Katika tafakuri zangu za kujiandaa kurudi kubeba maboksi kwa wazungu nimejikuta tena nikiitafakari nadharia tata ya 'Miafrika Ndivyo Ilivyo'. Ila leo nimeiangalia kwenye upande wa pili wa thumni. Hivi hawa wazungu ambao mwananadharia wa 'Miafrika Ndivyo Ilivyo' anadai wamependelewa na Mungu kuwa na vichwa vya kuvumbua sana wao huwa wanajisikiaje?
Kwa mfano, yanapotamkwa majina ya Galileo Galilei, Isaac Newton, Abraham Lincoln, Marie Curie, William Shakespear, Albert Einstein, Bill Gates na wazungu wengineo je mzungu anajisikiaje? Je, anajisikia kuwa hayo ni mafanikio ya Kizungu tu? Au anakubaliana na Frantz Fanon kuwa mafanikio hayo ni ya watu wote duniani ikiwamo Miafrika/Mitanzania?
Kama kuna mzungu humu ndani au mtu anayewaelewa vizuri wazungu basi naomba anisaidie kuelewa hili suala maana nadhani lina jibu la matatizo yetu Miafrika. Ningependa kujua mtu kama
Jim Sinclair anajisikiaje hasa anapotoa yale matangazo yake kuhusu jinsi wanavyochota madini ya Mitanzania. Je, na yeye anajisikia kama yule
Paul Mooney wa Makuadi wa Soko Huria? Kwa ujumla, je, wanajisikiaje kuhusu 'Miafrika ndivyo Ilivyo'?
Mkuu Companero, heshima mbele.
Mimi nipo ughaibuni miaka mingi sasa na toka nimetia mguu huku nimejifunza mengi saaana.
Nimejifunza kwamba wazungu ni watu wa aina gani, tabia zao, hulka zao na ni kwanini hawaoneshi kwa nje kwamba mwafrika wanamchukulia kwamba yupo majuu kwa bahati mbaya.
Jamii ya wazungu hasa Ulaya Magharibi) inaamini kwamba wanaamini kwamba jamii yao imejengwa kwa utaratibu ambao una mpangalio unaoeleweka na ambao utatambulika kote ulimwenguni.
Hizi vita yoote unayoiona duniani inatokana na dhana hio na ukifuatilia kwa makini utasikia wanatamka maneno kama "our tradition and values", "freedom", "better life", "world order" na "our way of life".
Marekani walitawaliwa na waingereza lakini baada ya vita vya kikabila na kuvumbuliwa kwa "The New World", George Washington na Abraham Lincoln waliondoa mawazo hayo ya kwamba jamii fulani ni bora kuliko ingine na kuweka dhana kwamba jamii yote ni sawa na itatambulika kwa misingi ya usawa na tofauti na mifano umeiona kwamba Collin Powel, Condoleesa Rice walikuwa mawaziri wakuu wa kwanza nchini humo na sasa kuna raisi Barak Obama na hawa wana damu ya mwafrika ukiondoa mama Rice.
Sasa kama hali hii ya mtu mweusi kuweza kuwa na nafasi ya juu katika vyombo vinavyoongoza nchi kama Uingereza na akakubalika katika jamii yote ndio ambayo huwa naisubiri niione Mwenyezi Mungu aniendelea kunipa uhai.
Sisi waafrika tulitawaliwa na wazungu miaka hio iliopita na bado mpaka sasa tunatawaliwa kwa mtindo wa utandawazi, biashara huria, na migogoro katika maeneo kama DRC, Darfur, Niger Delta, Somalia, Elitrea, Ethiopia na sasa Guinea Bissau.
DRC kuna vita ambayo ni ya kubadilishana silaha kwa dhahabu na almasi, na vita hii majeshi ya umoja wa mataifa yanashiriki na nyuma yake serikali zote za Kiafrika zinashirikiana na zile za mataifa ya magharibi.
Hali ni hiohio katika maeneo mengine niliyoyataja. Lakini waandishi wa habari wa Afrika wakiwemo wale wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya nchi za magharibi wamekuwa ni wasimulizi tu wa habari za vita hivyo pasipo hata siku moja kuwaweka kiti moto viongozi wa nchi hizi na kuwasuta.
Ughaibuni huwezi kwenda kugonga mlango kuomba chochote ule, huwezi kuokota pesa, huwezi kuomba mtu pesa njiani na akakuonea huruma, na huwezi kufanya madili ya ajabuajabu, ila unaweza kuchakarika kwa kazi na kula kwa jasho lako.
Kwa hio mimi nadhani bado sisi waafrika wengi wetu bado ni watu tunaoendekeza tabia ya kujijali binafsi na ndio unaona watu wanafanya madudu ya ajabu ya EPA na kadhallika.
Wazungu wengi wakija Afrika wanaendeleza desturi zao bila kujali kwamba wapo wapi na mifano mbona ipo mingi tu kwa kuangalia wanaishi wapi, wanafanya manunuzi wapi, na wanapata starehe wapi.
Sidhani kama wanajali kwamba sisi waafrika kama tunawasumbua.