Lula inspirations inataka kujua nini kiko nyuma ya pazia la maridhiano.Auliza ni kwanini sasa na sio zamani au baada ya uchaguzi.Sio kwamba yamefanyika na tujaribu kuyapa nafasi kama yatafanikiwa?
...Sasa wazenj wanasema lets give this attempt a shot, yeye anaona bora tuache tusubirie hadi uchaguzi upite.Naona kama amesahau kama tatizo lenyewe limeanzishwa na uchaguzi....sasa kupata uchaguzi mwengine si ndio maafa zaidi???...i guess he doesnt even care about that
😀
Makala hiyo ya kijana akijadili masuala ya Zenj.
Kuna nini nyuma ya pazia la mariadhiano ya Seif, Karume?
NIANZE kwa kumpongeza mwanasafu Lula wa Ndali Mwananzela. Nampongeza kwa kutekeleza vyema jukumu la kuhabarisha na kuelimisha umma wa Watanzania kupitia makala zake.
Lazima nikiri kwamba mimi ni msomaji mzuri wa makala zake kupitia gazeti la Raia Mwema. Licha ya kuwa kwangu nje ya nchi kwa sasa, hiyo hainifanyi nisifuatilie kinachoendelea huko nyumbani.
Nimevutika sana na hali ya kisiasa inayojitokeza kwa sasa huko nyumbani; hususani sehemu za Visiwani. Hata hivyo kuvutika kwangu si kwa uzuri; bali kwa mshawasha wa kujua siri ya hili jambo linalopigiwa kelele na kushupaliwa na karibu watu wengi; hasa wale wenye kujiita Wazanzibari wenye kuijua historia yao.
Nataka kukubaliana na Bw. Lula kuhusu suala moja; nalo ni kuwa mimi kuijua au kutokuijua historia ya Zanzibar, niwe au nisiwe Mzanzibari (Rejea Raia Mwema Na. 118), hakunifungi mdomo kuacha kuzungumzia ninachokiona kinaendelea huko Visiwani.
Hoja za hao wanaomsakama wakidai kwamba wao ndiyo pekee wanaoijua historia ya Zanzibar, ni hoja za watu wenye jazba ambao hufikiri kwa mdomo badala ya ubongo!
Suala linalotushtua tulio wengi; ni nini hasa kipo nyuma ya pazia la hayo yanayoitwa maridhiano ya hawa mabwana wawili Seif na Karume? Ni kwa heri ya Zanzibari kweli kweli au kuna lililojificha nyuma ya pazia kwa manufaa yao wawili?
Iweje maridhiano ya wawili hao yaje leo tunapokaribia uchaguzi mkuu? Ni kipi kilichobadilika ambacho kilikuwa kinakwamisha haya makubaliano (sijui niyaite maridhiano au mapatano) yasifanyike huko nyuma pamoja na vikao na mijadala kadhaa kufanyika?
Kwa maswali yangu haya simaanishi kuwa napingana na hayo wanayoyaita maridhiano au mapatano; bali najaribu kujiuliza nia yake hasa. Ninachokiona ni kuwa, kuna ukungu mkubwa katika hayo yanayoitwa maridhiano. Na mbaya zaidi, ukungu huu umewafunika macho hao wanaojiita Wazanzibari wenye kuijua historia yao kiasi kwamba hawataki hata kuhoji kinachoendelea, na badala yake wanakurupuka na kushupalia tu kwa ushabiki.
Inapotokea wengine kuuliza maswali kama haya ninayojiuliza ndipo tunapoonekana watu wa Tanzania Bara hatuitakii mema Zanzibar, na kwamba tunafurahia wao waendelee kuvurugana.
Ninachojiuliza ni kuwa; hivi hatuwezi kuzungumzia mapatano ya Zanzibar bila watu kuleta hoja za kuuvunja Muungano? Hivi dawa ya kutufunga midomo tunaohoji siri ya hayo makubaliano au maridhiano ya Seif na Karume ni kututishia kuvunja Muungano?
Hii inakuwa kama mwanamke mwenye gubu usimuulize swali lolote, ukimuuliza tu atakutishia kukuacha. Huu ni utoto. Swali hupewa jibu la hoja, na si vinginevyo.
Kitu ambacho wote mnapaswa kukumbuka ni kwamba vijana wengi hatukuwepo wakati huo mnaouita Muungano unazaliwa. Sisi tuliukuta tu. Tunafahamu faida za nchi kuungana lakini tunapojaribu kulinganisha aina ya Muungano tulionao Watanzania, hapo ndipo mazongezonge yanapotujia.
Amini usiamini, itafika kipindi vijana wa Watanzania Bara tutaona this is nonsense aina gani ya Muungano hii? Ama tuurekebishe au tuuvunje. Tukubali au tukatae, wengi wa vijana hawaoni faida ya huu unaoitwa Muungano.
Kwa hiyo kunapokuwa na sehemu moja ya Muungano inaamua kujifanyia mambo yake, ambayo kwa namna moja yanaweza kuathiri sehemu nyingine ya Muungano na hawataki waulizwe ama kutoa maoni, hapo ndipo tatizo linapokuja. Na hakuna taifa la leo ama la kesho la vijana wa Tanganyika litakalotaka kulea hali hii.
Tunachotaka kujua vijana ni je: Nini kipo nyuma ya pazia ya haya maridhiano ya Seif na Karume? Je Serikali ya mseto haiwezi kuundwa hata baada ya uchaguzi? Kwani ni lazima kuahirisha uchaguzi?
Kwa nini katiba haiwezi kuheshimiwa kwa sababu ya matakwa ya mtu mmoja, Karume au Seif? Kwani hayo makubaliano ya Seif na Karume hayawezi kuendelezwa na Rais mwingine yeyote ajaye isipokuwa Karume tu?
Haya ndiyo maswali ya vijana wa Bara yanayohitaji majibu, na si kutaka kutufunga midomo; eti hatuna haki ya kuzungumzia historia ya Wazanzibari. Kutuambia kwamba kila Mzanzibari anapozaliwa tu, basi, historia tayari ipo ndani ya damu yake, ni ushabiki usiomithilika na hoja za ubabe wa kitoto.
Serikali ya mseto ni jambo jema kwa mustakabali wa Zanzibar, lakini bila mapatano naona si suluhisho pekee la mivurugano ya Zanzibar. Tuambiwe ni nini kilichokuwa kinakwamisha hiyo serikali ikakawia siku zote hizo, lakini ghafla ije leo tena na kutaka kubadilisha katiba ili Karume aongezewe muda wa kuwepo madarakani. Kuna nini hapo? Mtujibu kwa hoja, msitutishie nyau!
Makala hii imeandikwa na kijana wa Kitanzania anayeishi nje ya nchi kwa sasa. Barua pepe:
tanzafpm@yahoo.com