Hiki Sicho Hicho

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
SICHO HICHO

Hiki kilichoko sicho, hiki sicho kilichoko,
Ndicho hiki hichohicho, ndicho hiki hakiko,
Hiki ni kile si hicho, kile kisichokuwako
Hakuna cha mgao, kilichoko ni historia;
Ya mgao!

Aliyesema hakiko, kwamba hakitakuwapo,
Yeye mwenyewe hayuko, alichosema hakipo,
Huyu bwana yuko yuko, kama popo mwenye pepo,
Hakuna cha mgao, kilichoko ni historia;
Ya mgao!

Wanachogawa hakipo, kwani kisingekuwepo,
Ugawe vipi hakipo, hakipo huko mlipo,
Kama wafuata upepo, ndugu zangu mpo mpo,
Hakuna cha mgao, kilichoko ni historia;
Ya Mgao!

Cha nini hki cha nani, kwanini tena ni nini?
Tutamuuliza nani, kinaendelea nini?
Tunakuwa kama nyani, kujenga nyumba mtini!
Hakuna cha mgao, kilichoko ni historia;
Ya Mgao!

Tukubalini watani, janja ya jiwe ya nini?
Hili jambo siyo geni, linarudia kwa nini?
Ahadi zao jamani, twaamini kama dini!
Hakuna cha mgao, kilichoko ni historia;
Ya Mgao!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Nimekupata Mwanakijiji,maneno yako murua
yafaa uvikwe taji, vizuri umechambua
inahitaji kipaji, tungo yo' kuifumbua
Sicho hicho kilichoko, mgao waendelea

Alosema ni Muhongo, utakuwa historia
kumbe yeye ni muongo, mbinafsi wa tabia
amezidisha maringo, matusi yamemjaa
Sicho hicho kilichoko, mgao waendelea

Huyu jamaa ni Profesa, msomi alo bobea
ila anapenda pesa, na majivuno kazidia
ali letaga mkasa, na yule 'mengi' bilionea
Sicho hicho kilichoko, mgao waendelea

wanasema mgao haupo, wapate kutuibia
wamekuwa kama popo, mgao unaendelea
hasara tuipatapo, nani ata tulipia?
Sicho hicho kilichoko, mgao waendelea

By Gstar
 
Nimezipenda tungo zenu wakuu,bahati mbaya natumia simu hapa,pokeeni pendezo.
 
Hongereni kwazo tungo, zilizosheheni mafunzo
Ila kama kuwa ni mhungo, bora muanze mwanzo
Msomi mshupaza shingo, kama kichwani hamnazo
Kilichopo ni uongo, hadaa za kutupotezea.
 
Hongereni kwa tungo nzuri

Sent from my BlackBerry 9780 using JamiiForums
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…