Hisia za Kielektroniki: Athari za Maisha ya Mitandaoni Tanzania

Hisia za Kielektroniki: Athari za Maisha ya Mitandaoni Tanzania

Joined
Sep 3, 2026
Posts
11
Reaction score
10
Na Hatibu Shemnyama,

Hisia za kielektroniki ni hisia dhahania zinazojitengeneza katika fikra za mtu kupitia maandishi na taswira zinazoonekana kwenye mitandao ya kijamii.

Watu wengi wameathiriwa na hisia za kielektroniki kwa namna mbalimbali. Kuna watu wanaokosa furaha kwa kujilinganisha na maisha ya watu wengine wanaowaona kwenye mitandao ya kijamii. Kuna wanaodharau kazi zao za kawaida kwa kuzilinganisha na kazi za watu wengine wanaowaona kwenye mitandao ya kijamii. Kuna wanaochukia miili yao kwa kujilinganisha na miili ya watu wengine wanaowaona kwenye mitandao ya kijamii.

Pia wapo watu wanaowachukia wengine kwa jinsi tu wanavyowaona kwenye mitandao ya kijamii. Kuna wanaofikiri kwamba wanawapenda watu fulani, kumbe wanatamani tu maisha yao wanayoyaona kwenye mitandao ya kijamii. Kuna wanaofikiri kwamba wanapendwa sana, kumbe kinachopendwa ni umaarufu wao unaoonekana kwenye mitandao yao ya kijamii. Kuna wasiowathamini watu wao wa karibu wanaowajali kwa sababu tu watu hao hawana umaarufu kwenye mitandao ya kijamii.

Na kuna watu wanaojihisi hawana thamani kwa sababu tu hawapewi pongezi na 'attention' kama wanavyopewa watu wengine kwenye mitandao ya kijamii.

Je, na wewe ni mhanga wa hisia za kielektroniki zinazokupa shinikizo linalofanya ushindwe kujithamini kwa kujilinganisha na maisha ya wengine mitandaoni? Usijali, unaweza kupona.

Unachopaswa kufanya ni kuanza kukubali kwamba wewe ni wa thamani sana. Kisha tambua kwamba hakuna mtu mwenye mamlaka ya kupima thamani yako isipokuwa Mungu na wewe mwenyewe.

Na kama upo katika hatua ya maisha ambayo bado haijakidhi matarajio yako, fahamu kwamba unayo nafasi ya kujiboresha na kuendelea kuwa bora bila kumchukia mwingine, bila kujidhihaki wala kujishusha thamani.

Kuna falsafa yangu ambayo inaniongoza katika maisha yangu. Inasema hivi:

“Kama kaburi langu bado halijachimbwa, nina nafasi nyingine ya kufanya chochote katika dunia hii.”

Hata wewe unaweza kuitumia falsafa hiyo katika maisha yako. Na kwa kufanya hivyo, utaweza kujinasua kutoka kwenye hisia hasi za kielektroniki.
 
Back
Top Bottom