Ni kweli biashara ya utumwa ilikuwa moja kati ya historia mbaya sana kwetu sisi waafrika, watu walichukuliwa kutoka sehemu mbalimbali za Afrika kwa nguvu na kuuzwa kama bidhaa bila ya kujali utu wao, jamii zao, familia zao na nyanja mbalimbali za maisha yao binafsi. Wazungu, Waarabu na hata
Waafrika wenzetu walikuwa wakifanya biashara hii kutokana na tamaa ya pesa na utajiri.
Pamoja na ubaya wote ulioletwa na hali hii, ninaona ni hali ambayo isingeweza kuepukika katika historia ya maisha yetu binadamu, watu wenye nguvu wamekuwa wakiwatumikisha wanyonge tangu enzi na enzi, siku zote mtu mwenye nguvu atatamani kubaki na nguvu hizo na pengine kuziongeza zaidi, hii ni hali ya maisha ya ubinadamu, tumeumbiwa tamaa ya vitu vikubwa na kudharau vinyonge. Nafikiri hata kama historia ingepinduka kiasi kwamba Mwafrika angepata nguvu na teknolojia bora kuzidi ya watu wengine mambo yangekuwa hivi hivi, angetamani naye kwa njia yoyote aweze kuongeza nguvu zake na utawala kwa wale ambao angewachukulia kuwa chini yake.
Hata sasa ninaweza kusema kuwa utumwa bado unaendelea ila ni kutokana na sheria zilizopo katika zama hizi tunaona kama mambo yametulia lakini ndani kwa ndani tuna chembechembe bado za kutumikisha pale tunapopata mtu/watu ambao tunaoweza kuwafanyia hivyo kama tuna uhakika hayupo wa kutuzuia.
Nikijaribu kufikiria kwa mtu yeyote sasa hivi akipewa uwezo wa kuwa na watu wa kukufanyia kazi kiasi kwamba mali na utajiri wako unakuwa ukiongezeka na unapewa uamuzi wa kulipa mshahara mkubwa, mshahara mdogo au kutowalipa kabisa. Je wengi wetu tungechagua kipi? tungeweza kumlipa mtu kama hakuna kitu kinachotulazimisha kumlipa? kama tungepewa uamuzi wa kumpa mtu sehemu ya utajiri tulio nao au kuendelea kulimbikiza tungechagua kipi? Mwisho wa siku nionavyo mimi ni kwamba binadamu tumeumbiwa uroho na ubinafsi hasa pale tunapopata nguvu kupita watu wengine, kama hakutakuwa na kizuizi chochote cha nje basi naona watu watatumia njia zozote watakazoona zinafaa kuzidi kujinufanisha.
Nikirudi katika mada, kuhusu kuombwa radhi na heshima yetu sidhani kama itasaidia katika kufuta yaliyokwisha kutendeka na kwa namna mambo ninavyoyaona hata kama tukifanikiwa kuombwa msamaha itakuwa imefanywa kinafiki ili kuzima kelele na sio kwamba kutakuwa na majuto yoyote nyuma yake, kama ni heshima tunaitaka basi isiwe heshima ya kupewa bali iwe ni heshima tutakayoijenga sisi wenyewe bila ya kuwa watu wa kutia huruma na kusingizia shida zote tulizonazo zimetokana na utumwa (ni kweli utumwa umechangia kuturudisha nyuma lakini hatuwezi tukawa tunanyooshea vidole Wazungu/Waarabu kwa kila aina ya matatizo tuliyonayo), heshima hii kama Waafrika bado hatuna katika dunia ya sasa na sidhani kama kuombwa msamaha itaongeza heshima yoyote mbele ya macho ya waliotutawala.