Heshima na hadhi ya Sheikh Ponda katika nyoyo za Waislam

Heshima na hadhi ya Sheikh Ponda katika nyoyo za Waislam

Mimi ni mkristo tena mkatoliki, naamin Allah atamruzuku sheikh Ponda kwa kuipigania haki na ustawi wa uislamu, nashangaa waumin wa Bakwata wanavomponda laiti wangejua nasema laiti wangeujua ukweli wa dini yao na inavyopelekwa wasingethibutu kumdhihaki sheikh ponda mtu alieteswa, kunyanyaswa kwa kuutetea uislamu
 
Masheikh wa Bakwata hua tunawaita masheikh ubwabwa ashakhum sii matusi, wamewagawa waislamu, shirikisho la uislamu afrika mashariki ambalo linahistoria kwenye uhuru wetu pia, fedha zilizochangwa misikitini kwenye kupigania uhuru, wa nchi yetu yote yamepotea, ama hikma ya kafir ipo usoni pake na sio akilini.
 
FAHAMU HESHIMA NA HADHI YA SHEIKH PONDA KATIKA NYOYO ZA WAISLAM

''Allah ni Mjuzi Allah na ni Mbora wa kulipa.

Sheikh Ponda utayakuta malipo yako kwa Allah yakiwa makubwa kwa subra na ustahamilivu kwa ajili ya dini yake. Hukuwa tayari kuuza uhuru wako kwa matakwa ya wenye kudhulumu. Muda wote ulitutia moyo mawakili wako kila tulipokutana na vitimbi. Mara nyingi sisi mawakili tulikuwa kama wateja na wewe ndiye wakili.

Hakika wewe ni kiongozi. Umma huu wa Waislam wa Tanzania utaishi kwa mfano wako. Alhamdulilah leo uko huru baada ya miaka miwili na miezi mitatu jela ukiwa na jeraha kubwa la risasi. Allah anayo siri kubwa katika maisha yako Sheikh Ponda. Allah akuhifadhi kiongozi wetu. Amin.''

Wakili Juma Nassoro

Ilikuwa katika semina ya Vijana wa Kiislam Tanzania mwaka wa 1988 ndipo kwa mara ya kwanza nilipofahamiana na Sheikh Issa Ponda. Ninachokumbuka kwa Sheikh Ponda ni kuwa alitusalisha sala moja na niliusikia usomaji wake mzuri wa Qur'an. Nilimpenda Ponda kutoka siku hiyo. Semina hii ilikuja baada ya mambo mengi dhidi ya Uislam kutokea nchini.

Kulikuwa na sakata la Sophia Kawawa kutaka Qur'an ibadilishwe. Hii ilitokea mwezi Mei 1988. Baada ya kauli hiyo palifanyika maandamano makubwa Zanzibar kumpinga Sophia Kawawa na Waislam walishambuliwa, baadhi wakauliwa na wengine wakapata ulemavu wa maisha.

Sheikh Said Gwiji mshtakiwa namba moja na wenzake walishitakiwa na wakafungwa jela miezi 18. (Mwaka wa 2012 nilifanya mahojiano na Sheikh Gwiji na akaniambia hajuti kuwa katika historia ya maisha yake alipatwa kufungwa jela). Kosa lao likiwa ni kuihami Qur'an ya Allah isichezewe.

Kulikuwa na vita vikipigwa dhidi ya vazi la hijab na kesi maarufu ilikuwa ya Fikira Omari mfanyakazi wa Kiltex. Kulikuwa na kesi ya Sheikh Kurwa Shauri aliyeshitakiwa kwa ''uchochezi'' na mambo mengine. Sheikh Kurwa Shauri aliwekwa rumande na akiletwa mahakamani yuko nusu uchi. Alishinda kesi lakini alifukuzwa Zanzibar na kupelekwa "kwao," Zanzibar.

Katika hayo kulikuwa na tatizo la Mchungaji Christopher Mtikila aliyekuwa akimbughudhi Rais Mwinyi na kuwashambulia Waislam hasa wenye asili ya Kiasia na Kiarabu bila woga na magazeti yakimtoa katika picha na sura ya kuzidi kumjaza jeuri na ukaidi.

Kulikuwa pia na ''Christian Lobby,'' mtandao wa siri katika vyombo vya habari vilivyokuwa vikiwapiga vita Waislam waliokuwa katika serikali ya Rais Mwinyi achilia mbali kuupiga vita Uislam wenyewe wakitumia nafasi zao katika vyombo hivyo. Ulikuwapo mtandao wa chini kwa chini wa vijana wa Kiislam kupambana na fitna hizi. Mwaka wa 1988 wakakutana Dodoma na hapa ndipo nilipojuana na Sheikh Ponda Issa Ponda.

Historia ya Waislam wa Tanzania itakapokuja kuandikwa jina la Sheikh Ponda Issa Ponda litaunganishwa na jina la Mufti Sheikh Hassan bin Amir kwa kitu kimoja nacho ni ardhi ya Chang'ombe Dar es Salaam ambako Waislam chini ya uongozi wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) walikusudia kujenga Chuo Kikuu mwaka wa 1968.

Katika uwanja huu ndipo Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere akishuhudiwa na Tewa Said Tewa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir aliweka jiwe la msingi la chuo hicho.

Chuo hakikujengwa na EAMWS ikapigwa marufuku na serikali. Mambo hayakuishia hapo. Sheikh Hassan bin Amir akakamatwa na kufukuzwa nchini akarudishwa ''kwao'' Zanzibar. Serikali ikaunda BAKWATA na Chuo Kikuu cha Waislam hakikujengwa.

Nini kilisababisha nakma hii?

Leo si tabu kujua sababu yake. Kulikuwa na viongozi ndani ya serikali ambao hawakuoendezewa kuona Waislam wanaelimika.

Waliokuwa karibu na Sheikh Hassan bin Amir wanasema katika siku zake za mwisho kila alipotajiwa ule mradi wa chuo kikuu alikuwa akilia na kusema ilikuwa hamu yake kujenga chuo Kikuu kama Azhar ya Misri na akifika hapo alikuwa akibubujikwa na machozi.

Wakati ule Sheikh Hassan bin alikuwa na miaka zaidi ya 90 na aliishi na simanzi hizi hadi alipokufa mwaka 1979.

Sasa msomaji wangu fikiria na jiulize kwa historia kama hii Waislam wanawatazamaje masheikh wa BAKWATA wanapokusanyika na kumshambulia Sheikh Ponda?

Ponda aliyeongoza maandamano ya Waislam dhidi ya Baraza la Mitihani Tanzania lililokuwa likishutumiwa kuhujumu wanafunzi katika shule za Kiislam.

Sheikh Ponda ana historia ya kutukuka katika kupigania haki bila hofu hawa masheikh wa BAKWATA hawataishi kuifikia.

Picha: Picha ya kwanza Sheikh Ponda na Wakili Juma Nassoro Mahakamani Morogoro. Picha ya pili Sheikh Ponda akiwa kafungwa pingu na picha ya tatu Sheikh Ponda ameelekea Kibla Msikiti wa Kichangani anaomba dua kabla hajaongoza maandamano dhidi ya Baraza la Mitihani mwaka wa 2012.
Naomba uniulizie kwa Sheikh Ponda vipi ule utabiri wake wa Lissu kuwa rais na yeye kuwa waziri wa dini na mshauri mkuu wa Lissu umefikia wapi.
 
Nilikua nikimuona mitaani sheikh Ponda na alikua mtu mkimya lakini mkakamavu, mara nyingi akitembea kwa hatua zake za harakaharaka. Jambo moja kumuhusu ni kwamba hawezi kupita bila kusalimia watu atakao wakuta mahali, na wewe huwezi kuwa wa kwanza kumtolea salamu, ataanza yeye maana kafanya salamu kama ni ibada vile!

Mara ya kwanza nilipomsikia akiongea ilikua 1993 katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Nilikua nimefika Mahakama ya Kisutu kugonga muhuri wa Hakimu karatasi zangu za kisheria, na kumbe siku hiyo ndio ilikua hukumu ya kina Mazinge na wenziwe katika ile kesi ya kadhia maarufu ya kuvunjwa mabucha ya nguruwe (Mbokomu Butcher) pale Manzese

Kwenye chumba cha mahakama waliruhusiwa wasikilizaji wachache tu. Mawakili wa Washtakiwa ambao walikua ni Yusuph Mchora na Nassib Mselem walimuita Sheikh Ponda ambaye alifika akiwa amechelewa na chumba kishajaa ili naye aingie

Baada ya kama saa moja na ushei hivi Ponda akatoka na kuwakusanya baadhi ya watu ambao niligundua ni Waumini wenzao pia ndugu na jamaa wa Washtakiwa na kuwaeleza kwamba pamoja na ushahidi usio na shaka kwamba hao wahadhiri kina Mazinge, marehemu Magezi na wengine kuonesha kutokuwepo kwenye hayo maeneo wakati vurugu zinatokea lakini hakimu kaamua kuwafunga miaka mitano kila mmoja! Kesi ilitolewa hukumu na marehemu Jaji Projestus Rugazia ambaye wakati huo alikua Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu

Ponda alikua akiongea kwa kukasirika sana na baada ya pale akawaomba wale watu waondoke wakakutane na wenzao ama Msikiti wa Mtoro au Mwembechai(sikumbuki vizuri hilo) ili wajue nini cha kufanya

Walimsikiliza na wote walitii na wakaondoka pale Kisutu bila vurugu kuelekea huko walipokubaliana. Hawa jamaa baadae walikuja kutolewa kwa msamaha wa Rais wakati Mzee Ali Hassan Mwinyi anakaribia kumaliza kipindi chake cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kunzia siku hiyo nimekua namuona na kumfatilia Sheikh Ponda ambapo utamkuta katika kila harakati za Waislamu. Hata mwaka 1998 kwenye vurugu za Mwembechai Sheikh Ponda alikua mbele ingawa sikumbuki kama na yeye alikamatwa. Hata huyu Rajab Katimba anayekua kwenye misafara ya Tundu Lissu ni miongoni mwa waliokua wakiratibu michango kwa ajili ya huduma za waliofungwa na walioathirika na vurugu za Mwembechai
 
Sheikh ponda anaheshimika na jamii nzima sio waislam tu kwakuwa anasimamia haki za raia na binadamu kwa ujumla sio waislam peke yao
 
Sheikh ponda anaheshimika na jamii nzima sio waislam tu kwakuwa anasimamia haki za raia na binadamu kwa ujumla sio waislam peke yao
Nakubaliana nawe mkuu Kayaman. Wilfred Rwakatare aliyewahi kua Mbunge wa Bukoba mjini wakati fulani alijikuta yupo mahabusu na wakakaa selo moja na Sheikh Ponda

Alikua curious kumfatilia kutokana na sifa zake "mbaya" alizokua akizisikia na kuaminishwa lakini anakiri mwenyewe baada ya kumfahamu kua Sheikh Ponda ni mtu mwenye maadili, tabia njema na muungwana sana sana.

Alimuelezea kama ni mtu mpenda haki, anayechanganyika na watu wa aina zote na mwenye hofu ya kweli ya Mungu. Anasema hata wakiwa wanaletewa chakula kutoka kwenye familia zao walikua wanakula pamoja bila kujali kimeletwa na mke wa Rwakatare au mke wa Sheikh Ponda. Anasema mengi juu ya Ponda ni propaganda chafu tu hasa kutoka kwa BAKWATA
 
Back
Top Bottom