Mkutano mkuu wa 20 wa Chama cha Kikomunisti cha China CPC utafanyika tarehe 16 Oktoba hapa Beijing. Lakini kabla ya kufanyika kwa Mkutano huo, ikiwa sasa watu wa China wanakuwa katika mapumziko ya siku saba ya kusherehekea miaka 73 ya kuzaliwa kwa taifa la China, siku ya taifa inayoangukia tarehe mosi, Oktoba, tuangazie mafanikio ambayo China imeyapata katika miaka hii 10 tangu Xi Jinping achaguliwe kuwa katibu mkuu wa Kamati Kuu ya CPC, leo hii tukiangazia suala la ujenzi wa miundombinu. Leo tutaangazia suala zima la maendeleo makubwa ambayo China imepata katika sekta ya afya.
China ni nchi ambayo imepata mafanikio makubwa katika kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Kwa mfano, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa China imefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malaria, baada ya juhudi za miaka karibu 70. Mwaka 1955, China ilizindua Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria, na sera kadhaa zilitekelezwa ili kuboresha mfumo wa umwagiliaji, kupunguzia maeneo ya mazalia ya mbu, kutumia viuawadudu na kutumia vyandarua. Kutokana na juhudi hizo, kesi za malaria zilipungua kutoka milioni 30 mwaka 1955 hadi 117,000 mwaka 1990.
WHO ilisema kwamba hakuna kesi ya malaria iliyoripotiwa nchini China kwa miaka minne mfululizo, na hivyo kuthibitisha kuwa nchi hiyo imefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa malaria. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dr. Tedros Ghebreyesus amesema mafanikio hayo ya China yametokana na juhusi kubwa, na yametimia baada ya miongo kadhaa ya malengo na hatua endelevu.
Licha ya kutokomeza ugonjwa wa malaria, China ni nchi iliyopata mafanikio makubwa katika kudhibiti virusi vya Corona (COVID-19).
Mara mlipuko wa ugonjwa huo uliporipotiwa mwishoni mwa mwaka 2019, serikali ya China, chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, ulichukua hatua kadhaa za dharura ambazo ziliweza kwa asilimia kubwa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.
Hatua kali zilichukuliwa na serikali ya China, ikiwemo kufunga baadhi ya miji, kuzuia usafiri wa kutoka na kuingia katika baadhi ya miji, na pia shughuli za kijamii pamoja na biashara zilifungwa. Kutokana na hatua hizi kali, maambukizi ya virusi vya Corona yaliweza kudhibitiwa, na kupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizi pamoja na vifo vinavyotokana na COVID-19.
China pia imepiga hatua kubwa katika matumizi ya Tiba ya Jadi ya Kichina (TCM) katika kutibu magonjwa mbalimbali, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa. Tiba hiyo ni utaratibu mzima wa matibabu ambao umetumika nchini China kwa maelfu ya miaka, na inajumuisha njia nyingi za matibabu ikiwa ni pamoja na tiba vitobo, tiba ya hijama, dawa za mtishamba, na Tai Chi.
Katika kutibu watu waliopatwa na maambukizi ya COVID-19, China ilitumia dawa za mitishamba pamoja na dawa za magharibi, na hivyo kufanikiwa kukwepa vifo vya watu wengi.
Tiba hiyo ya jadi imeendelea kuongezwa ubora wake, na inapatikana katika mfumo wa mitishamba, vidonge, na hata dripu. Kwa wenye dalili ndogo na za kati za COVID-19, dawa za mitishamba za Kichina ziliweza kuwasaidia kupona virusi hivyo.
Shirika la Afya Duniani limesema katika ripoti yake mwaka huu kuwa, TCM inaweza kuwa na manufaa kama msaada wa dawa za kawaida katika matibabu ya dalili ndogo na za kati za COVID-19.
Tiba ya Jadi ya Kichina imeendelea kupata umaarufu katika nchi mbalimbali duniani, zikiwemo nchi za Afrika. Watu wengi barani Afrika wameonyesha kuvutiwa na tiba hiyo na kuipendelea zaidi. Kwa mfano, nchini Namibia, madaktari katika hospitali ya Katutura iliyoko mjini Windhoek, wanashangazwa na idadi ya wagonjwa wanaovutiwa na tiba ya jadi ya Kichina, ambapo hospitali hiyo inapokea zaidi ya wagonjwa 100 wa aina hiyo kila siku.
Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu pekee, uagizaji wa bidhaa za tiba ya jadi ya Kichina nje ya nchi uliongezeka kwa asilimia sita ikilinganishwa na mwaka jana na kufikia karibu dola za kimarekani bilioni mbili.
Kutokana na sera makini na ufanisi katika utekelezaji, China imeweza kupata mafanikio makubwa katika sekta ya afya, na kuweza kujenga taifa lililo na watu wenye afya na nguvukazi bora.