Source: Majira
Chimbuko na mafanikio ya JKT kwa Taifa
*Ni nguzo muhimu ya malezi, uzalendo, kiuchumi na ulinzi wa nchi
09 July 2009
Na Juma Kiyenze
JESHI la Kujenga Taifa (JKT), Leo linatimiza miaka 46, tangu kuanzishwa kwake Jijini Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Ndani na aliyekuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Hayati Joseph Nyerere.
Sherehe za uzinduzi wa jeshi hilo, zilifanyika Julai 10,1963 ambapo Hayati Nyerere, alifafanua malengo ya kuanzishwa kwa chombo hicho muhimu na masharti ya kujiunga na JKT.
Wazo la kuanzishwa kwa JKT, lilitolewa mwaka 1958, kwenye Mkutano wa Umoja wa Vijana wa (TANU), mkoani Tabora. Wazo hilo lilitolewa na Mzee Rashid Mfaume Kawawa, baada ya kurejea kutoka nchini Ghana alikokwenda kuhudhuria sherehe za Uhuru wa nchi hiyo.
Akiwa nchini humo, Mzee Kawawa alikutana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Bw. Golda Meir, ambapo walifanya mazungumzo yaliyohusu maendeleo ya nchi zao.
Bw. Meir ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Israel, alimweleza Mzee Kawawa jinsi nchi yake ilivyokuwa ikiwaandaa vijana kijeshi na kushiriki katika shughuli za ujenzi wa Taifa kwa njia ya kujitolea.
Alimfahamisha jinsi vijana hao, walivyokuwa wakitayarishwa kuitumikia nchi yao kwa moyo wa uzalendo, upendo, kujituma, ujasiri, uvumilivu, kuinua uchumi, ulinzi na usalama wa nchi yao.
Mara baada ya Mzee Kawawa kurejea hotelini kwake, alikwenda kuonana na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa pamoja naye nchini humo. Alimweleza kiini cha mazungumzo kati yake na Bw. Meir ambapo Mwalimu Nyerere, alifurahishwa na maelezo hayo na kumtaka ayafanyie kazi baada ya kurudi nyumbani Tanganyika.
Baada ya Mzee Kawawa kurejea nyumbani, aliwasilisha wazo hilo kwa viongozi wa Umoja wa Vijana wa TANU. Wazo hilo lilifanyiwa upembuzi yakinifu na kufikishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja huo uliofanyika mkoani Tabora mwaka 1958.
Mkutano huo kwa kauli moja, uliafiki wazo la kuanzishwa kwa JKT, ili kuwatayarisha vijana kujikomboa kutoka kwenye makucha ya Wakoloni. Wakati maandalizi hayo yakishika kasi, nchi ilikuwa chini ya utawala wa Waingereza.
Malengo mengine ya JKT, yalikuwa ni kufuta makosa na makovu yaliyotokana na Wakoloni kuwagawa wananchi katika matabaka mbalimbali ili kurahisisha utawala wao, kudharau kazi za mikono, tofauti za makabila, dini, kipato, jinsia na rangi.
Tanganyika ilipopata madaraka mwaka 1960 na uhuru wake mwaka 1961, vuguvugu la utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa kwenye mkutano wa Tabora, yalipamba moto.
Mwaka mmoja kabla ya Tanganyika kupata uhuru, Mzee Kawawa, alialikwa nchini Israel 1960. Akiwa nchini humo, alitembezwa sehemu mbalimbali kujionea shughuli zilizokuwa zikifanywa na vijana.
Baada ya uhuru mwaka 1961, Serikali iliomba msaada wa mafunzo nchini Israel yaliyosaidia kuanzishwa kwa JKT. Israel iliridhia ombi hilo na kutoa nafasi mbalimbali za mafunzo ya uongozi kwa vijana nchini.
Miongoni mwa vijana wa kwanza kupelekwa katika ya uongozi nchini humo ni Meja Jenerali (mstaafu) Makame Rashid Nalihinga, ambaye alikuwa Mkuu wa JKT wa tano.
Wengine ni Brigedia Jenerali Dismas Msilu na Marehemu Brigedia Jenerali Irungi Athumani Msonge. Israel iliendelea kutoa nafasi zaidi za masomo kwa vijana wa Tanganyika na ilileta wataalam wake nchini kusimamia uanzishwaji wa JKT.
Serikali iliwapeleka vijana wengine nchini Bulgaria na Yugoslavia kujifunza mbinu mbalimbali za malezi ya vijana. Baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu na kuwapata viongozi waliohitajika, Julai 10, 1963, JKT ilianzishwa kwa kuanza kuwachuka vijana wa kujitolea kutoka mijini na vijijini.
Baada ya kuimarishwa kwa JKT, Serikali ilitangaza utaratibu mwingine wa kuwachukua vijana wasomi kutoka sekondari, vyuo na chuo kikiuu kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kuwajenga uwezo kisaikolojia.
Kuanzishwa kwa JKT:
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilipitisha sheria nambari 16 ya 1964, ambayo ilianzisha chombo hicho na kutoa uwezo wa kuandikisha vijana kujiunga na JKT. Hata hivyo, sheria nambari 64 ya mwaka 1966, ilifanyiwa marekebisho, ili iweze kukidhi matakwa ya kuwachukua vijana wasomi .
Vijana mbalimbali wasomi wa Kitanzania waliomaliza elimu ya sekondari kidato cha nne na kupata kozi zaidi ya miezi sita vyuoni pamoja na wahitimu wa kidato cha sita na kuendelea, walitakiwa kujiunga na JKT kwa mafunzo ya kijeshi na stadi za kazi.
JKT iliunganishwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwaka 1975, kutokana na marekebisho ya sheria namba 22 ya mwaka 1975 (The National Service ammendment act No. 22 of 1975, amalgamation with TPDF).
Lengo la kuanzishwa kwa JKT ni kutoa malezi kwa vijana wa taifa huru kwa kuwafundisha moyo wa upendo, kuondoa dhana ya ubaguzi, kupenda kazi za mikono, kuwa raia wema wenye kujituma, kujiamini, uzalendo, uchungu kwa nchi yao na kuthamini mila, desturi na kudumisha utamaduni wa taifa.
Dhima ya JKT ni kuwapatia vijana mbinu za kijeshi ili kuwa na Jeshi la akiba, kuwaandaa vijana kujiunga kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na kuwatayarisha kushiriki katika maafa yanayoweza kujitokeza katika kuokoa mali na maisha ya jamii.
Vijana hutayarishwa kisaikolojia kwa kupatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo yenye kukidhi haja ya kulitumikia taifa katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na ulinzi wa taifa kikamilifu.
Jukumu kubwa la JKT ni kuwafunza vijana mafunzo ya kijeshi na ufundi, ili kuwajengea uwezo wa kujiamini, nidhamu, uzalendo, ushirikiano, maadili, ubunifu, uwajibikaji na kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao mbalimbali yatakayotolewa kitaifa na kimatifa.
Mafunzo ya kwanza ya JKT yalifanyika katika ya mafunzo ya JKT Mgulani, Dar es Salaam yaliyofahamika kama Operesheni 1JLC. Mafunzo hayo yalianza Julai 10 hadi Septemba 28,1963 na kushirikisha vijana mbalimbali wa Watanzania.
Mgomo wa wasomi kujiunga JKT:
Kutokana na uelewa mdogo, baadhi ya vijana wasomi wa vyuo vya elimu ya juu na chuo kikuu walisusia kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria, baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo mwaka 1967.
Vijana hao, walifanya maandamano kupinga mpango huo wa Serikali. Hata hivyo, Hayati Mwalimu Nyerere kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kitaifa, walisimama imara kutetea uamuzi wao.
Serikali iliwarejesha majumbani vijana waliokaidi kujiunga na JKT, ili waungane na wazazi wao waweze kutafakari kwa kina kitendo hicho. Baada ya kuona ukweli huo, waliomba radhi.
Yapo mafanikio mengi yaliyofikiwa na JKT ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa, maadili kwa vijana, kupanua ajira katika sekta binafsi, kujituma katika majukumu, kupenda kazi za mikono na kuboreka kwa nidhamu sehemu mbalimbaliza kazi.
Vijana wengi waliopitia mafunzo hayo, waliajiriwa Serikalini, sekta binafsi na wengine walijiajiri wenyewe kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali kulingana na ubunifu walioupata.
JKT ilisaidia kupika viongozi wazuri wa kitaifa na kimataifa, ambao wanafanya kazi kwa uadilifu, ubunifu, uhodari, kujituma, wavumilivu na wenye nidhamu ya hali juu.
Vijana wa JKT walikuwa chachu ya kuthamini na kuhifadhi utamaduni wa taifa kwa kuibua vipaji vingi vya wasanii na wachezaji wa fani mbalimbali katika medani ya michezo kitaifa na kimatifa kwa kuiletea sifa Taifa.
Walishiriki kikamilifu kuitetea nchi yao wakati wa Vita vya Kagera dhidi ya uvamizi wa Majeshi ya Uganda mwaka 1978/79, kuhamisha waathirika wa majanga yaliyotokea nchini kwa nyakati tofauti, hasa ilipotokea ajali ya treni mkoani Dodoma, kuporomoka kwa jengo la ghorofa kumi jijini Dar es Salaam, na maeneo mengine.
Mkuu wa Majeshi (mstaafu), Jenerali David Msuguli alisema, wakati wa Vita vya Kagera, vijana wa JKT walionesha moyo wa uzalendo, kujituma na nidhamu ya hali ya juu kuihami nchi yao dhidi ya uvamizi wa majeshi ya Uganda, yaliyoongozwa na Marehemu Nduli Idd Amin.
Alitoa mwito kwa Serikali, kutilia mkazo mafunzo ya JKT kwa vijana na wale wanaohitimu watafutiwe ajira katika sekta za umma na binafsi kutokana na uadilifu na nidhamu yao. Jenerali Msuguli aliitaka Serikali, kuisaidia JKT ili iweze kufungua shule zaidi za ufundi, kuwawezesha vijana wengi kujifunza mbinu mbadala ili kupata wataalamu wengi wa nyanja mbalimbali za ufundi.
JKT ilisitisha mafunzo kwa vijana wa kujitolea kwa mujibu wa sheria mwaka 1994 kwa sababu za kiuchumi mpaka 2001, yalipoanza kutolewa kwa vijana wa kujitolea. Pamoja hayo, katika kipindi hicho cha mpito, taifa liliathirika kimaadili kutokana na vijana wengi kujihusisha katika vitendo vyenye kuhatarisha uvunjifu wa amani na usalama katika jamii.
Urejeshwaji mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria, ulitokana na Serikali kutafakari kwa kina na kufanya uamuzi wa busara kurejesha mafunzo hayo kwa vijana wasomi ili kuwajengea dhana ya uzalendo, kujitegemea na kuitumikia nchi yao kwa uadilifu.
Mbunge wa Kuteuliwa, Bw. Kingunge Ngambare Mwiru, aliitaka Serikali ijiandae kwa hilo, kwani idadi ya vijana wanaomaliza shule na vyuo kila mwaka ni kubwa.
Akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi bajeti ya Wizara ya Ulinzi na JKT iliyowasilishwa bungeni na Waziri wake, Dkt. Hussein Mwinyi, Juni 6 mwaka huu, anasema takribani vijana 80,000 wanahitimu elimu ya juu katika vyuo mbalimbali nchini.
Alifafanua kuwa, maandalizi hayo ni pamoja na upatikanaji wa wakufunzi bora wenye uwezo wa kuwapatia mafunzo yenye maadili mazuri yanayolingana na utamaduni wa nchi.
Akiwasilisha hotuba ya makario ya matumizi ya bajeti ya Wizara yake, Dkt. Mwinyi anasema, vijana waliopo kwenye makambi ni 7,110, ambapo kati ya hao 2,819 ni wa Operesheni Maisha Bora na 4,219 Operesheni Uadilifu.
Anaeleza kuwa, hatua mbalimbali za kuboresha malezi na mafunzo ya vijana zimechukuliwa ili kuimarisha kada ya ukufunzi kwa kuwapeleka kozi za ukufunzi zinazoendeshwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi nchini (VETA).
Malengo mengine ni kuendesha semina za kilimo, ufugaji na ufundi kwa wakufunzi na kuwahimiza kujiendeleza kitaaluma ili waweze kumudu malezi ya vijana na kushiriki kozi za ujasiriamali ambazo zitawajengea uwezo wa kuwafundisha vijana kubuni na kuendesha miradi mbalimbali baada ya kumaliza mkataba wao.
Aliyataja makambi saba ambayo yatatumika kwa ajili ya mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wa kujitolea kuwa ni Rwamkoma-Mara, Mgulani-Dar es Salaam, Chita-Morogoro, Maramba-Tanga, Itende-Mbeya, Nachingwea-Lindi na Mbweni-Dar es Salaam.
Akitoa salamu za JKT, Mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Samuel Kitundu, anasema JKT inatarajia kuanza kupokea vijana wasomi wa kidato cha nne na sita ifikapo 2010, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali.
''Vijana hawa ni wengi na hatuwezi kumudu kuwachukua wote, tumependekeza kuchukua vijana wa kidato cha sita wanaotegemea kujiunga na vyuo kikuu, tunaendelea na maandalizi ya wakufunzi, miundombinu, upanuzi wa makambi na kufungua mengine, ili kuwapokea hapo mwakani'', anafafanua Meja Jenerali Kitundu.
Anafafanua kuwa, changamoto nyingine ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuitaka JKT kuzalisha mbegu bora. Jukumu hilo ni kubwa na muhimu sana, inabidi tujipange vizuri sana kwa kuwa JKT haina nyenzo za kutosha. Msimu wa mvua JKT huanzisha kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na changamoto ya ukame.
JKT imefungua kambi mpya ya Kanembwa mkoani Kigoma na kufufua kambi ya zamani ya Msange iliyoko kilomita 15 kutoka Tabora mjini. Hivi sasa, wanaendelea na mikakati endelevu na utaratibu wa kufuatiliaji maeneo katika mikoa ambayo haina kambi za JKT.
Mapinduzi ya Kilimo:
Alifafanua kuwa, JKT inaendelea kufufua shughuli za kilimo ambazo mara baada ya kusitisha shughuli za JKT mwaka 1994, uzalishaji ulishuka kwa kiwango kikubwa. Nyenzo nyingi kama matrekta ya kulimia na yale ya kuvuna, yaliachwa na kuchakaa vikosini baada ya idadi ya watendaji kupungua.
Anasema kwa mujibu wa sheria, mwaaka 2010 watasaidia kuinua hali hiyo. Juhudi za ununuzi wa matrekta kwa mfumo wa vikosi wa kujinunulia kupitia faida ya miradi yao zimeanza kutekelezwa,
Changamoto:
Dkt. Mwinyi anasema, changamoto iliyopo ni ufufuaji wa mafunzo ya JKT na kujenga uwezo wa makambi yake kuweza kuwachukua vijana 10,000 kwa wakati mmoja.
Changamoto nyingine ni jinsi ya kuwatumia vijana watakaohitimu mafunzo hayo kuleta mageuzi ya kilimo, kuimarisha ulinzi na uzalendo wa taifa dhidi ya athari hasi zinazotokana na utandawazi, maendeleo ya teknolojia na mwingiliano wa watu duniani.
Sekta ya ujenzi:
JKT inamiliki Shirika la Uzalishaji Mali (SUMAJKT), linalojishughulisha na ujenzi wa majengo marefu (maghorofa), nyumba za kawaida, barabara, kilimo, uvuvi, ufugaji, kufanya biashara, viwanda na kufanya shughuli zingine ili kufikia lengo.
SUMAJKT inaendelea na ujenzi wa barabara ya Bagamoyo-Msata kwa ushirikiano na Kampuni ya Korea, ujenzi wa nyumba za Chama cha Walimu Tanzania (CWT) unaotekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara, nyumba za watumishi wa umma na machinjio ya kisasa mkoani Pwani.
Katika salamu zake kwa JKT kutimiza miaka 46, Meja Jenerali Kitundu anasema, umuhimu umeelekezwa katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda, ili viweze kuongeza tija na mapato.
Tangu kuanzishwa kwake, JKT limeongozwa na wakuu mbalimbali kwa nyakati tofauti. Viongozi hao ni Assistant Supaeritendant of Police (ASP), David Nkulila kuanzia Julai 1963-Desemba 1967.
Wengine ni Robert Kaswende Januari 1968-Mei 1970, Laurence Gama Mei 1970-Januari 1973, Meja Jenerali (mstaafu) Nelson Mkisi Januari 1973-Januari 1989, Meja Jenerali (mstaafu) Makame Rashid Nalihinga Januari 1989-Oktoba 2001.
Wengeni ni Meja Jenerali (Jenerali) Davis Mwamunyange, Novemba 2001-Juni 2006, Meja Jenerali (Luteni Jenerali) Abdulrahman Shimbo Januari 2006- Septemba 2007, Meja Jenerali (mstaafu) Martine Madata, Septemba 2007-Septemba 6, 2008 na Meja Jenerali Samuel Kitundu Februari 9, 2009 ambaye ni Mkuu wa JKT kwa sasa.