Hili la kukutana na viongozi wa kisiasa, linajenga hatima ya Tanzania ijayo

Hili la kukutana na viongozi wa kisiasa, linajenga hatima ya Tanzania ijayo

Elius W Ndabila

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
324
Reaction score
649
KUKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA NI JAMBO MHIMU KWA MAENDELEO YA TAIFA

Na Elius Ndabila
0768239284

Jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliwahutubia Watanzania kupitia Bunge. Hotuba yake ilichukua dakika 98.

Sikubahatika kuitazama hotuba hiyo mbashara, lakini nimefanikiwa kuisikiliza yote kupitia YouTube ya Bunge. Nimeisikiliza kwa umakini mkubwa. Lakini pia nimesoma uchambuzi wa wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Kwa ufupi hotuba ni kazi ya Fasihi. Na ubora wa kazi ya Fasihi inategemea na Wachambuzi na Wahakiki wa hiyo kazi. Kwa kuwa hotuba ya Mhe Rais ilikuwa ni ndefu leo nimeona nije na Uchambuzi kwenye upande wa siasa. Msingi wa uchambuzi huu utajikita kwenye maneno ya Rais.

"Rais alisema, Nakusudia kukutana na viongozi wa kisiasa wa Tanzania, ili kwa pamoja tuweke msimamo wa kuendesha shughuli za kisiasa".

Kwanza tukubaliane kuwa siasa ni maisha. Maisha tunayoishi Duniani yanatawaliwa na siasa. Hivyo huwezi kuikimbia siasa kwenye uhai wako. Siasa ndiyo inayoamua udhaifu wa Maendeleo au ubora wa Maendeleo, siasa ndiyo inayoamua amani ya nchi au migogoro ya nchi. Ukitengeneza siasa umetengeneza Maendeleo na ukibomoa siasa umebomoa Maendeleo. Wanasiasa ndio wanapanga hatima ya Maendeleo ya nchi.

Mwanafalsafa wa zamani Plato aliwahi kusema hivi "Ninaomba kuwaambia wanaodhani siasa haiwahusu, moja ya madhara ya kukataa kujihusisha na siasa ni kwamba utaongozwa na watu uliowazidi akili. Na kwa upungufu wao wa akili watafanya maamzi ya kila kitu kinachohusu maisha yako".

Kauli ya Mhe Rais ni kauli ambayo inalengo la kuliweka Taifa pamoja. Mhe Rais bila shaka ameona kuna nyufa ambazo tunashindwa kuyafikia malengo ya millennium tuliojiwekea kutokana na siasa. Ameona kama Taifa hatuna lugha moja kitu kinachoweza kuchelewesha safari ya mapinduzi ya kiuchumi.

Binafsi ninaitazama hoja ya kukutana na Wanasiasa ndio inaweza kuleta majawabu ya mipango yote aliyonayo Rais kwa Taifa hili. Kukiwa na migogoro ya kisiasa ni rahisi kujitengenezea bomu ndani ya nchi kwani Wanasiasa wasiokubaliana na Mambo kadhaa ni rahisi kushirikiana na maadui wa nje kuliangamiza Taifa.

Kama Mhe Rais atafanikiwa kuwakutanisha Wanasiasa wote na kuridhiana inawezekana hata matumizi mabaya ya mitandaoni yatapungua kama si kuisha. Rais wa awamu ya nne alishawahi kukutana mara kadhaa na viongozi wa vyama vya Upinzani ambapo mazungumzo yao yalipelekea Bunge la Katibu.

Hayati Magufuli alikuwa akikutana na viongozi wa vyama vya upinzani katika matukio ya kijamii na katika masuala mahususi lakini hakuwahi kutangaza kwamba atakutana nao kwa ajili ya kujadili masuala ya uongozi wa nchi. Lakini ni Rais aliyewapa nafasi nyingi sana serikalini na hata walijiunga na CCM aliwapa nafasi serikalini.

Viongozi wa vyama vya Siasa huu si muda kuanza kuikosoa hotuba ya Rais, ni muda wa kuanza kutafakari ni Mambo gani mtaenda kushauriana mkiitwa?

Mandela aliwahi kusema "Nimepigana dhidi ya mfumo wa utawala unaowapendelea makaburu, na nimepigana dhidi ya mfumo wa utawala unaowapendela weusi. Nimekuwa na ndoto ya jamii ya kidemokrasia na huru ambayo watu wote wanaishi pamoja kwa mshikamano na fursa sawa. Ni ndoto ambayo nataraji kuiishi na kuitimiza. Lakini, kama itahitajika, hiyo ni ndoto ambayo nimejiandaa kupoteza maisha yangu kwa ajili yake".

Kitendo Cha Mhe Samia kuongea jana kina tafsiri nia njema aliyo nayo kwa ajili ya Taifa. Ana paswa kuungwa mkono ili kujenga Taifa la mshikamono. Hatuna sababu ya kushindana upande wa kukosoa na kuunga, bali tunayo nafasi ya kuyaomba anayofikiria ayatimize.
 
Back
Top Bottom