NILICHO KISHUHUDIA USIKU WA WABABE WA ULAYA...
Kulikuwa na mechi nyiingi ambazo zilichezwa ili mradi ratiba kukamilika. Kiasi kwamba zipo ambazo tulizishuhudia zikiwa na matokeo kama ya Bonanza.
Baada ya kutafakari kwa kina niliyakumbuka maneno ya mwamba wa Real Madrid Mkandarasi Florentino Perez ambae aliwahi kunena maneno haya nami nitamnukuu...
Champions League bila Milan ni sawa na kuvaa Suti bila koti
Kwa mara ya kwanza katika ligi ya mabingwa baada ya kipindi kireefu tumeshuhudia mechi iliovuta hisia za Watu wengi.
Duru za Soka zilitaka kuishuhudia Milan ile ambayo ndio yenye ladha kamili ya mashindano haya.
Wachambuzi walitamani saana kuona ukubwa halisi wa mchezo huu baina ya timi hizi kongwe.
Hakika hakuna aliejutia.
Vibanda umiza kwa mara ya kwanza vilipokea watazamaji wa jinsia na rika zoote, hii ni kwa sababu Milan imerudi tena Ulaya.
Kwanini Milan?!
Milan itabaki kuwa Milan TU.
Historia katika Mchezo huu wa Soka ambayo wameijenga ni kubwa na inapaswa kuheshimika.
Tangu enzi ya Hayati Cesare Maldini na Giovanni Trapatonni era ya miaka ya 60 Milan wanabeba ubingwa wa Ulaya na kwenda kubeba ubingwa wa Dunia kwenye Dimba la Maracana nchini Brazil huku watemi hao wawili wakimkaba Pele aliekuwa mvamizi wa Santos ambayo ilikuwa bingwa wa Copa Libertadores, aliekuwa kwenye fomu ya hatari ni jambo la kuheshimika mno.
Ikaja miaka ya mwishoni mwa 1980 mpaka katikati ya miaka ya 1990 Milan ilitawala Soka la Dunia. Hapa kama kuna atakaebisha basi atakuwa ni mgeni wa Soka ama amejisikia tu kubisha.
Inaaminika kuwa Miaka hii Robo 3 ya wapenzi wa Soka Duniani walikuwa washabiki wa AC Milan.
Hivi ni nani ambae hakutamani kushabikia timu yenye nyota kama, Costacurta, Baresi, Maldini, Mswaki wa Jini Demetrio Albertini, Roberto Donadoni, Carlo Ancelotti, Frank Riijkhard, Ruud Gullit na Marco Van basten?!
Ninaposema AC Milan ni kubwa basi mnatakiwa muwe mnanielewa, Milan ina historia ya mataji na historia ya kuwa timu iliowahi sajili Nyota wengi waliong’aa Duniani katika vipindi tofauti.
Sitaki kukizungumzia kile alichokipata Barcelona mwaka 1994 kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya kwa maana Barcelona ni wakubwa wenzetu, hivyo nitakuwa kama nawadhalilisha.
Ladha ya Soka imerudi, na Watu wa Soka walifurahia sana Mtanange uliopigwa usiku wa jana pale Anfield.
Sasa nirudi kwenye mechi husika ambayo Liverpool walipata ushindi wa magoli 3-2.
Baada ya kupotea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa kwa miaka kidogo ya hivi karibuhatimae AC Milan ilirejea uwanjani jana.
Huku ikiwa imesheheni chipukizi wenye vipaji halisi vya Soka, Milan walipambana kiume na kuweza kuwabishia Liverpool ambao ilikuwa imebeba wakongwe na wazoefu wa mashindano haya.
Mambo mawili yalioiua Milan usiku wa jana ni:..
1. Uzoefu
2. Kujiamini.
UZOEFU.
Rejea andiko langu hapo juu likisema kuwa Milan imerudi Ulaya huku ikiwa na Nyota Chipukizi. Hii inamaana robo 3 ya wachezaji wa Milan jana ilikuwa mechi yao ya kwanza katika mashindano hayo.
Nilichokiona ni kuwa,
kama Milan wangekuwa na Ibracadabra pale mbele ambae ana uzoefu na mashindano haya basi mechi ingewawia ugumu sana Liverpool.
Kuwepo kwa wazoefu ambao wangeweza kukaa na mipira na ikibidi kupiga pasi zenye uhakika na wakati basi mechi ingekuwa ndefu zaidi kwa Liverpool.
Milan walicheza, lakini wazi kabisa walionekana kukosa uzoefu wa mashindano, kiasi kwamba mipira mingi ilipotea na pasi nyingi hazikuwa na macho.
Kuna Muda Milan walikuwa wanaonekana kuanza kuzoea mechi na kuondoa hofu ya Mchezo na kuweza kupiga pasi na kufika golini mwa Liverpool, lakini ghafla walikuwa wanarudi tena kwenye hofu, ndio maana nasema kama Ibra angalikuwepo ile jana basi wangeweza kuwa na kiongozi
ambae angeweza kuwahamasisha na hata kufanya vizuri.
KUJIAMINI.
Nyota hawa wa Milan walikosa kujiamini.
Hiki kilipelekea kucheza chini ya kiwango.
Kwa wanao wajuwa Theo Hernandez, Frank Kessie, Ismail Benacer, Rafael Leao na Davide Calabria ni wazi kuwa nyota hawa chipukizi jana hawakuwa kwenye viwango vyao vile na kukosa kujiamini.
Mwalimu pia alicheza kamali, kamali ambayo haikufanya vyema. Aliwaanzisha kwa pamoja Kessie na Benacer pale kati. Wawili hawa hawajacheza kwa pamoja kwa kipindi kirefu sasa kutokana na kuwa majeruhi kila mmoja kwa nyakati tofauti.
Tofauti ilikuwepo kubwa sana kwani maelewano yao hayakuwa sawia kama ambavyo tumewazoea.
Wengi tuliamini Mwalimu angeendelea kumpa nafasi Sandro Tonali ambae tangu msimu umeanza amekuwa rythim ya kiungo cha Milan, na hata dakika za mwisho za Mchezo alipoingia Milan walifunguka na kufanya kugonga hodi kwa wapinzani.
All in all hongera sana Liverpool.
Pongezi pia kwa vijana wa Milan kwa kuonesha uthubutu.