Wala si ulimbukeni, ni kukosa kwako kuelewa zaidi ya mambo yaliyozoeleka. Kwani kufikiri nje ya mazoea (boksi) kunahitaji ubunifu na uthubutu. Vinginevyo kwako hakuna kinachowezekana. Maelezo ya msingi ni kuwa masuala ya reli zilizopo, barabara, shule, maji, nakadhalika hayastahili kuwa kwenye ajenda ya mgombea uraisi kwani ni ya kawaida. Haina maana kuzungumzia vitu ambavyo raisi yeyote atakayechaguliwa atavitendea kazi. Mgombea anatakiwa kuzungumza vile ambavyo vitamuwezesha kujipambanua na wagombea wengine. Anatakiwa atoe maono ambayo yatatufanya tujue kuwa asipochaguliwa tutakosa 1,2,3
Si kuwa na rais ambaye akiwepo au asipokuwepo yote sawa tu. Wala haina maana kuwa ukianzisha mradi mpya wa reli basi ya zamani lazima ife. Reli inayozungumziwa, hakika ni mpya na ya moja kwa moja kutoka Dar hadi Mwanza. Huwezi ukawa na vituo lukuki njiani kwa treni ya kasi inayozungumzwa.
Wala si lazima reli hiyo ipitie mikoa uliyoitaja, kwani mikoa hiyo nayo inaweza kuwa na miradi kama hiyo. Mradi huo hauzuii kuigwa sehemu nyingine. Unapokuwa na jambo jipya lazima uwe na pa kuanzia. Kwa maelezo yako unakiri kwa
limbukeni kuwa kitekinolojia inawezekana na imeshafanyika kwingine duniani kwa mafanikio. Ila kwa mawazo yako pia unaamini kuwa kwa vile hapa ni Tanzania hiyo haiwezekani. Hiyo ndiyo tofauti kubwa iliyopo kati ya wanaoamini kuwa wanaweza na wa aina yako ambao mnaamini kuwa haiwezekani kufanya chochote. Utawala huu kama ungekuwa ndio unaongoza enzi za kujenga reli ya TAZARA basi akina Kibunango wangeshauri iachwe kwani haiwezekani na inapita porini bila kujua kwamba porini kwa leo (2010) ndiko mjini ifikapo 2030.
[Ukipima umbali huo moja kwa moja toka kwenye ramani, utapata kilometa 850.20 hivi. Na sijawahi kuona reli iliyoonyoka toka pointi A hadi B kama ambavyo wewe unavyotaka kutuambia hapa!]
Umbali kutoka Mwanza hadi Dar usikupe shida. Kwa treni za moja kwa moja (ambazo ziko duniani) kama alivyoainisha mtoa kiroja ni kati ya 250 hadi 400 km kwa saa. Kwa hiyo hakuna ubishi kuwa hizo km 1,000 (kwa njia mpya ya mkato na kona za lazima) zinawezekana kabisa kwa saa tatu. Tukubaliane mpaka hapo. Kama nilivyoeleza hapo awali huu ni mpango wa miaka 15. Katika kipindi hicho teknolojia inayoongezeka kila uchao itakuwa na majibu mazuri zaidi.
[Reli ya kati imepita katika mikoa zaidi ya minne(Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, na Mwanza), sasa wewe na slaa wako mnataka kutuambia kuwa mtajenga reli mpya bila kupita katika mikoa hiyo? Mtaipitisha angani nini? Je wananchi wa mikoa iliyobaki wasahau huduma hiyo muhimu kwao kwa usafiri?]
Treni ya sasa itaendelea na shughuli zake kwani huo ni mpango ambao tayari unafanya kazi. Cha muhimu kufahamu ni kuwa tunahitaji kusogea mbele ya hapo. Huwezi kusogea bila kuwa na mipango. Kwa maneno mengine wakati akina Kibunango mnaamini kuwa miaka kumi na tano ijayo Watanzania waendelee kuwa na treni na reli ya mwaka 47 (kilomita 65 kwa saa) wenzenu wanathubutu kubuni mpango mpya. Huu ni uthibitisho kuwa hakuna ubunifu wala uthubutu upane wa Kibunango. Kila kisichokuwepo, hakiwezekani kana kwamba sisi si binadamu kama binadamu wengine duniani.
Kibunango, ukitaka kuwaua wanao hali wakiwa hai waimbie tu huo wimbo wako mtamu kuwa hawawezi. Kama hamu yako ni kuidhoofisha jamii iaminishe kuwa haiwezi kuthubutu kufanya lolote. Ukitaka kulifuta taifa katika ramani ya dunia huna haja ya kutumia nyuklia, wewe lilishe tu sumu kuwa taifa hilo haliwezi, utakuwa umefanikiwa kupita maelezo.
Tuliambiwa na akina Kibunango hatuwezi kuongoza TANESCO wakaletwa Net Group Solution, nini kilichotokea? Haikutosha tukaelezwa hatuwezi kuendesha hata kampuni ya maji ya Dar es Salaam, wakaletwa. Benki eti tumezishindwa, wakaletwa. Hawakuishia hapo, hata reli waliyojenga wakoloni na ambayo imeendeshwa kwa miaka mingi kwa ufanisi mzuri tu, ghafla tukawa hatuwezi, imekodishwa kwa kampuni ya Kihindi. Kweli hatuna tunachoweza? Hatujui hata kulima na hivyo ili kuokoa kilimo kwanza, wako mbioni kuleta walowezi. Mambo haya yakiachwa kuendelea bila kukemewa na kusitishwa, Watanzania tunaweza kujikuta kuwa kivutio tu cha watalii, kama walivyo wahindi wekundu Amerika na Australia.
Kwa maana: Dawa ya Mjinga ni kuumia