KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU KUELEKEA ETHIOPIA
SEHEMU YA TATU
Rais mpya wa Rwanda Bw. Juvenal Habyarimana aliingia rasmi madarakani siku ya Tare 5 July mwaka 1973. Kabla ya hapo alikuwa ni Jenerali katika jeshi la Rwanda akishikilia cheo cha Mnadhimu Mkuu wa jeshi. Mapinduzi yaliyofanywa na Habyarimana kumuondoa madarakani Rais Gregoire Kayibanda hayakuwa mapinduzi ya kumwaga damu.
Mapinduzi haya yalipokelewa kwa shangwe na vifijo hasa maeneo ya mijini nchini Rwanda. Rais aliyepinduliwa, Bw. Kayibanda ilifika kipindi alianza kuchukiwa mno na wananchi kutokana na kushindwa kabisa kuituliza Rwanda na kuiletea maendeleo badala yake aliendeleza visasi dhihi ya Watusi. Hii ilisababisha Rwanda kutengwa na majiranio zake, hasa jirani yao muhimu zaidi, nchi ya Uganda ambayo ilikuwa na Watusi wengi wanaoishi nchini humo. Hii iliathiri hata maendeleo ya Kiuchumi ya Rwanda.
Hivyo basi kitendo cha Jererali Jevenal Habyarimana kumuondoa madarakani Rais Kayibanda kilipokelekwa kwa furaha na wananchi wengi na Habyarimana alionekana kama shujaa.
Japokuwa nimeeleza kuwa mapinduzi yaliyomuingiza madarakani Habyarimana hayakuwa ya umwagaji damu, lakini kati ya mwaka 1974 mpaka mwaka 1977 takribani watu hamsini na sita, hasa wale ambao walikuwa na nyadhifa za juu kwenye serikali iliyopita ya Kayibanda waliuwawa kwa maelekezo ya Habyarimana mwenyewe huku Rais aliyeondolewa madarakani Gregoire Kayibanda akifariki mwaka 1976 akiwa gerezani kwa sababu inayoelezwa ilitokana na kunyimwa chakula kwa muda mrefu.
Baada tu ya kuingia madarakani Habyarimana alivifuta vyama vyote vya siasa nchini humo akieleza kuwa hataki Rwanda iendekeze majibishano ya kisiasa kila siku badala ya “kuchapa kazi” na mara nyingine akituhumu vyama vya siasa kutumika na maadui wa Rwanda ili kuvuruga taifa. Mwanzoni wananchi karibia wote waliunga mkonmo msimamo wake huu. Lakini ajabu ni kwamba mwaka uliofuata baada ya kuingia madarakani, yaani mwaka 1975 Rais Juvenal Habyarimana aliunda chama chake cha siasa ambacho alikiita Mouvement Revolutionnaire National pour le Developpement (MRND) na kutangaza kwamba hicho ndicho kitakuwa chama pekee cha siasa nchin Rwanda.
Mwanzoni Habyarimana alipendwa na watu wa makundi karibia yote, yaani Wahutu na Watusi. Wahutu walimpenda kwa kuwa alikuwa ni Muhutu mwenzao na Watusi walimpenda kwa kuwa mwanzoni mwa uongozi wake baada ya kumpindua Kayibanda, alipiga marufuku sera ambazo mtangulizi wake alizitengeneza kwa ajili ya kuwapendelea Wahutu pekee. Watusi walifurahishwa sana na hatua hii. Kwa upande wa Wahutu wenzake japokuwa suala hili liliwaudhi lakini hapa mwanzoni walimvumilia na kuendelea kumuunga mkono kwa kuwa alikuwa ni mwenzao (Muhutu).
Kwa muda wote huu serikali ilikuwa chini ya jeshi, yaani hakukuwa na serikali ya kiraia. Jeshi ndilo lilikuwa serikali nay eye Habyarimana akiwa kiongozi mkuu wa nchi. Lakini kufika mwaka 1978 kulifanyika mabadiliko mengine ya kikatiba ambayo yalitaka kurejea kwa serikali ya kiraia. Kwa hiyo mwaka huo ukaitishwa “Uchaguzi Mkuu”. Haukuwa uchaguzi mkuu haswa kwa maana ya uchaguzi mkuu kama ambavyo unapaswa kuwa, kwa maana ulikuwa ni kiroja cha kuchekesha ambazo kilitoa taswira kwamba kuna harufu ya shari iliyo mbele.
Ni kwamba kwa kuwa vyama vyote vya siasa vilipigwa marufuku nchini humo, hivyo basi MRND, chama cha Juvenal Habyarimana ndicho chama pekee ambacho kilishiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huo 1978 kwa kusimamisha wagombea na katika nafasi ya Urais kulikuwa na mgombea mmoja tu, Juvenal Habyarimana.
Siku ya Desemba 24 mwaka huo 1978 matokeo ya uchaguzi yalitangazwa ambapo Habyarimana alishinda ‘kwa kishindo’ akipata 98.99% ya kura zote na kuapishwa kuwa Rais wa Rwanda kwa muhula wa miaka mitano. Uchaguzi uliofuata miaka mitano baadae, yaani mwaka 1983 kwa mara nyingine tena, MRND kikiwa chama pekee cha siasa killichoshiriki uchaguzi huo na katika nafasi ya Urais Juvenal Habyarimana akiwa mgombea pekee, alipata tena ‘ushindi wa kishindo’ ambapo siku ya Desemba 19 matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa Habyarimana alipata ushindi wa 99.97% ya kura zote zilizopigwa. Kama hiyo haitoshi, miaka mingine mitanao tena baadae, yaani mwaka 1988 siku ya Desemba 19 matokeo yalitangazwa na kumpa tena Habyarimana ushindi wa 99.98% ya kura zote zilizopigwa huku MRND kikiwa chama pekee kilichoshiriki uchaguzi na Habyarimana akiwa mgombea peke wa nafasi ya Urais.
Watu wenye hekima na wanao ona mbali walianza kuhisi joto ambalo lilikuwa na dalili ya kurudi tena ndani ya Rwanda .
Habyarimana hakuishia hapo tu, bali pia wafuasi wake wallianzisha utaratibu wa kufundisha raia mitaani kwa lazima nyimbo na tungo zilizotungwa kwa ajili ya kumsifu Rais Habyarimana pamoja na staili za kucheza nyimbo hizo. Katika mikutano yake ya siasa raia wa Rwanda walitakiwa kuimba nyimbo hizi za kumsifu na kucheza kwa staili ya kufanana kama ambavyo walikuwa wamefundishwa.
Kwa kifupi Rais Juvenal Habyarimana aligeuka kutoka kuwa ‘malaika wa ukombozi’ ambaye Warwanda walihisi ameshushwa labda kutoka juu na bila kupindisha maneno Habyariamana sasa alikuwa ni Dikteta.
Udikteta wake ulikuwa ni udikteta haswa… sio udikteta uchwara! Ilikuwa ni ngumu kuchora mstari kati ya chama chake cha MRND na pia nghumu zaidi kuchora mstari wa ukubwa wa madaraka yake ndani ya chama tawala cha MRND. MRND ndio ilikuwa serikali na Habyarimana ndiye alikuwa MRND. Kwa hiyo yeye ndiye alilkuwa serikali na yeye ndiye alikuwa chama tawala.
Ofisi zote za serikali pia zilifanya kazi kama ofisi za MRND. Katika serikali za mitaa, ‘Maafisa Watendaji’ wa kata au vijiji au mitaa pia ndio walifanya kazi kama makatibu wa chama.
Kadiri ambavyo Habyarimana alikuwa anajivika utukufu na kukoleza makali yake ya udikteta ndivyo ambavyo hata watu wa kabila lake, Wahutu walianza kumchukia.
Kama dikteta mwingine yeyote yule duniani, naye akaanza kufanya makosa ya kipuuzi kabisa ya kimkakati. Ati ili kuwafurahisha watu wa kabila lake, Habyarimana taratibu akaanza kurejesha sera za mtangulizi wake ambazo zilikuwa zinawabagua Watusi. Kwa mfano kwenye udahili wa vyuo vikuu au ajira za serikali, walirejesha vipengele ambavyo moja kwa moja vilikuwa vinamnyima fursa Mtusi.
Hili lilikuwa ni kosa kubwa kwake kwani watu wa kabila lake tayari walikuwa ‘watembukiwa nyongo’, wengi walikuwa hawamtaki na hata Watusi ambao walikuwa wanamuunga mkono nao wakamchukia kutokana na kurejesha sera za kibaguzi. Kwa kifupi alikuwa anaenda kinyume na misingi na sababu ambazo alizitumia kuhalalisha mapinduzi yake mwaka 1973 na vitu ambavyo vilifanya Wahutu na Watusi kwa pamoja kumpenda.
Tofauti na ambavyo nchii ilitulia mara baada ya Habyarimana kumpindua Kayibanda, lakini kutokana na udikteta wake na kutokubalika tena kwa wananchi, ‘order’ ilianza kupotea mitaani na taratibu chuki za kikabila ambazo zilikuwa zinawafurukuta watu zikaanza kumea tena upya.
Lakini hapa ndipo ambapo msemo wa “kila mwanaume mwenye mafanikio nyuma yake kuna mwanamke imara” ulidhihirika.
Hapa nieleze kidogo japo kwa uchache lakini kwa mawanda…
Katika kipindi chote cha uongozi wa Rais Habyarimana kulikuwa na minong’ono kwamba maamuzi mengi sana yalikuwa yanafanyika kwa ushawishi wa mke wake aitwaye Agathe Kanziga Habyarimana. Minongono hii ilidhihirika ukweli wake katika kipindi hiki ambacho kiwango cha kukubalika cha Rais Habyarimana kilifikia chini kabisa nchini Rwanda.
Kwa kifupi ni kwamba; Agathe anatoka kwenye familia ambayo ukoo wao walikuwa ni watawala wa eneo la magharibi mwa Rwanda kwa miaka mingi sana sana. Mizizi na mataji wa kisiasa wa familia yake ndio ambao inasemekana kumsaidia kwa kiwango kikubwa Habyarimana kuingia madarakani na kukubalika japo alikuwa kiongozi wa kijeshi asiye na umahiri mkubwa wa medani za siasa.
Hivyo basi, pia katika kipindi hiki cha mumewe kutokukubalika na wananchi ndani ya Rwanda na hata viongozi wenzake wa kiserikali kuanza kumfitini, Agathe alichukua hatua ya kuhakikisha madaraka ya mumewe hayatetereki. Agathe akaunda makakti na kufanya uratibu wa weledi wa hali ya juu sana mpaka kuanzishwa kwa jumuiya ya siri (ilikuwa ya siri mwanzoni) ambayo ilijumuisha Wahutu wenye ushawishi mkubwa ndani ya Rwanda na wenye msimamo mkali dhidi ya Watusi. Jumuiya hii iliitwa ‘Akazu’.
Kwa hiyo Akazu iliundwa na ndugu wa Habyarimana ambao aliwajaza kwenye nyadhifa za juu serikalini, ndugu wa Agathe na marafiki zao wenye ushawishi mkubwa.
Agathe Kanziga Hibyarimana
Lengo la jumuiya hii ilikuwa ni nini?
Akazu kama nilivyoeleza kuwa iliundwa na watu wenye ushawishi kwenye jamii ya Rwanda (hasa kwa Wahutu)lakini wote walikuwa ni Wahutu wenye msimamo mkali. Kama ambavyo wenyewe walijipambanua kwenye nyaraka zao za siri kwamba lengo la lilikuwa ni kuona “Rwanda with zero Tutsi” (Rwanda yenye Watusi sufuri). Hii ndio sababu ya muda mwingine mafungamano ya jumuiya hii kuitwa ‘zero networks’. Kiu yao kuu ilikuwa ni kuona ‘watesi’ wao wa kale, Watusi hawapo ndani ya ardhi ya Rwanda.
Sasa kwa nini Habyarimana afungamane na watu wa dizaini hii? Nimeeleza hapo awali kwamba ushawishi wa Habyariamana kwa wananchi ulidodorora kupitiliza. Pia kule mwanzoni kabisa nilieleza kwamba, Wahutu ni 84% ya Wanyarwanda wote. Kwa hiyo ili uweze kuitawala Rwanda ni vyema kuhakikisha kwamba unaishika mioyo ya Wahutu. Lakini Wahutu hawa tayari walikuwa wametumbukiwa nyongo dhidi ya Habyarimana… kwa hiyo mkewe alianzisha mafungamano haya na Wahutu hawa wenye ushaiwshi mkubwa japo wana misimamo mikali kwa lengo la kuiteka tena upya mioyo ya Wahutu. Pia watu hawa wa Akazu ilikuwa kwa faida kwao kufungamana na Rais Habyarimana ili kushawishi kutungwa kwa sera za kuwabagua Watusi.
Uwepo wa jumuiya hii ya Akazu san asana iliwasaidia Wahutu wenye msisimamo mikali kufanikisha sera zao na chuki yao dhidi ya Watusi lakini hakuwa na manufaa sana kwa Habyarimana kwani ushawishi wake uliendelea kudorora na kuambulia kuungwa mkono mtaani na Wahutu wenye misimamo mikali pekee huku sehemu kubwa ya jamii ya Rwanda ikiwa kinyume chake.
Nilieleza pia hapo mwanzo kuhusu vikundi vidogo vidogo vya waasi wa Kitusi walioko kwenye ukimbizi nchi za jirani na Rwanda vilivyokuwa vimebatizwa jina la ‘Inyezi’ (cockroaches (mende)) kufanya mashambulio ya mara kwa mara bila mafanikio yoyote. Lakini mwanzoni mwaka 1973 Habyarimana alipochukua nchi hali itulia kidogo na hata Inyezi walikuwa kimya. Lakini baada ya Habyarimana kukengeuka, tena kukengeuka kwa hali ya juu na mateso kwa watusi kurudi… Inyezi walianza tena mashambulizi yao.!!
Safari hii vikundiu hivi vilikuwa na dira madhubuti na thabiti zaidi. Walitaka kukomesha milele mateso dhidi ya Watusi nchini Rwanda.
Mfano mzuri wa Watusi hao ambao walikuwa wamejiapiza kukomesha mateso hayo ya ndugu zao nchini Rwanda walikuwa ni wale waliokuwa wanaishi uhamishoni nchini Uganda. Hawa walikuwa na dira madhubuti, weledi na morali ya kuwaokoa ndugu zao Watusi ndani ya Rwanda.
Pale Uganda kulikuwa na maelfu kadhaa ya Watusi ambao walikuwa na morari hiyo ya kukomesha mateso ya ndugu zao waliosalia Rwanda na kuondoa uongozi gandamizi na wa kidikteta. Lakini kati ya hawa maelfu wote, kulikuwa na Watusi wawili ambao walikuwa muhimu zaidi, walikuwa na morarli zaidi na weledi zaidi. Watusi hawa wawili naamini historia yao itabakia hata miaka mia tatu kutoka leo hii. Nawaongelea Paul Kagame na Fred Rwigyema.
Nafahamu wengi wamesimulia mengi kuhusu Mauaji ya Kimbari y Rwanda ya mwaka 1994, na hata makala hii ndilo lengo lake kuu kujadili tukio lile la kihistoria. Lakini tangu mwanzo nimeanzia mbali tangu kuanzishwa kwa Taifa la Rwanda karne kadhaa zilizopita nikiwa na lengo hasa la kuonyesha kiini cha mgogoro wa Wahutu na Watusi ni upi na walifikaje kwenye Kimbari ya mwaka 1994. Katika kujadili kwangu huku kiini cha mgogoro kabla sijajitosa miguu yote kuongelea mauaji yenyewe ya mwaka 1994, sitakuwa nimekata kiu kama sitawaongelea watu hawa wawili na chimbuko lao na kuibuka kuwa wakimbizi wenye ushawishi zaidi. Paul Kagame na Fred Rwigyema. Pia sitakuwa nimekata kiu kama sitochambua ni kwa namna gani Paul Kagame na Fred Rwigyema wakiwa bado ni “wakimbizi” nchni Uganda lakini waliweza kuiweka kiganjani mwao serikali ya Rais Yoweri Musseveni. Sitakuwa nimekata kiu kama sitaeleza ‘ufundi’ waliotumia mpaka kupata nyadhifa ndani ya baraza la mawaziri la Uganda wangali bado ni “wakimbizi”! lakini pia sitakuwa nimekata kiu kama sitoeleza namna ambavo waliunganisha Watusiu mia tano tu, na kuazisha harakati za kijeshi ambazo zilikuja kuling’oa madarakani jeshi la Kihutu lenye maelfu ya maafisa wa kijeshi na silaha za kisasa.
Paul Kagame enzi hizo
Fred Rwigyema
Kwa wanaokumbuka, nilipokuwa nachambua “Operation Entebbe” iliyofanywa na jeshi la Israel kuokoa raia wao walioshikiliwa mateka nchini Uganda kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe, mwishoni mwa ile makala niliuliza swali, Kwamba oparesheni ile ilifanywa na jeshi la Israel mwaka 1976 ndani ya ardhi ya Uganda, baada ya hapo mahusianio ya Uganda na Israel yalidorora mno. Miaka miwili baadae ndipo sisi Tanzania majeshi yetu yalivamia Uganda na kumtoa Idd Ami madarakani nakukimbilia uhamishoni mpaka mwisho wa maisha yake. Nikauliza, je tunafahamu kuna uhusiano gani kati ya Operation Enntebbe ya Waisrael na Vita ya Kagera? Katika makala hii nitagusia kiduchu jawabu la swali hili. Lakini sitaishia hapo tu bali pia tutajadili ushiriki wa Paul Kagame na Fred Rwigyema kwenye vita ya Kagera.!! Yes, Vita ya KAgera…na si vita ya Kagera tu bali pia uhusika wao katika harakati za FRELIMO nchini msumbuji.! Natamani tuweze kufahamu kinagaubaga kabisa kuhusu mnyororo uliopelekea kukatikia kwenye mauaji yale ya 1994.
Lakini pia, tutajadili namna ambavyo Paul Kagame alifunzwa na kufundwa na Idara yetu ya Usalama wa Taifa (kabla ya kuanza kuitwa TISS) na hatimaye kuwa ‘Jasusi’ mbobezi wa daraja la kwanza vile ambavyo yuko sasa.!
Nimeeleza hapo juu kwamba, lengo kuu la makala hii ni kujadili mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 lakini nimeanzia mbali tangu historia ya Taifa la Rwanda kwa makusudi kabisa ili kuonyesha kiini cha tatizo. Kwa sababu mauaji ya 1994 ni “Matokeo” ya tatizo kubwa la muda mrefu lenye mzizi ya karne kadhaa nyuma ambayo mizizi hiyo ilikuja kumea mwaka 1994. Kwa hiyo kabla siajajadili tukio lenyewe la 1994 nataka tufahamu mnyororo wa matukio muhimu niliyoyaeleza hapo juu kwamba kiu haitakata kama sitayajadili. Lakini pia kuna msululu wa wahusika na matukio ambayo vitabu vya historia kwa makusudi au kwa kutokuwa na uelewa nayo hayasemwi (naamini hayasemwi kwa makusudi kabisa).
Katika sehemu ya nne, nitajadili, nitachambua na kuelezea wahusika, mfululizo wa matukio na yale ambayo yalitokea ‘nyuma ya pazia’ mpaka kufikia mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 yaliyogharimu maisha ya watu karibia milioni moja ambayo damu yake mpaka leo hii bado inalia kwenye ardh ya Rwanda na nyingine ikiendelea kutiririka kwenye mifereji ambayo wauaji wao walisema “mifereji iendayo Ethiopia.!”
Itaendelea…
The Bold
To Infinity and Beyond
0718 096 811 (Whatsapp only)
Note: Tafadhali naomba tujitahidi kunifollow na kusubscribe kwenye uzi. Tag hazifanyi kazi bado JF nadhani wanashughulikia. Kwa hiyo nifollow ili upate notification kila ninapo post kitu kipya.
Pia group la Whatsapp kuna malipo ya Tshs. 5,000/- kwa mwezi
Shukrani.