dalili zake za kwanza ni kuonekana kama magonjwa mengine. Watu wanapata homa, kujisikia kuchoka, maumivu ya kichwa, maumivu ndani ya tumbo, maumivu katika viungo na maumivu ya kooni. Kwa dalili hizo, watu hufikiria kwamba wana magonjwa mengine kama vile malaria au homa ya matumbo.
Baada ya dalili hizo, mgonjwa huanza kutokwa damu kwa kiasi kikubwa sambamba na kupata mshituko huku shinikizo la damu likiwa chini. Pia mapigo ya moyo kwenda kwa kasi, na mzunguko wa damu kuwa hafifu mwilini.
Wataalamu wa afya wanasema hali hiyo husababisha viungo vya mwili kuuma sana na baadaye viungo vya mwili hunaacha kufanyakazi. Ugonjwa huo pia husababisha ukakamavu mwilini na humuacha muathirika kitandani na hata kama atafanikiwa kufika hospitalini, lakini wengi wao hupoteza maisha.
Huu ni ugonjwa hatari sana na usiotaka masihala. Hii ni changamoto kubwa kwa jamii nzima ya Tanzania kuchukua hatua zinazostahili ili kuudhibiti kuepusha uwezekano wa kutokea vifo.
Hatua ya kwanza ni serikali kupeleka wataalamu wa kutosha wa afya katika maeneo ya mipakani wakiwa na vifaa kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi wageni wanaoingia nchini.
Hatunabudi kukumbuka kwamba ugonjwa unapoingia katika nchi jirani, kuna uwezekano mkubwa kuingia nchini kwa urahisi ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa.
Ni matarajio yetu kwamba serikali imekusudia kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti ebola isiingie nchini kutokana na kauli hii ya Waziri Dk. Rashid.
CHANZO: NIPASHE
