Mwanzoni mwa karne ya 20, harakati za wahifadhi mazingira zilizochochewa na watu mashuhuri kama vile John Muir, Gifford Pinchot, na Paul Sarasin zilisisitiza haja ya kuhifadhi mazingira ya asili. Katika kukabiliana na mahitaji yanayokua ya kulinda mazingira haya ya asili na kuratibu juhudi za kimataifa za uhifadhi, Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) ulianzishwa mwaka 1948 katika Mkutano wa Fontainebleau.
Ufahamu wa uharibifu wa bahari ulipoongezeka, mahitaji ya kulinda mazingira ya baharini yakawa ni suala la linalohitaji kushughulikiwa kwa umakini na haraka zaidi. Aidha mabadiliko ya tabianchi yanachochea sana ongezeko la kina cha maji ya bahari na kutishia uwepo wa nchi zinazoendelea za visiwa vidogo pamoja na jamii zinazoishi maeneo ya pwani. Maji ya bahari yamekuwa na viwango vya juu vya joto vilivyovunja rekodi na kuchochea matukio ya hali ya hewa ya kupindukia yanayotishia kila mtu.
Kwa kutilia maanani hilo kampuni ya mawasiliano ya China ya Huawei imeshirikiana na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) ili kuendeleza juhudi za uhifadhi wa eneo la baharini katika pwani ya kusini mwa Kenya. Mradi huo uliozinduliwa hivi karibu na ambao utaendelea kwa miaka mitatu, unalenga kulinda afya ya kiikolojia ya Eneo la Hifadhi ya Bahari ya Kisite-Mpunguti, ambalo ni la bayoanuwai lililo kwenye ukingo wa kaunti ya pwani ya kusini ya Kwale. Washirika wengine wanaotekeleza mradi wa “Tech4 Nature” ni pamoja na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya na Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Wanyamapori ambao ni wakala wa serikali.
Mradi huu unaenda sambamba na mpango wa Huawei wa TECH4ALL na Orodha ya Kijani ya IUCN huku lengo lake kuu likiwa ni kuongeza ufuatiliaji na usimamizi wa eneo linalohifadhiwa la baharini, ambalo lina utajiri mkubwa wa miamba ya matumbawe ya asili pamoja na viumbe maarufu kama vile kasa wa kijani na pomboo wenye pua ya chupa ambavyo kwa sasa viko katika hatari ya kutoweka.
Akifafanua kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Vyombo vya Habari wa Huawei Kenya Khadija Mohammed Ahmed alisisitiza haja ya kutumia teknolojia na ubunifu ili kuimarisha afya na uhimili wa mifumo ya ikolojia ya baharini, inayotishiwa na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu.
Kwa sasa inaonekana kwamba maji ya bahari yanazidi kuwa na tindikali na kuharibu matumbawe mengi chini ya bahari, ikiwa ni pamoja na kuharibu uhusiano muhimu wa upatikanaji wa chakula huku utalii wa bahari na mbinu za kujipitia vipato kwa jamii za maeneo ya pwani ukitishiwa.
Shughuli zisizo endelevu za kuendeleza maeneo ya pwani, uvuvi kupindukia, uchimbaji wa madini kwenye kina kirefu cha bahari, uchafuzi wa mazingira na utupaji wa taka za plastiki baharini vyote vinasababisha mvurugano wa mfumo anuai wa baharini duniani kote.
Mradi huo wa Huawei utahusisha usambazaji wa kamera za chini ya maji, teknolojia ya upigaji picha na ufuatiliaji kwa njia ya sauti ili kufuatilia viumbe vya baharini, wakiwemo samaki wa aina mbalimbali katika Hifadhi ya Bahari ya Kisite-Mpunguti.
Mwakilishi wa nchi katika Ofisi ya IUCN Kenya, Innocent Kabenga, alisema teknolojia mpya za Huawei zitasaidia kunasa na kuchanganua data katika eneo linalohifadhiwa la baharini, kukuza uhifadhi wake na kuleta manufaa kwa jamii za wenyeji.
Suluhu ya kiteknolojia iliyosambazwa baharini na Huawei na washirika wake ni akili bandia iliyofunzwa kutambua spishi zinazolengwa kwa kuona na kusikia sauti, kutoa maarifa ya wakati halisi yanayotokana na data kuhusu tabia, mienendo ya idadi za spishi na usambazaji wa bayoanuwai katika hifadhi ya bahari.
Huawei ilisema teknolojia hizi pia zitaweza kutambua boti zinazotumika kwa uvuvi haramu na kutuma tahadhari kwa walinzi kuingilia kati kwa wakati halisi, na kuongeza kuwa suluhisho la umeme wa kidijitali na uboreshaji wa muunganisho wa mtandao katika eneo la hifadhi na mnara wa ufuatiliaji utaimarisha usambazaji wa haraka wa data zilizokusanywa hadi kwenye seva ya wingu kwa ajili ya uchambuzi.