Wakuu wanaJF kuna mgogoro uliwahi kulipotiwa ktk blog ya michuzi na ukatolewa maoni na wadau mbali mbali. Nimeona si vibaya tukishiriki pia kuona ni yapi yanaendelea kujiri ktk mgogoro huo.
Yafuatayo hapa chini ni maelezo ya wafanyakazi wa hoteli hiyo kujibu michango ya wadau mbali mbali wa blog ya Michuzi.
Kaka Michuzi,
Pole na majukumu yako ya kila siku, pia tunashukuru kwa kuweka malalamiko yetu katika blog yako ya jamii na wadau wengine wakapata fursa ya kuchangia maoni yao.
Kaka Michuzi sisi wafanyakazi wa Hoteli ya Movenpick tumesoma kwa makini maoni ya wadau wote waliochangia kuhusiana na sakata lililoikumba Hoteli yetu, pamoja na maoni mazuri lakini tumesikitishwa sana na baadhi ya wadau kuchanganya mada aidha kwa kutaka kumaliza hasira zao au tuseme kutojua kuwa sisi tunazungumzia nini.
Kwa mfano wapo waliotoa maoni ya jumla kuwa ni kweli sisi watanzania ni wezi na kutuunganisha sisi na wafanyakazi wa Bandari na wale wa Airport. Hawa naamini ni watanzania wanaoishi Ughaibuni, kwamba baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa hizo taasisi mbili wamekimbilia kutuunganisha nao.
Sisi tunasema hiyo sio sawa, sisi hatuhusiki na kutoa mizigo bandarini wala kukagua mizigo Airport. Kuna mdau mmoja yeye alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa hata Ivory Coast ililalamikia Hoteli yetu kuwa ina huduma mbovu na vyumba na vyoo ni vichafu pia, huyu tunadhani alishindwa kutofautisha kati ya Movenpick na Kilimanjaro Kempinski. Timu ya taifa ya Ivory Coast haikulala Movenpick bali ililala katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinsk, na hayo ndio matatizo ya kudandia mada bila kufanya utafiti.
Kuhusu swala la wizi, na udokozi, tunaomba kuweka bayana kuwa ni kweli vitendo hivyo vipo kama ilivyo katika taasisi yoyote, huwezi kuendesha taasisi iliyoajiri wafanyakazi zaidi ya 300 halafu uwe na wafanyakazi wote wasafi, labda kama umeajiri malaika.
Kuna wafanyakzi wengi wamefukuzwa kwa makosa ya aina hiyo na wengine wamevuliwa vyeo kwa uzembe, pale inapoonekakana kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Hoteli yetu, na labda hili wengi hawalifahamu. Katika Hoteli zote zilizopo hapa nchini Movenpick ndiyo Hoteli pekee yenye tawi la CHODAWU na kuna kamati maalum ya nidhamu inayoshirikisha uongozi wa hoteli na wajumbe wa CHODAWU ambapo jukumu lake ni kusikiliza kesi za wafanyakazi kabla ya mfanyakazi kufukuzwa.
Kamati hii imekuwa ikishirikiana na uongozi wa Hoteli katika kukomesha tabia ya wizi na uzembe kazini na hili limekuwa likifanyika kwa ushirikiano wa Meneja rasilimali watu anayeondoka.
Tatizo lililopo ni kwamba hawa wenzetu wazungu na hasa Meneja mkuu msaidizi bwana Shousha, na mpishi mkuu Bwana Vicenzo kutaka kuindesha hoteli hii kwa mkono wa chuma, wamekuwa hawaheshimu sheria za kazi na wamekuwa na maamuzi ya kuonea wafanyakazi. Ni watu ambao wanapotaka mfanyakazi aondolewe kazini hilo lifanyike bila kufuata taratibu na sheria za kazi, na huyu bwana Shousha ndiye anayesisitiza zaidi kutaka Meneja rasilimali watu kutoka Kenya aajiriwe akiamini kuwa yeye anaweza kufanya kazi bila kufuata sheria na kanuni za kazi za hapa nchini.
Sisi hatulalamiki kwa sababu ya huyo mkenya kuletwa, sisi hatuna matatizo na yeye, kilichotusukuma kuleta malalamiko yetu katika blog ya jamii ni kupinga ile nia ovu ya kuletwa kwa mkenya huyo, yaani ile kauli ya kusema kuwa atatukomesha, pili ni kutaka taratibu zote na sheria za uhamiaji zifuatwe.
Tunaamini kuwa ajira yoyote inayohusu mgeni ni lazima idhibitike kuwa hakuna mtanzania mwenye sifa hizo. Je ina maana tangu tupate uhuru mwaka 1961 serikali yetu imeshindwa kusomesha watu wenye uwezo wa kuwa mameneja rasilimali watu?
Hotel hii inayo wafanyakazi wageni zaidi ya 10, ambao hata hivyo vibali vyao vina mashaka matupu, wamekuwa wakikitumia kituo cha uwekezaji cha TIC kufanikisha malengo yao ya kuleta wageni kuchukua ajira zetu.
Kuna siku walikuja watu wa uhamiaji kutaka kuona vibali vya hawa wageni, mbona wote walikimbia, kwani kuna ambao wanaishi hapa hotelini na vibali vyao vya kuwepo hapa nchini vinaonyesha kuwa ni watalii.
Tunachotaka ni sheria za uhamiaji na taratibu zote za ajira kwa wageni zifuatwe kwa mujibu wa sheria, hatuna shida na wageni, lakini ikumbukwe kuwa ni serikali hii hii iliyoahidi katika kampeni za mwaka 2005 kuwa itazalisha ajira milioni moja, sasa kama ajira zenyewe zinachukuliwa na wageni, hizo ajira milioni moja zitapatikana wapi?
Wale mliosema kuwa ni heri waajiriwe wageni kwa kuwa watanzania ni wezi, jaribuni kutafakari kauli zenu, mkumbuke kuwa hata nyie ni watanzania na kwa kusema kuwa watanzania ni wezi, ni sawa na kuuambia ulimwengu kuwa sisi sio watu wa kuaminiwa, kwa wale walioko nje mjue kuwa hata nyie mmejitia kitanzi, hamtaweza kuaminiwa kabisa.
Je hamjui kuwa kuna nafasi za ajira ambazo zingeweza kushikwa na wake zenu watoto wenu, wajomba zenu, shangazi zenu, dada zenu, na ndugu zenu watanzania ambazo zimeshikiliwa na hawa wageni?
Kuhusu kuwa wakenya ni wachapa kazi, sawa tunakubali, lakini je nao ni wasafi kiasi gani? Hivi mnajua kuwa kuna baadhi ya mawaziri nchini Kenya hawaruhusiwi kuingia nchini Marekani na Uingerza kwa sababu ya makosa ya Rushwa, je Uzalendo wao uko wapi, uadilifu wao ulo wapi? Je sisi, ni mawaziri wangapi wamezuiwa kuingia katika nchi hizo?
Hawa wazungu, wanasema kabisa kuwa katika nchi ambazo wananchi wake ni wapole na wanyeyekevu hata uwafanyie nini ni Tanzania, na ndio maana hapa Movenpick kuna baadhi ya wazungu wameongeza muda wa kuishi na kufanya kazi hapa nchini zaidi ya mara nne kwa kubadili nafasi zao za ajira ili kupata ridhaa ya kuendelea kuishi hapa nchini.
Hawataki kuondoka kwa kuwa nchi yetu ni Corrupt katika kila sekta. Wazungu hawa wanajilipa mishahara mikubwa tofauti na wazawa. Mtanzania anaweza kulipwa shilingi milioni 2 lakini akija mzungu kwa nafasi hiyo hiyo analipwa dola elfu sita, sio shilingi za kitanzania namaanisha dola za kimarekani achilia mbali malazi chakula na huduma nyingine kama kufuliwa nguo na kadhalika.
Mshahara mkubwa kabisa wa mtanzania hapa ni shilingi milioni mbili na mshahara wa mzungu wa chini kabisa ni dola elfu sita, na huyu mzungu anayelipwa hizi fedha ni nokoa tu, hajui kazi, kazi zote zinafanywa na mtanzania, rangi tu ndiyo inayomlinda.
Tunapenda kumalizia kwa kusema kuwa Mkenya aletwe lakini sheria na taratibu za uhamiaji zifuatwe.
Ni sisi wafanyakazi wa Hoteli ya Movenpick
Dar Es Salaam.