Simba wanahisi wana wachezaji bora kuliko timu yoyote ya Ligi Kuu, na kwa hivyo hawapaswi kuhangaishwa na timu yoyote ya Ligi Kuu au kwengineko Tanzania hii na hata Afrika ya Mashariki yote. Wanaamini kwamba kutoridhisha kwa kiwango cha timu yao kunasababishwa na makocha walio nao, wakisahau kwamba walijiridhisha (kama walivyojiridhisha kwa huyu Mzungu) awali kabla ya kuwateua. Uhalisia ni kwamba Simba wana mchanganyiko wa wachezaji aina nne: 1. Wachezaji hodari lakini wanaoshindana zaidi na umri kuliko wachezaji wenzao uwanjani. 2. Wachezaji vijana wenye uwezo lakini bado hawajakomaa 3. Wachezaji vijana wenye uwezo mkubwa lakini waliokata tamaa kwa sababu moja au nyengine 4. Wachezaji vijana wenye uwezo mkubwa lakini wanaolemazwa na kudekezwa mpaka wakajiona wakubwa kuliko timu. Sidhani kama kuna atayemfunulia kocha huyo mpya ukweli huu. Na bila ya ukweli huu, Simba itabaki kuuguza majeruhi ya Okwi na Niyonzima huku kina Mlipili wakisubiri Nyoni aumie. Hata watapoamua, mathalan, Ndemla aingie uwanjani akiwa bado na msongo wa mawazo ya safari ya Sweden, bado kina Kichuya wataendelea kucheza na mfundo moyoni kwa sababu hakuingizwa mchezaji waliyemtarajia wao. Wataendelea hivyo mpaka Haji Manara atapopata wasaa mwengine wa kuwabembeleza. Unategemea kocha atamudu vipi kuonesha uwezo wake kwenye mazingira ya aina hiyo?