Ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka Uganda mpaka bandari ya Tanga Tanzania umesitishwa.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa mashirika ya habari ya kimataifa ya Reuters na Bloomberg ni kufuatia kampuni ya uchimbaji mafuta ya Tullow kushindwa kuwauzia kampuni za Total ya Ufaransa na CNOOC ya Uchina vitalu vya mafuta wiki iliyopita.
Kampuni ya Total ndiyo inasimamia ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445.
Tayari hatua za awali kuelekea ujenzi huo kama ramani, baadhi ya kandarasi na utanuzi wa bandari ya Tanga Tanzania zilishaanza.
"Shughuli zote za ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline) ikiwemo kandarasi zimesitishwa mpaka hapo taarifa mpya itakapotolewa kutokana na kushindikana kwa mauzo ya visima," afisaa mmoja nchini Uganda ameiambia Reuters kwa sharti la kutotajwa jina.
Makubaliano ya uuzwaji wa vitalu hivyo yalivunjika Agosti 29 kutokana na mzozo wa kodi na mamlaka za Uganda.
"Kuvunjika kwa makubaliano ya mauzo kunaleta suitafahamu juu ya nani atagharamikia kitu gani katika kuendeleza mradi huo, ambao ungekuwa na mfumo sawia wa umiliki kama ule wa vitalu vya mafuta," kwa mujibu wa afisa huyo.
Image captionKampuni ya Total ndiyo inasimamia ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,445.
Uganda iligundua mafuta ghafi miaka 13 iliyopita, lakini uchimbaji wa kibiashara ulicheleweshwa kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu, ikiwemo bomba la mafuta.
Mradi wa ujenzi wa bomba hilo ulipangiwa kugharimu dola bilioni 2.5, kutoka Hoima. magharibi mwa Uganda mpaka bahari ya Hindi, Bandari ya Tanga Kaskazini mwa Tanzania.