Ferruccio Lamborghini
JF-Expert Member
- Apr 15, 2020
- 1,667
- 2,595
HOSPITALI 10 zitajengwa Unguja na Pemba ndani ya kipindi cha miezi sita, hatua itakayoboresha kwa kiwango kikubwa huduma za afya Zanzibar.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Wazee, Nassor Ahmed Mazrui wakati akiwapa taarifa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu ujenzi wa hospitali hizo ambazo zitajengwa kwa fedha za mkopo wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19.
Alisema tayari mchakato wa ujenzi wa hospitali hizo umekamilika, ambapo jumla ya kampuni nne zimeshinda zabuni ya ujenzi. “Hospitali hizo zitajengwa kwa kuzingatia kiwango cha ubora wa hali ya juu na pia kusimamiwa na Wakala wa Bodi ya Majengo iliyopo chini ya Serikali ya Zanzibar.”
‘’Nataka niwajulishe wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba, ujenzi wa hospitali 10 Unguja na Pemba utatekelezwa na fedha za ahueni ya ugonjwa wa Covid-19 ambazo ni mkopo wa IMF na sasa tunasubiri kuanza kazi katika kipindi cha miezi sita,’’ alisema.
Alizitaja kampuni zitakazofanya kazi ya ujenzi wa hospitali hizo ni Rans ambayo itajenga Hospitali ya Mwera, Pongwe, kampuni ya China ya CRJE East Afrika ambayo itajenga Hospitali za Chumbuni, Magogoni na Mbuzini.
Alisema kampuni iliyopewa jukumu la kujenga Hospitali ya Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja ni Quality Building Contractor, wakati kampuni ya WCEC itajenga Hospitali ya Pangatupu Mkoa wa Kaskazini Unguja.
’Hospitali zitakazojengwa tutahakikisha zinafikia kiwango na ubora wa hali ya juu ili ziweze kudumu muda mrefu kwa ajili ya kizazi kijacho ambapo tutakuwa tukifuatilia ujenzi kwa karibu sana,’’ alisema.