Mzee wangu Mohamed
Labda ili wengine wafurahi na waone uko fair hizi historia mara nyingine uwe unazitoa ukiwataja wale wenye majina ya kiyahudi.
Makala zako mara nyingi husifia wale wenye majina ya wafuasi wa Mtume.
Hebu siku moja tuambie mtu mmoja aliyesaidia sana kupambania Uhuru wetu ukimuacha Nyerere.
Asprin,
Kumtaja mtu mmoja aliyesaidia sana katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika ni kazi ngumu sana na naweza kusema haiwezekani.
Haiwezekani kwa kuwa ni tabu kupima kwa uhakika kuwa huyu fulani ndiye.
Ngoja nikupe mfano kwa wazalendo waliokuwa Dar es Salaam.
Hapa nitakutajia majina yao na waliyofanya kila mtu kwa kile alichokuwa na uwezo nacho na hii michango yao baadhi haikuwa ya siri wanachama wote wa TANU wakijua.
1950 kulikuwa na wajumbe wa TAA Political Subcommittee: Dr. Vedasto Kyaruzi, Abdul Sykes, Hamza Mwapachu, Mufti wa Tanganyika Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Said Chaurembo, John Rupia na Steven Mhando.
Katika kamati hii alikuwapo pembeni ingawa jina lake halipo katika orodha ya wajumbe, Earle Seaton mwanasheria aliyekuwa akiishauri kamati hii kuhusu Tanganyika kuwa katika Udhamini wa Uingereza.
Huyu Earle Seaton ndiye aliyeishauri TAA iweke nguvu ya kwenda UNO kuwasilisha madai ya uhuru wa Tanganyika.
Katika kamati hii mjumbe aliyekuwa na heshima kubwa na wafuasi wengi nje ya duru hili la wanasiasa wa TAA alikuwa Sheikh Hassan bin Ameir aliyekuwa na wafuasi Tanganyika nzima na hawa wote walijiunga na TANU kwa wakati mmoja TANU ilipoasisiwa 1954.
Lakini mambo hayaweza kwenda bila fedha.
TAA hadi TANU ilikuwa hapa Dar es Salaam na wafadhili wake wakubwa: John Rupia, Dossa Aziz na Abdul na Aly Sykes.
Abdul Sykes ndiye aliyekabidhiwa kuishi na Nyerere nyumbani kwake Mwalimu alipoacha kazi mwaka wa 1955, Dossa akatoa gari yake kuipa TANU imsaidie Nyerere katika shughuli zake za chama kama President wa TANU.
Kulikuwa na askari wenda kwa miguu, ''foot soldiers,'' waliopita nyumba kwa nyumba kuwashawishi wananchi kujiunga na TANU - Bi. Titi Mohamed, Bi. Tatu Bint Mzee, Hawa bint kwa kuwataja wachache na hawa wanakwenda pamoja na Bantu Group akina Rashid Sisso na wenzake akina Juma Mlevi wahamasishaji umma na walinzi wa viongozi.
Sheikh Hassan mwenyewe akiuza kadi za TANU misikitini nchi nzima alipokuwa anakwenda kwa ajili ya kusomesha.
Abdul Sykes akiuza kadi za TANU Kariakoo Market alipokuwa Mkuu wa Soko, yaani Market Master.
Hii ni Dar es Salaam peke yake akini nchi nzima palipofunguliwa matawi ya TANU wazalendo kama hawa walikuwapo.
Huwezi kusema kuwa Nyerere ndiye aliyepigania uhuru wa Tanganyika peke yake kama ilivyo katika historia au anaweza kupatikana mtu zaidi ya Nyerere aliyepigania uhuru wa Tanganyika.
Swali lako halikukaa vyema limehitaji kutengenezwa.
Nyerere peke yake asingefika popote.
Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anamjua wala hakuwa na fedha za kuendesha chama si wakati wa TAA wala wakati wa TANU.
Umefika wakati historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika iwekwe wazi.
Kuwa ''fair'' ndiyo huku.
Katika picha hiyo hapo chini yuko Bi. Titi Mohamed, John Rupia, Mohamed Jumbe Tambaza na wazee wa Dar es Salaam wana TANU.