HISTORIA YA NENO ZANZIBAR:Ukweli ni kwamba kila kilichopo hapa duniani kina historia yake. Na ifahamike kuwa kabla ya kuja kwa wageni katika bara la Afrika, kila kitu kIlikuwa na jina lake. Na majina mengi yaliyokuwepo na mengine bado yalikuwa na huhusiano wa karibu sana na jamii za kiafrika.
Lakini mara baada ya ujio wa wageni kulikuwa na utajaji mpya wa baadhi ya maeneo . Na hii ilisababishwa na wageni kuwa na taaluma ya uandishi. Na zaidi ya hapo kulikuwa na maeneo ambayo yalipata majina mengi kwa wakati tofautitofauti kulingana na ujio wa wageni. Mfano ,mzuri ni kisiwa cha Zanzibar.
Hapa inatupasa tuelewe kuwa tunachokiangalia hapa ni neno Zanzibar na habari za Unguja tutaangalia kwa upande mwingine. Ifahamike kuwa wakazi wa kwanza kuishi kisiwa cha Zanzibar ni Wabantu, na kwa mujibu wa Prof. Chami aliyefanya tafiti zake Zanzibar alitoa ushahidi wa uwepo kwa makabila ya kibantu katika maeneo hayo kabla ya wageni miaka ya 600 BK/BM.
Neno Zanzibar lina maana ya eneo lote la Pwani linalopatikana kuanzia kusini mwa Somalia( Mto Juba) hadi maeneo ya Msumbiji. Kabla ya kuitwa Zanzibar, hapo mwanzoni kwa mujibu wa wageni walipaita Zanji/Zenji/Zinji kwenye miaka ya 1200 bila kuongeza “Bar”, wakiwa na maana ya Watu Weusi.
Na kwenye vita vya Kiislamu huko Asia miaka ya 700, kulichukuliwa Waafrika zaidi ya 400 kutoka Pwani ya Zanji na walifahamika kwa jina la Wazanji. Kwa uchanganuzi tu neno zanji kwa Kiswahili ni Zanchi yaani nchi ya Za. Ikiwa na maana ya Za- maeneo yote yaliyozunguukwa bahari ya Hindi. Na neno Chi au Nji lina maana ya ardhi.
Kwa hapo tukapata maana ya watu weusi walikuwa wakiishi kwenye ardhi (kisiwa) kilichozunguukwa na bahari ya Hindi. Na baadae kwenye maiaka ya 1200/1300 Waarabu walitaka kutofautisha baadhi ya watu wakaongeza neno “Bar” ikiwa na maana ya ardhi inayomilikiw na wa Zanji. Na hivyo kupata Zanjibar au Zanjbar.
Na hata ushahidi wa maandiko ya Ibn Hawqal yalionesha kuwa mji huo ulifahamika kama Zangbar kutokana na maandishi na matamshi yake. Na hata kwenye karne ya 12 sawa na miaka ya 1100 kwenye maandiko ya Al-Idris aliandika Zangbar ikiwa na maana ile ile.
Na hata Wachina walipofika maeneo hayo waliyatambua kwa jina la (Ts’ong-pa) ikiwa na maana ya Zangbar. Na mpaka Wareno walipofika maeneo hayo kama Vasco Da Gama na Marco Polo walitambua eneo kama Unguja. Hivyo neno Unguja lilikuja kufahamika mara baada ya ujio wa Wareno.
Tukiachan na habari za Unguja, turudi kwenye suala zima la Zangbar. Historia inafafanua kuwa Zanzibar ilikuwa chini ya uangalizi wa Mwingereza kuanzia miaka 1890, na wakati huo Wazungu walipatambua kama Zanzibar, ili kurahisisha matamshi ya kiingereza. Zanzibar ilipata uhuru mwaka 1963 na uhuru huo ulikuwa wa wachache. Mnamo miaka ya 1964 kulifanyika mapinduzi kisiwani hapo. Na mwaka huohuo mwezi wa 4, Zanzibar iliungana na Tanganyika na kuunda Tanzania.
Mchakato ulikuwa hivi, zilichuliwa herufi 3 za mwanzo kutoka kwenye kila neno, yaani Tan-kutoka Tanganyika na Zan –kutoka Zanzibar na kupata Tan+zan-. Na mwisho kuchua herufi zilizobakia yaani kutoka Zanzibar tukapata –a- na Tanganyika tukapata –i- na mwisho tukapata –ia- na kuzaa neno Tanzania. Na hii ilifanywa na Hayati, Julius Kambarage Nyerere na Hayati Aman Abeid Karume. Ukweli ni kwamba licha ya changamto nyingi muungano huu una faida sana kwa nchi hizi.
SOMA HAPA CHINI NA PICHA YA IQBAL MBUNIVU
Jamvi La Utubusara
April 18, 2016 ·
...
Mohammed Iqbal Dar ndiye aliyebuni jina zuri la Tanzania. Vijana wengi pengine hata wazee hawamjui wala kusoma historia yake kwani haifahamiki.
Mwandishi mmoja wa Redio Safari ya Mtwara Alphonce Tonny Kapelah alipata bahati ya kuonana ana kwa ana na kuzungumza na Mohammed Iqbal Dar akajieleza:
Swali: Uliingiaje katika shindano la kubuni jina la nchi?
Jibu: Siku moja nilikuwa maktaba nikijisoma Gazeti la Tanganyika Standard ambalo siku hizi linaitwa Daily News, mikaona tangazo lililosema: “Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unafahamika kama Republic of Tanganyika and Zanzibar jina likaonekana refu sana. Kwa hiyo wananchi wote mnaombwa kushiriki kwenye shindano la kupendekeza jina moja litakalozitaja nchi zote mbili yaani Tanganyika na Zanzibar.”
Swali: Baada ya kuona tangazo hilo ukafanyaje?
Jibu: Niliamua kuingia kwenye shindano hilo.
Swali: Ulianzaanzaje kubuni jina linalofaa?
Jibu: Nilichukua karatasi nikaandika kwanza Bismillah Raahman Rahimu hii ni kutokana na imani ya dini yangu. Baada ya hapo nikaandika jina la Tanganyika kisha nikaandika Zanzibar halafu nikaandika jina langu la Iqbal halafu nikaandika jina la Jumuiya yangu ya kidini ya Ahmadiya. Baada ya hapo nikamrudia tena Mwenyezi Mungu, nikamuomba anisaidie ili nipate jina zuri kutoka katika majina hayo niliyokuwa nimeandika. Baada ya hapo nilichukua herufi tatu kutoka jina la nchi ya Tanganyika yaani TAN na kwa upande wa Zanzibar nikachukua herufi tatu za mwanzo ZAN, kisha anikaunganisha nikapata jina TANZAN.
Swali: Mbona halijakamilika?
Jibu: Nami niligundua kuwa halijakamilika hivyo nikachukua herufi ya kwanza ya jina langu ambayo ni herufi I katika jina langu la Iqbal kisha nikachukua herufi ya kwanza A ya jina la dini yangu yaani Ahmadiya. Niliandika jina la awali la TANZAN nikaunga na herufi hizo likawa TANZANIA nikaona ni jina kamili tena zuri.
Swali: Ulipopata jina hilo la Tanzania ulifanyeje?
Jibu: Kabla ya kulipeleka kunakohusika serikalini nilifanya utafiti mdogo na kugundua kuwa nchi nyingi za Afrika majina yao yanaishia na IA kwa mfano EthiopIA, ZambIA, NigerIA, TunisIA, SomalIA, GambIA, NamibIA, LiberIA, MauritanIA. Baada ya utafiti huo nikapendekeza na kuamua kwamba jina TANZANIA ndilo litumike kuwakilisha nchi hizi mbili yaani Tanganyika na Zanzibar. Kwa maana hiyo jina TANZANIA limezaliwa kutoka katika majina manne ambayo ni Tanganyika, Zanzibar, Iqbal na Ahmadiyya.
Swali: Ikawaje?
Jibu: Baada ya kujiridhisha kuwa jina hilo linafaa nikalituma kwenye kamati ya kuratibu shindano. Baada ya muda mwingi kupita baba yangu Dk. Dar alipokea barua nzito kutoka iliyokuwa Wizara ya Habari na Utalii ilisomeka kama ifuatavyo:
“Utakumbuka kuwa miezi michache iliyopita ulituandikia kutupa ushauri kuhusu jina jipya la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar….ili iitwe Tanzania.
“Nafurahi kukuarifu kuwa mshirikiane zawadi ya sh.200 iliyoahidiwa na leo nakuletea cheki ya sh.12/50 ikiwa ni hisa yako katika zile sh. 200.
Nashukuru sana kwa jitihada ya kufikiri jina la jamhuri yetu.”
Barua ikasainiwa na Idrisa Abdul Wakil Waziri wa Habari na utalii kipindi hicho.
Swali: Kwani washiriki mlikuwa wangapi?
Jibu: Tulikuwa watu 16 lakini mimi nikaibuka mshindi lakini alijitokeza mtu mmoja, Yusufal Pir Mohammed aliyedai naye alishinda, hata hivyo, alikosa sifa baada ya kushindwa kutoa barua ya uthibitisho na kupongezwa kama nilivyoandikiwa mimi na serikali, sasa nikapewa cheki ya shilingi 200 na zawadi ya ngao. Nilileta mabadiliko makubwa sana ya jina jipya. Ninachosikitika ni kuwa mchango wangu bado Watanzania hawauthamini lakini mimi naipenda Tanzania na najivunia kuwa Mtanzania ila naamini kuwa siku moja ukweli utajulikana.
Swali: Hivi sasa unaishi wapi?
Jibu: Kwa sasa naishi Uingereza kwa kuwa huko ndiko nilipata kazi eneo la Birmigham b35 6ps UK, Dar es Salaam House, 18 Turnhouse Road.
Swali: Unaweza kutueleza historia yako kifupi?
Jibu: Mimi Mohamed Igibal Dar ni Mtanzania mwenye asili ya Kihindi, nilizaliwa mkoani Tanga mwaka 1944. Baba yangu alikuwa daktari wa binadamu mkoani Morogoro alikuwa anaitwa Dk. Tadar na alihamia Tanganyika kutoka India mwaka 1930. Nilipata elimu ya msingi mkoani Morogoro katika Shule ya Msingi H.H Agha Khan, kwa sasa ni shule ya serikali.
Baadaye nilijiunga na Shule ya Mzumbe nikasoma kidato cha kwanza mpaka cha sita.