SoC02 Hili la madarasa ya giza, tufanye kitu kunusuru watoto wetu

SoC02 Hili la madarasa ya giza, tufanye kitu kunusuru watoto wetu

Stories of Change - 2022 Competition

Abeida

Member
Joined
Jul 14, 2022
Posts
13
Reaction score
7
Abeid Abubakar

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu katika habari iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi la Julai 23, 2022 ukurasa wa 23, alinukuliwa akisema kuwa Watanzania wapo hatarini kupata upofu kwa kukosa huduma za macho, huku akiweka bayana kuwa ni watu milioni moja pekee wanaopata huduma hiyo kati ya milioni 12 wanaohitaji huduma za tiba ya macho.

Mpaka anafikia kusema kauli hiyo kiongozi huyu aliyepewa dhamana ya kusimamia sekta ya afya kwa wananchi, ameshaona mwenendo usioridhisha kuhusu afya ya macho nchini.

Wakati Waziri Ummy anatoa kauli hiyo, natazama jambo moja ambalo kwa hakika linapaswa kuchukuliwa hatua za haraka na za makusudi . La sivyo tunaandaa kizazi cha watu watakaokuwa na matatizo ya uoni kwa sasa na hata siku zijazo.

Msomaji umewahi kuchunguza mazingira ya shule nyingi katika maeneo mbalimbali nchini? Mimi ninakupa ushuhuda wa uchunguzi wangu wa siku nyingi katika baadhi ya shule za mkoa wa Dar es Salaam hasa wilaya ya Ilala.

Uchunguzi wangu umeonyesha shule nyingi wanafunzi wanasoma wakiwa kizani kwa sababu ya madarasa yao kuwa jirani mno na miti inayopandwa, majumba ya makazi au ya biashara.

Ni kweli utunzaji wa mazingira hasa upandaji wa miti umekuwa ukisisitizwa mno mashuleni na kwa hakika miti hiyo inatoa mandhari mazuri kwa shule zetu, lakini kwa upande mwingine miti ina athari kwani imekuwa chanzo cha vyumba vya madarasa kuwa na giza. Kibaya zaidi shule zetu nyingi hazina huduma ya umeme ili darasa likiwa na mwanga hafifu, taa ziwashwe kuongeza mwanga.

Tembelea shule mkoani hapa, utathibitisha hiki ninachozungunza. Kama sio miti kuwa jirani mno na madarasa basi majengo. Wanafunzi wanasoma katika madarasa yenye mwanga hafifu, hali inayoweza kuathiri afya ya macho yao na hata walimu.

Tunaweza tukaona sawa leo lakini kwa muda wanaosoma darasa la kwanza hadi la saba, siku tano kwa wiki kwa miaka yote hiyo na baadaye miaka minne ya sekondari, tujiulize ni kwa namna gani watoto hawa wanaathirika?

Yale madarasa aghalabu huwa ni makubwa kwa urefu wa mita tisa kama unavyosema mwongozo wa ujenzi wa madarasa. Sasa fikiria darasa lina giza na mtoto yuko nyuma huku ubao ukiwa mita tisa mbele yake. Huku sio kuharibu uoni wake?

Nimeambatanisha picha mbili nilizopiga katika Shule ya Msingi Kipunguni iliyopo wilaya ya Ilala kuonyesha namna miti ilivyosongamana jirani na madarasa.

Mwalimu mmoja Mwamibi Mnubi baada ya kumweleza hali hiyo alinijibu kwa kusema wao kama walimu wameishazoea hali ya madarasa yao.

"Tunafundisha hivyo hivyo shida zaidi ikiwa hali ya mvua na mawingu ndiyo giza linazidi, alisema kumwambia mwandishi wa makala haya.

Aliongeza kusema: ‘’Tatizo sio miti tu tatizo madirisha madogo inawalazimu watoto kukaa chini ili wawe karibu na ubao. Pia kipindi cha joto hali huwa mbaya sana mchana,watoto wanalowana jasho walimu wanashindwa kusimama darasani kwa muda mrefu, kwani darasa linakuwa na joto kali sana. Inafikia wakati tunawatoa watoto nje ili wapate mwanga na hewa.’’

Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya, Dk Amir Batenga, macho ya binadamu licha ya kuwa na uwezo wa kujibadilisha na kufanya kazi kutegemea na hali ya mwanga ilivyo, lakini inapotokea mwanga huo ukawa mkubwa sana au mdogo sana na mtu akawa eneo hilo kwa muda mrefu, hali hiyo inasababisha macho kufanya kazi ya ziada.

Huku kufanya kazi ya ziada hatimaye ndiko kunakoweza kusababisa majanga ambayo makala haya yanataka yaepukwe. Fikiria mtoto anayesoma katika mwanga mdogo siku tano kwa wiki asubuhi hadi mchana miaka nenda rudi, ni kwa namna gani macho yake yanafanya kazi kwa ziada?

Mmoja wa maofisa elimu niliyemweleza hali hiyo katika Manispaa ya Ilala, Musa Ally alisema kitaratibu darasa huwa linatakiwa kuwa na urefu wa mita tisa.

Sasa fikiria mwanafunzi anayekaa madawati ya nyuma na namna anavyolazimika kutumia nguvu kubwa kutazama ubao ulio mita tisa mbele yake. Hiki ndicho alichosema hapo awali mwalimu Mwamibi kuwa baadhi wanalazimika kwenda mbele kukaa jirani na ubao. Kwa hali hii lazima tukubali kuwa hii ni hatari kwa afya ya macho ya watoto ama kwa sasa au huko baadaye.


Nini kifanyike?

Ni kweli miti ni uhai na inapendezesha mazingira yetu na hata Serikali imekuwa ikihamasisha mazingira ya shule yapendeze, lakini kwa hali hii kuna haja ya kuangalia upandaji wa miti hasa jirani na vyumba vya madarasa ili isiwe chanzo cha kuziba mwanga.

Ikiwa lazima kuwe na miti jirani kabisa na madarasa, basi tuhakikishe yanakuwa na mwanga wa ziada ambao unaweza ukawa ule wa taa. Na hapa sasa lazima shule ziwe na huduma ya umeme.

Tunapozungumza kuwa kuna tatizo la uoni kwa wananchi, inawezekana moja ya sababu ikawa ni hii ya watoto kuanza kuathirika tangu wakiwa shuleni.

Pengine tunaovaa leo miwani kwa sababu ya uoni hafifu, ni kwa sababu miaka mingi iliyopita macho yetu yalipoteza nuru ya kuona kwa sababu ya kusoma gizani shuleni.

Usomaji wa gizani haupo shule hii ya Kipunguni na ile jirani yake ya Kilimani ambazo ziko eneo moja. Hili nimeliona kwa shule kadhaa jijini hapa ikiwamo ya Minazi Mirefu.

Inawezekana kweli macho ya watoto yana nguvu kwa kuona hata kwenye mwanga hafifu, lakini hata kwa maarifa madogo huku ni kuharibu afya yao ya macho hasa kwa siku za mbele wanapokuwa wakubwa. Tuchukua hatua kunusuru watoto wetu.

Abeid Abubakar ni mkazi wa Dar es Salaam anapatikana kwa barua pepe; abeidothman@gmail.com
 

Attachments

  • kip1.jpg
    kip1.jpg
    126.4 KB · Views: 5
  • kip2.jpg
    kip2.jpg
    112.7 KB · Views: 6
Upvote 0
Back
Top Bottom