WilsonKaisary
JF-Expert Member
- Apr 4, 2017
- 392
- 949
Sanamu ya Askari au Askari Monument ni sanamu iliyopo kwenye kitovu cha jiji la Dar es salaam kwenye mahali ambapo mitaa ya Samora na Azikiwe (zamani: Maktaba) zinakutana. Sanamu inamwonesha Askari Mwafrika katika sare ya Kijeshi, Jeshi la King's African Rifles la wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) akishika bunduki yenye kisu (sime) cha kando na kutazama upande wa bahari.
Sanamu hiyo iliyowekwa katika eneo hilo mwaka 1927, ni moja kati ya tatu zilizochongwa huko London na Mchongaji James Alexander Stevenson kama kumbukumbu ya Askari na Wapagazi Waafrika waliopigana katika vita hivyo katika Afrika ya Mashariki kati ya Uingereza na Ujerumani ambao wengi wao walikufa.
Sanamu nyingine mbili zilipelekwa Nairobi, Mombasa.
Chini ya Sanamu hii pana Maandishi ya kumbukumbu kwa Kiingereza na Kiswahili kilichondikwa kwa herufi za Kiarabu na herufi za Kilatini pia. Maneno yake kwa Kiswahili ni kama yafuatayo:
"Huu ni Ukumbusho wa Askari Waafrika wenyeji waliopigana katika Vita Kuu na ni Ukumbusho pia kwa Wapagazi ambao walikuwa miguu na mikono ya majeshi. Ni Ukumbusho pia kwa watu wote waliotumika wakafa kwa ajili ya Mfalme na nchi yao katika Afrika ya Mashariki kwenye Vita Kuu toka mwaka 1914 mpaka 1918. Ukipigania nchi yako ujapo umekufa watoto wako watalikumbuka jina lako."
Sanamu ya askari ya Dar ilichukua nafasi ya sanamu nyingine iliyosimkwa mwaka 1909 kwa kumbukumbu ya Meja Hermann Von Wissmann, Gavana wa pili wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, ambayo ilibomolewa na Waingereza walipoiteka Dar es Salaam mwaka 1916.
Na ndio asili ya jina "Picha ya Bismini" kwani Wamatumbi walishindwa kutamka "Wissmann"
Baada ya kumteka na kumyonga Abushir, mtawala/sultani wa Pangani Tanga, Von Wissman alirejea Ujerumani na kisha baadaye kuteuliwa kuwa Gavana wa Nchi zilizokuwa chini ya Ujerumani za Afrika Mashariki (German East Africa). Alitwaa Dar es Salaam na Pwani nzima, japo alikaa muda mchache Dar es Salaam.
Gavana huyu alifanya utafiti wa kutafuta ni wapi kitovu cha mji wa mji wa Dar es Salaam. Yaani katikati mwa mji kwa vipimo, ndipo alipogundua eneo lile pale Posta na kisha akaagiza pajengwe bustani na Sanamu lake likasimikwa. Inadaiwa pale ndipo palikuwa katikati mwa Dar es Salaam miaka ile.
Inaaminika ndiye aliyetoa wazo la kutengeneza ramani ya kujenga makambi ya wapiganaji ama wanajeshi wa Jeshi la Ujerumani eneo ambalo lilikuwa likiitwa Carrier Corps (Waswahili wakaita Keriakoo/Kariakoo). Ndio maana utaona mitaa ya Kariakoo imenyooka na kujengeka vizuri. Ilikuwa makambi ya wanajeshi.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyopiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 ambapo Waingereza walishinda na kuchukuwa koloni la Tanganyika, mwaka 1916 ndipo Sanamu la Bwana Herman Von Wissman liliondolewa na likawekwa Sanamu la sura ya Askari Mweusi mwaka 1927 kama ishara ya kuthamini mchango wa Askari Waafrika waliopigana kwenye Vita hivyo.