NB: Picha kutoka mtandaoni
Lilikuwa ni wazo jema sana kuanzisha kampuni za uzoaji taka kwenye Jiji na hata kwenye maeneo ya makazi ya watu ili kuweka Jiji safi na kuondoa taka mitaani ili kuuweka mji mbali na milipuko ya magonjwa.
Lakini wazo hilo limegeuka wazo butu au kutiwa doa na aidha uzembe wa kampuni hizo au mamlaka za kusimamia utimilifu wa zoezi hilo kwani magari ya kuzoa taka mitaani na barabarani ikiwemo kwenye mikusanyiko kama masoko yamekuwa adimu yanaonekana kwa nadra kama kichwa cha kobe anayehisi hatari.
Soma:KERO - Gari la Taka linapita kwa kubeep Mtaa wa Sanawari – Arusha lakini kudai ushuru wako fasta sana
Kuna taka nyingi sana mitaani hasa kwenye masoko, ni shangwe tu za nzi zikisikika wakifurahia mrundikano wa matunda mabovu yaliyorundikwa. Huku mitaani ndio usiseme unaishia kupigiwa hodi za kudai pesa ya taka huku gari la kuchukua taka likiwa halijulikani litafata taka lini zilizojazana na kuoza.
Yote tisa, kumi mvua ndio hizo zipo uwanjani zinachanganya! Swali ni je kwa tabia hii, magonjwa ya milipuko yatatuacha salama wakazi wa Dar? Au tunasubiri kuambiwa hospital A imetengwa mahususi kupokea wagonjwa waliopataka kipindupindu kutokana na uzembe wa kutozoa takataka?
Ni nani alaumiwe katika hili? Je, ni mwananchi aliyeambiwa haruhusiwi hata kuchoma taka au kuzifukia hata kama anaona hali mbaya au wazoa taka ambao nao hawana hata sura ya kutaka kushauriwa wala kuhojiwa kwa nini hawazoi taka au mamlaka ambayo ndio msimamizi Mkuu wa kuhakikisha zoezi la uzoaji taka linafanyika pasavyo?
Na hili tunahitaji nani aje aseme ndio litekelezwe ipasavyo? Mfano ukipita pale Mbezi stendi ya Malamba upande wa barabarani utaoni michirizi ya maji yaliyojichuja kutoka kwenye taka na kuchora michirizi myeusi ikiingia mtarano, Je, kwa hali hiyo tutabaki salama?
Pia soma
~ Rais Samia: Dar es Salaam ni kuchafu, ni aibu
~ DC Mpogolo: Atakaye tupa taka Ganda la Ndizi na Pipi faini Milioni 1, Dar