Tarehe ya Mei 09, 2009 baada ya maandamano makubwa yaliyotanguliwa na Bango
> lenye ujumbe Karibu Zitto Kabwe, Karibu Obama wa Tanzania, Mwongoze
> Magessa Bungeni, huku mbele yake wakiwa vijana waliobeba jeneza
> lililozungushwa kitambaa cha kijani katika kata ya Katoro ambayo ndio kata
> yenye wapiga kura wengi takribani asilimia thelathini ya wapiga kura wote wa
> jimbo la Busanda.
>
> Leo ni furaha isiyo kifani kwa maandamano na mahudhurio makubwa kiasi
> hiki. Umati huu mkubwa unanikumbusha Mkutano wangu mkubwa wa kwanza kuwahi
> kufanya, Mkutano wa Jangwani niliofanya viwanja vya Jangwani baada ya
> maandamano marefu ambapo watu takribani laki mbili waliandamana na
> kukusanyika viwanja vya Jangwani mwezi Agosti 2007 wakipinga uamuzi wa
> wabunge wa chama cha mafisadi-CCM, kunisimamisha ubunge baada ya kuwashinda
> kwa hoja, katika mjadala uliohusu mkataba mbovu na wakifisadi wa Buzwagi.
>
> Ni imani yangu mahudhurio haya tafsiri yake ni imani yenu kwa mgombea wetu
> Finnias Maggesa. Ni imani yangu kuwa Busanda na Katoro hamtatuangusha.
> Viongozi wenzangu waliotangulia kuhutubia wamezungumzia matatizo mengi
> yanayolikumbuka taifa letu, matatizo ambayo kwa miaka 48 utawala wa CCM
> umeshindwa kuyatatua.
>
> Mtakumbuka matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 kwa kura halali na zisizo
> halali yalikipa CCM ushindi wa wabunge 274 na CHADEMA wabunge 11.Lakini kwa
> kipindi cha miaka mitatu, wabunge 11 wa CHADEMA tumeweza kuhakikisha masuala
> mengi muhimu kuhusu mwenendo wa Taifa letu yanajulikana kwa Umma. Bila
> CHADEMA watanzania wasingejua ufisadi wa Buzwagi, EPA wala ufisadi wa
> Richmond uliosababisha serikali ya awamu ya nne kuanguka. Nasema kuanguka
> kwasababu kikatiba waziri mkuu ndio mwenye serikali. Kwahiyo serikali hii ni
> ya awamu ya nne na nusu.
>
> Wananchi wa Busanda, Ingawa tupo wabunge 11, lakini CHADEMA tupo makini
> kukabiliana na utawala huu mbovu chini ya uongozi mahiri wa Naibu Kiongozi
> wa kambi ya upinzani bungeni,na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dr Willibrod Slaa.
> Hii ndio sababu kwanini tunaomba mtuongezee mpiganaji wa 12, ambaye si
> mwingine bali kijana wenu, msomi wetu, mwenye sababu za kutosha kwa
> mapambano haya, Finias Magessa.
>
> Ndugu zangu wa Busanda, Uchaguzi huu sio uchaguzi wa Ilani za vyama.
> Uchaguzi wa Ilani za vyama ulikuwa mwaka 2005, ndipo vyama viliomba kura kwa
> Ilani , na CCM ikapata asilimia 86 ya wabunge pamoja na Urais. Mwenendo wa
> serikali ya CCM wote mmeouna. Wanasikitisha na kukatisha tama wananchi. Ndio
> maana ninawaambia, Ilani ya CCM ni ileile, kama kwa kuwapa wabunge zaidi ya
> 200 pamoja na Urais wameshindwa kuwatumikia, mnadhani mkichagua mbunge huyu
> mmoja wa CCM atabadilisha kitu? Ataongeza nini kama wenzake zaidi ya 200
> wameshindwa ? Jamani CCM hawana nyongeza ya Ilani! Ni hivi hivi! Ndio maana
> ninawaambia kwamba uchaguzi huu ni muhimu sana sio tu kwa nyie wakati wa
> Busanda, bali watanzania kwa ujumla. Ni kipimo. Ni kura ya maoni ambayo
> katika nchi nzima nyie watu wa Busanda ndio mmepata fursa hii ya kujibu.
> Mmepata fursa ya kuwaambia watawala tarehe 24, Mei mwaka huu kama
> mnakubaliana na mwenendo huu wa watala au hamkubaliani. Mnaridhika au
> hamridhiki.
>
> Ukipigia kura mgombea wa CCM Mei 24, tafsiri yake ni kwamba unaridhika na
> mwenendo wa utawala wa CCM, na ukipigia kura CHADEMA maana yake ni kwamba ni
> unatuma signal kwa watawala wetu kuwa hauridhiki na mambo yanavyokwenda
> katika nchi yako.
>
> Ndugu zangu wa Busanda, labda nyie hamkumbuki CCM inatupeleka awamu mmoja
> hadi nyingine. Kwa mujibu wa taarifa ya Hali ya Umasikini na Maendeleo
> nchini, Mwaka 2005, Tanzania ilikuwa na wananchi ambao ni fkara milioni 11,
> yaani hawa wanaishi chini ya dola moja kwa siku. Yaani mapato yao ni chini
> ya ya shilingi 1300 kwa siku.
>
> Rais Jakaya Kikwete alipokuwa kwenye kampeni aliahidi maisha bora kwa kila
> mtanzania. Na CCM ikaahidi kwenye ilani yake kwamba itapunguza idadi ya watu
> hawa masikini kabisa kwa asilimia 50%. Leo mwaka 2009, mwaka mmoja kabla ya
> mwaka wa uchaguzi 2010, Taarifa ya Hali ya umasikini inaonesha kuwa idadi ya
> watanzania wanaoishi chini ya kipato cha dola moja(shilingi 1300) kwa siku
> wameongezeka badala ya kupungua, na sasa wamefikia milioni12.7. Umasikini
> unapungua, au unaongezeka?
>
> Hili ndilo Busanda mnalo Mei 24. Ukipigia kura CCM maana yake unakubaliana
> na mwenendo wa serikali ya CCM uliosababisha idadi ya masikini kuongezeka
> mwaka hadi mwaka. Leo mwaka 2009 masikini kabisa wameongezeka kufikia
> milioni 12.7 kutoka milioni11 mwaka 2005. Maana yake katika miaka 3 CCM
> imeongeza idadi ya watu masikini kabisa milioni moja na laki saba.. Kwa
> mwenendo huu, Je kufikia kipindi cha uchaguzi wa 2010 watanazania wangapi
> watadumbukia kwenye shimo hilo la masikini kabisa? Milioni3? 5?.
>
> Hii ndio maana ya uchaguzi huu. Ni uchaguzi wenu wakazi wa Busanda. Sisi
> tumekuja kuwawezesha tu. Tumekuja kuwaunga mkono mfanye maamuzi sahihi kwa
> niaba ya watanzania wengine ambao hawakupata fursa hii. Mkichagua CCM
> mtakuwa mmewaangusha watanzania. Watanzania wana imani kubwa na nyie
> mliochaguliwa na Mungu kupiga kura hii ya maoni!
>
> Hebu fikiria wewe Baba na Mama wa Busanda. Mwaka 2005, katika kila wanawake
> 100,000, wanawake 520 walifariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito, Leo
> mwaka 2009, wanawake 527 wanafariki kutokana na matatizo ya ujauzito,
> matatizo ambayo msingi wake ni huduma duni za afya. Takwimu hizi maana yake
> nini? Maana yake katika kila lisaa limoja la Tanzania chini ya utawala wa
> CCM mwanamke mmoja anafariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito
> yanayosababishwa na serikali kutojali wanawake wan chi hii, na zaidi
> wanawake wa vijijini kama Busanda.
>
> Hebu fikirieni ninyi wazazi na wakazi wananchi kwa ujumla. Mwaka 2005,
> katika kila watoto 1000, watoto 114 walipoteza maisha kwasababu ya matatizo
> ya uzazi, leo mwaka 2009, watoto 112 wanafariki dunia kwa matatizo hay
> ohayo. Tarehe 24 Mei unapokwenda kupiga kura maana yake unakwenda kujibu
> swali hilo. Ukimpigia kura Magessa wa CHADEMA maana yake unapinga watoto
> wasio na hatia kuendelea kufriki dunia kwasababu zinazotibika kabisa. Na
> ukipigia kura CCM maana yake unakubaliana na mwenendo wa vifo vya watoto
> wasio na hatia kama hivi.
>
> Sisi CHADEMA tunaomba utupigie kura katika uchaguzi huu ili watawala
> washituke, wajirekebishe. Wajue kwamba watanzania haturidhiki na mwenendo
> huu wa umasikini na vifo. Wewe mwananchi ukiipigia CCM kura hawatajua kama
> kuna tatizo, hawatajua kama wananchi wanaumia. Hawatajirekebisha.
>
> Hali ya Taifa hili ni mbaya sana. Na tusipoangalia, Taifa hili tutalipeleka
> shimoni kabisa. Tangu mwaka 2007, Asilimia 38% ya watanzania wamedumaa akili
> kutokana na lishe duni. Maana yake nini? Maana yake katika kila watanzania
> 100, watanzania 38 wamedumaa akili, hawafikiri vizuri kutokana na lishe
> duni. Lishe duni ni indicator ya ufukara. Kama madiwani wa CCM ni
> watanzania wa kawaida, basi katika kila madiwani 10, madiwani 4 wamedumaa
> akili. Au katika kila wabunge 10( wa CCM lakini), wabunge 4 wamedumaa akili
> kama wanatoka familia za kawaida. Hivyo hivyo kwa mawaziri wa serikali ya
> CCM, kwamba inawezekana katika kila mawaziri 10, mawaziri 4 wamedumaa akili.
> Pengine ndio sababu wamekuwa wanasaini mikataba mibovu ya kifisadi.
>
> Kwahiyo tarehe 24, Mei, Ukichagua CCM, maana yake ni kwamba unaunga mkono
> mwenendo wa serikali ya CCM kusababisha watanzania 4, katika kila watanzania
> 10 wawe waendelee kudumaa akili. Na ukimpigia kura Magessa wa CHADEMA, maana
> yake ni kwamba, unapinga , unakasirishwa na mwenendo huu. Jamani taarifa
> hizi hatuzitungi sisi! Wala hatuziandai sisi. Ni taarifa za serikali.
> Ukisoma taarifa ya serikali ya Hali ya Umasikini na Maendeleo nchini (Pverty
> & Human Development 2007).
>
> Haya ndio maswali CCM wakija muwaulize, ingawa sidhani kama watafanya
> mikutano ya hadhara mana nimesikia wanaogopa sana kuzomewa kwa uzembe na
> ufisadi wa serikali yao.
>
> Nimesikia hapa mji mdogo wa Katoro, ambayo ni makao makuu ya jimbo hamna
> umeme. Hamna tofauti na Kasulu wala Kibondo mkoani Kigoma. Madhara ya kukosa
> umeme sio tu kwa wenye uwezo wa kuwa na umeme kukosa umeme, hali hii
> inasababisha gharama za maisha kuwa juu, kwasababu gharama za uzalishaji
> zinakuwa juu.Tulifanya utafiti Dar es Salaam kwa vijana vinyozi. Umeme
> ukikatika wakawasha jenereta wanatumia shilingi 68,000. Lakini wakitumia
> umeme wa TANESCO wanalipia shilingi 8000 tu. Maana yake kwa kutumia umeme wa
> jenereta wanapata hasara ya ziada ya shilingi elfu sitini. Hii ni tafiti
> ilifanywa na Kamati ya bunge. Kwaiyo sio Katoro tu. Nchi nzima ni tatizo.
>
> Nilazima watanzania tutafakari kama tunakokwenda ni sahihi au la! Na tufanye
> maamuzi. Wakati tunapata uhuru, Asilimia 15 ya watanzania walikuwa na
> Umeme.Leo ikiwa ni miaka 48 ya Uhuru, watanzania wanaopata huduma ya umeme
> hawazidi asilimia 12. Maana yake katika nchi hii yenye umri wa miaka 48 ya
> uhuru, katika kila nyumba 100, ni nyumba 12 tu ndizo zenye umeme, ilhali
> wakati wa uhuru, katika kila nyumba 100, nyumba 15 zilikuwa na umeme.
>
> Kwahiyo ukienda kupiga kura tarehe 24, Mei, unapaswa kujiuliza kama
> unakubaliana au hukubaliana na mwenendo huu. Ukichagua CCM maana yake
> unaridhika kuona kwamba wakati miaka 48 iliyopita watanzania walikuwa na
> huduma ya umeme ilikuwa 15, ni sawa, na sio tatizo kwa leo Tanzania huduma
> ya umeme kuwa asilimia 12.Naukiipigia kura CHADEMA mana yake unatma ujumbe
> kwa watawala kwamba unaumizwa na hali hii. Haukubaliani na hali hii.
>
> Njia pekee yaw ewe mkazi masikini kukataa hali hii ni kukataa kuipigia kura
> CCM. Ni kuipigia kura CHADEMA. Ni muhimu uone kama nafasi hii adimu kuwa
> muhimu sana kwako. Maana uchaguzi huu umefanyika kwasababu ya mipango ya
> Mungu. Na tunao amini katika Mungu, tunaamini kwamba mipango ya Mungu haina
> makosa. Na kila mpango una busara yake. Msituangushe kwakupewa fursa hii
> kabla ya miaka5 kukamilika.
>
> Hali ni mbaya ndugu zangu. Tanzania nzima ina majimbo 232. Lakini ni ninyi
> watu wa Busanda mliopewa fursa ya kuchagua tena kabla ya miaka 5. Nimesikia
> viongozi wa CCM wakipita na kuahidi eti CCM ikishinda uchaguzi huu italeta
> umeme Busanda. Waulizeni walikuwa wapi miaka 48 yote hii. Kama wameshindwa
> kuleta ndani ya miaka 48, watawezaje ndani ya mwaka 1?
>
> Ndio maana sisi CHADEMA tunawaambia watanzania kwamba uchaguzi huu ni kura
> ya maoni , Tunaamini mtachagua CHADEMA ili kuonyesha kwamba hamkubaliani.
> Kuna matatizo mengi sana wilaya hii ya Geita. Kwa mujibu wa taarifa za
> uchumi za mwaka 2006, Geita ni miongoni mwa wilaya tatu masikini kabisa
> Tanzania, ikiwa pamoja na Bunda na Musoma vijijini.
>
> Ninyi wilaya yenu ya Geita, unaozalisha takribani wakia laki tatu na nusu
> kwa mwaka, ambazo ni sawa na bilioni 211 kwa bei ya sasa. Lakini utajiri huo
> hauna tafsiri yoyote kwa maisha yenu. Sisi kwenye Kamati ya Bomani
> iliteuliwa kupitia upya mikataba ya madini nchini tulipendekeza kanuni ya
> kukokotoa mrabaha kwanza ibadilishwe kutoka asilimia tatu hadi 5, lakini
> zaidi hesabu hizo zikokotolewe kutokana na gharama zote za uzalishaji, na
> sio mwekezaji azalishe kasha aondoe gharama zote za uzalishaji kasha ndio
> atupe watanzania asilimia 3 tu ya hilo salio. Kwasababu CCM haina dhamira ya
> kuwasaidia, bado imeendelea kupiga danadana utekelezaji wa Kamati yetu.
>
> Baada ya vuguvugu la kupinga mikataba mibovu liliasisiwa na CHADEMA tangu
> sekeseke la Buzwagi, Leo Geita mnapata dola laki 2 kutoka mgodi wa dhahabu
> wa Geita( Geita Gold Mining-GGM). Kule Tarime, Halmashauri ile chini ya
> Uongozi wa CHADEMA, kwa kuamini kuwa wawekezaji wanatunyonya watanzania
> wakawaida kwasababu ya elimu duni, CHADEMA tuliamua fedha yote ile ipelekwe
> kusomesha watoto bure kwa shule za sekondari. Ni kweli fedha hizi ni kiduchu
> sana, lakini si haba. Sio sawa na kukosa kabisa. Sasa kama Tarime fedha hizi
> zinasomesha watoto. Nyie wilaya ya Geita fedha hizi zinakwenda wapi?
> Zinaishia kwenye warsha, vikao na makongamano ya madiwani.
>
> Yote haya ni matokeo ya utawala dhaifu na usiowajali wa Chama cha
> Mapinduzi-CCM. Kwa mfano, kama Serikali ya CCM ingekubali kuetekeleza
> mapendekezo ya Kamati ya Bomani, Badala ya wilaya zenye migodi kupewa dola
> 200,000. Kila wilaya yenye mgodi ingelipwa dola milioni2 kwa mwaka. Yani
> mara 10 zaidi ya sasa.
>
> Tarehe 24 Mei, ukienda kupiga kura, ukichagua CCM, maana yake unakubaliana
> na utaratibu wa sasa wa CCM kutoa dola laki mbili kwa mwaka kwa halmashauri
> yako badala ya dola milioni mbili kama Kamati ya Bomani inavyotaka unufaike
> na madini. Kura yako ni alama! Ukienda ukampigia kura Magessa, maana yake
> unataka Serikali ya CCM itoe dola milioni mbili badala ya dola laki mbili
> kwa Halmashauri yako.
>
> Kwaiyo unaona thamani ya kura yako ilivyo kubwa. Zaidi ya utu wako, kura
> yako ina thamani ya mabilioni. Lakini leo tunasikia CCM wanapita wanawahonga
> watu shilingi elfu mbili, tatu,nne, tano. Inajua bei za wateja wake. Ukiwa
> mjanja mjanja kidogo inakupa hata elfu kumi. Ukiwa hujui kitu kabisa inaweza
> kukupa hata shilingi mia moja. Lakini wote hawa ni wajinga, tofauti yao ni
> bei za ujinga wao.
>
> Ukiuza shahada yako maana yake unahujuma maendeleo ya Taifa leko. Unahujumu
> maisha ya watoto wako.Lazima mjiulieze kwanini mtu akupe pesa kukuzuia
> usipige kura? Watoto wenu hapa wanasoma shule za kata zisizo na walimu,
> vitabu, wala maabara kwasababu mnakosea kupiga kura.
>
> Kura yako ni muhimu sana. Ukipigia kura CCM maana yake unaunga mkono
> ufisadi. Ukipigia kura CHADEMA maana yake umeamua kuunga mkono harakati za
> uzalendo. CCM haijawi kuwa na huruma baada ya Mwalimu Nyerere.
>
> Wakati kwa kipindi cha miaka 10, tangu mwaka 1997 hadi mwaka 2006, Bunge la
> Tanzania halikuwa limepata hoja binafsi kutoka kwa mbunge yeyote, Hoja
> binafsi ya kwanza ilitolewa na mimi Bungeni, Hoja ya Buzwagi kupinga ufisadi
> katika mikataba ya madini ambapo baada ya kuwashinda kwa hoja, bunge la CCM
> mafisadi waliamua kunisimamisha kazi yangu ya uwakilishi. Na hoja binafsi ya
> pili ni hoja ya ufisadi wa benki kuu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa
> CHADEMA, Dk Willibrod Slaa, ambayo ilikataliwa na tukaamua kuipeleka kwa
> Umma septemba 15, 2007 , na mpaka leo bado inaisulubu serikali ya CCM.
>
> Tangu sekeske la Buzwagi, Agosti 14, 2007, Hali ya taifa ni tete haijawahi
> kutokea tangu uhuru, na itaendelea kuwa tete mpaka hapo watanzania
> watakapofaidika na rasilimali za nchi yao. Na Tanzania haitafikia hali hiyo
> chini ya utawala wa CCM. Njia pekee ni kuondoa utawala huu uliojaa wezi,
> wasio na uchungu na maisha yaw ewe masikini wa Busanda.
>
> Asiwadanganye mtu kwamba ndani ya CCM kuna kiongozi mwenye ujasiri wa
> kupambana na ufisadi. Mana wameanza kujitokeza baadhi ya wabunge wa CCM eti
> wakijifanya na wao wana uchungu na nchi hii. Eti na wao wanapambana na
> ufisadi. Waulizeni walikuwa wapi miaka yote hii nchi ikiuazwa? Leo baada ya
> CHADEMA kuhamasisha Umma kwa kupinga ufisadi, nao kwa aibu ya kuogopa
> kuzomewa ndio wanachukua ajenda za CHADEMA ili nao wasionekane mafisadi.
> Mimi nawaambia, hakuna kiongozi safi ndani ya CCM. Wabunge wote wa CCM
> walishinda uchaguzi Mkuu kwa takrima.
>
> Vita dhidi ya ufisadi ni via takatifu. Haiwezi kufanywa kwa unafiki. Wala
> kwa hawa ninaowaita walokole wa vita dhidi ya ufisadi.. Nimeambiwa watakuja
> hapa akina Olesendeka, akina Dk Mwakyembe na wenzao. Mimi nawaambia wabunge
> wote wa CCM walipewa shilingi milioni5 ambazo ni sehemu ya fedha za ufisadi
> zilizochotwa benki kuu kupitia kampuni ya kifisadi ya Kagoda. Waulizeni
> wakija. Mana wakati walitumia fedha za ufisadi wa Kagoda, leo wanajifanya
> wanapinga ufisadi. Wapi na Wapi jamani?
>
> Ndio maana nawaambia kuwa uchaguzi huu wa Busanda ni wa kihistoria. Mnayo
> nafasi ya kuamua kuiangusha CCM, mnayo nafasi ya kutukataa. Sisi tupo
> wabunge 11. Lakini kazi tuliyoifanya kwa miaka hii mitatu tunaamini, kama
> mnaipenda nchi yenu mtatuongezea wabunge. Tumpate mpiganaji wa 12, Ndugu
> yangu Finias Magesa. Mkituchagua mtakuwa mmetupa moyo, na itatusaidia
> kuongeza mapamabno zaidi. Lakini mkituangusha mtakuwa mnatuvunja moyo. Ni
> sawa na kutuambia kuwa mapambano yetu dhidi ya ulinzi wa rasilimali za
> madini na vita dhidi ya ufisadi ni kelele tupu.
>
> Tumekuwa tukiwaambia watanzania. Mwenyezi Mungu hakudhmilia nchi hii iwe na
> watu masikini kiasi hiki. Hebu angalieni, Kanda ya ziwa imejaa dhahabu,
> Almasi, Nickeli na Almasi. Kanda ya Magharibi imejaa Shaba, Mafuta na madini
> ya fedha. Kanda ya kati ya ina madini ya uranium yanayotumika kutengenezea
> mabomu ya nuclear, Kanda ya Pwani imejaa gesi na mafuta. Kanda ya kusini
> imejaa makaa yam awe. Kila kanda Mungu ameipa utajiri. Lakini masikini
> wamejaa juu ya ardhi tajiri. Kwanini msichukue hatua? Mimi ninawaambia. Njia
> pekee ya kutoka hapa tulipo kwanza ni kuikataa CCM.Ndio maana ninarudia!
> Uchaguzi huu ni zaidi ya uchaguzi. Ni kipimo kama mnaridhika au hamridhiki
> na mwenendo wa utawala wa namna hii.
>
> Katika uchaguzi wa 2005, CCM waliwaahidi maisha bora kwa kila mtanzania
> kufikia mwaka 2010. Leo ni 2009, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, Wangapi
> maisha bora walau yamepiga hodi kwao? . Mwaka 2005 bei ya kilo ya sukari
> ilikuwa shilingi 600, leo bei ya sukari shilingi 1400. bei imepanda zaidi ya
> mara mbili, Je mapato yenu yamepanda au yameshuka? Bei ya khanga za akina
> mama mwaka 2005, khanga ya India ilikuwa sh 2000. Leo naambiwa hapa Busanda
> khanga ileile inauzwa shilingi 3500. Mfuko wa saruji mwaka 2006 uliuzwa kwa
> shilingi 11,000. Leo mwaka 2009 mfuko wa saruji unauzwa shilingi 21000.
> Mwaka 2006 nauli kutoka kijiji chochote cha jimbo la Busanda kwenda Geita
> ilikuwa ni shilingi 1000 mpaka 2000 tu.
>
> Leo mwaka 2009, nauli zimepanda hadi shilingi 3000. Lazima mjiulize kweli
> mapato yenu yamepanda?. Kweli haya ndio masiha bora mliyotarajia? Wakati
> bidhaa hizi zinapanda bei, mazao yenu ya kilimo kama pamba serikali
> imeshindwa kuzuia yasiporomoke bei. Wakati mwaka 2006 kilo ya pamba iliuzwa
> kwa shilingi 400, leo mwaka 2009, kilo ya pamba inauzwa kwa shilingi 300. Na
> haya ndio maisha bora mliyoahidiwa na CCM. Mapato yenu yanaporomoka, uwezo
> wenu wa kununua unashuka, lakini bidhaa za kununua zinaachwa zipande bei.
>
> Tarehe 24, Mei ukienda kupiga kura , ukichagua CCM maana yake unakubaliana
> na gharama za maisha kupanda. Ukichagua CHADEMA na Magessa maana yake
> unatuma ujumbe kwa watala kwamba hakubaliani na kupanda kwa gharama za
> maisha.
>
> Najua kwamba watawala hawa walioshindwa wamekuwa wakitumia nguvu za dola
> kukabiliana na utashi wa wananchi walioamua kufanya mabadiliko. RPC na OCD
> naomba mnisikilize kwa makini. Mjue kwamba chochote mlichovaa, kuanzia
> kiatu, magwanda ni kodi zetu wananchi. Na labda wananchi mkumbuke kuwa hawa
> polisi, wengi ni watoto wa masikini kama sisi. Ni mgawanyo wa kazi, wengine
> wanakuwa walimu, wengine madkari, wengine polisi, wengine wabunge. Sasa
> kwenda kwenu upolisi kusiwafanye mgeuke tatizo kwa wananchi badala ya
> kuwalinda.
>
> Polisi mnapaswa kukumbuka kuwa ninyi ni watoto wa masikini kama sisi.
> Mkimtesa kijana wa Busanda, basi ujue kwamba na wewe kwenu mdogo wako
> anateswa na polisi mwenzako. Ukimtesa mama wa Busanda hapa, ujue kwamba
> polisi mwenzako anamtesa mama yako huko kwenu. Ukimtesa mzee wa Busanda,
> ujue na wewe wazee wako wanateswa na polisi wenzako huko kwenu.
>
> Polisi wanapaswa kukumbuka ni sisi wabunge tunaojadili na kupitisha bajeti
> zao. Na sisi wabunge wa upinzani siku zote tumekuwa mstari wa mbele kudai
> maslahi bora ya polisi ili kupunguza udokozi wa polisi kwa wananchi masikini
> kabisa, na kuwasababishia usumbufu, na kukosa amani. Hatutaki polisi
> watupendelee, wala watuonee. Wakituonea tutajibu. Wakipendelea CCM
> tutakataa. Polisi wanapaswa kujua leo ni polisi, kesho raia. Hatutaki polisi
> waonee raia, ingawa hatutaki raia wavunje sheria.
>
> Jamani polisi wa Tanzania ndio polisi wanaolipwa kidogo kuliko polisi wote
> katika nchi kumi na mbili za SADC. Nchi zingine kama Malawi ambazo uchumi
> wake unategemea tumbaku lakini polisi wake wanalipwa vizuri kuliko polisi
> wetu, Nchi yenye madini, ziwa, bahari, ardhi yenye rutuba, watu wenye moyo
> wa kufanya kazi na kila aina ya utajiri.
>
> Polisi wanapaswa kufikiria upya kuhusu ukandamizaji wanaoufanya dhidi yetu
> wapinzani maana wao ni sehemu yetu. Wote tumepigika tu! Polisi ndio
> wanaolinda benki kuu, lakini wakati mafisadi yanaingia benki kuu, polisi
> wetu wanapiga saluti, mafisadi yanaingia yanachota mabilioni ya fedha,
> yanatoka. Polisi wanabaki ni wakukamata vibaka wanaoiba masufuria, mbuzi,
> kuku, na vitu vidogo vidogo. Mapapa na manyangumi yanayohujumu uchumi wetu
> hayaguswi.
>
> Mimi Zitto Kabwe nawambia, sitaki kusikia mtanzania yeyote wa Busanda
> ananyanyaswa na polisi eti kwa sababu ya chama chake.Nikipata polisi mmoja
> anayenyanyasa raia kwa sababu tu ya chama chake, nitamfanyia kazi kama
> nilivyomfanyia Nazir Karamagi. Na nilipokuwa Tarime kwenye uchaguzi mdogo
> niliwaambia polisi kauli kali kwasababu ya ujinga na upumbavu wa baadhi ya
> polisi. Sitarajii yaliyofanywa na polisi Tarime yatajirudia Busanda. Yeyote
> atakaye nyanyaswa na polisi hapa atoe taarifa kwa viongozi wa CHADEMA. Ila
> msivunje sheria.Hatutamtetea yeyote atakaye vunja sheria. Tunataka uchaguzi
> wa amani, tumapate Magessa tujenge taifa hili, Kazi ambayo CCM imethibitisha
> kwa vitendo kuwa wameshindwa.
>
> Tarehe 24, Mei mchague Magessa akutetee wewe mkazi wa Katoro, awatetee
> wakazi wa jimbo la Busanda. Awatetee wakazi wa mkoa wa Mwanza. Awatetee
> watanzania. Mkoa wa Mwanza una majimbo 11, yote mkaipa CCM. Kuna Kikao cha
> Kamati ya mashauriano ya mkoa, RCC, Nani atawatetea kwenye RCC ilhali
> mmejaza wabunge wa CCM humo?
>
> Mimi nawaambia kutoka uvungu wa moyo wangu kwamba, wabunge wa CHADEMA hata
> tufanye kazi namna gain Dodoma, kama hamna mbwa mkali Geita, Mwanza,
> mtaendelea kuibiwa tu!. Tunahitaji mbwa mkali ambaye akiona ufisadi kwenye
> Halmashauri, RCC na Serikali kuu aje kuwaambia. Tunahitaji mtu mwenye rekodi
> na tusiye na mashaka kuhusu dhamira yake ya kututumikia. Na katika wagombea
> hawa, hakuna Mwingine isipokuwa Magessa.
>
> Hakuna mtu yeyote wa CCM ambaye akiwa mbunge anaweza kupinga ufisadi wa CCM
> ilhali wabunge wote wa CCM ni zao la ufisadi.. Labda apinge kwa unafiki wa
> makundi ndani ya CCM lakini sio kwa dhamira ya mapenzi ya mtanzania kwa nchi
> yake. Magessa amesoma sekondari Tosa Maganga, Zitto amesoma sekondari
> Tosamanganga. Magessa amesoma shahada ya kwanza na kufanya harakati Chuo
> Kikuu cha Dar es Salaam, Zitto amesoma shahada ya kwanza na kufanya harakati
> Chuokikuu cha Dar es Salaam. Magessa amesoma shahada ya pili Ujerumani,
> Zitto Amesoma Shahada ya pili Ujerumani. Ninawaomba wananchi wa Busanda,
> mpeni nafasi kijana wenu Finias Maggessa. Ninaamini Magessa ni Zitto na
> Zitto ni Magessa.