SoC04 Huduma za Matibabu ya Kibingwa na Ubingwa Bobezi Nchini Tanzania: Faida, Changamoto na Mbinu za Kupata Matokeo Chanya

SoC04 Huduma za Matibabu ya Kibingwa na Ubingwa Bobezi Nchini Tanzania: Faida, Changamoto na Mbinu za Kupata Matokeo Chanya

Tanzania Tuitakayo competition threads

Cardalyn

Member
Joined
May 27, 2024
Posts
6
Reaction score
5
Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya, hususan katika huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi. Huduma hizi zinahusisha upasuaji wa moyo, upandikizaji figo, upandikizaji uroto, upandikizaji mimba, matibabu ya saratani kwa mionzi, na nyinginezo. Maendeleo haya yanachangiwa na mapinduzi ya kiteknolojia kama uwepo wa roboti na akili mnemba (AI).

Huduma hizi ni muhimu sana kwani huokoa maisha ya watanzania wengi, huimarisha afya, hurefusha muda wa kuishi, na hivyo kuimarisha nguvu-kazi ya taifa.

Changamoto

Ukosefu wa Takwimu za Wakati Halisi:
Takwimu nyingi zipo katika ngazi ya taifa, kanda, bara na dunia na haziakisi mazingira halisi ya Tanzania.

Ukosefu wa Maono na Mpango wa Utekelezaji: Maono ya wazi ndiyo dira inayoongoza utekelezwaji mzima wa mpango wa uanzishwaji, usimamizi na uendelevu wa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi zinazoanzishwa hapa nchini. Tunaweza kujiuliza maswali yafuatayo;
  • Kama maono ni yetu, Je tuna mpango wa uendeshaji, gharama, uendelevu, uboreshaji na mikakati ya kupata matokeo chanya?
  • Kama maono yametoka kwa mwekezaji, Je tuna mpango wa kuyatekeleza kwa namna inayoendana na uchumi na maendeleo ya Tanzania kwa sasa?
Uhaba wa Wataalam Wazawa: Ili huduma hizi ziwe endelevu, ni lazima kuwa na wataalam wazawa wenye nia ya dhati ya kuziendesha. Ukosefu wa mafao na rasilimali unawakatisha tamaa wataalam hawa, na hivyo kuongeza utegemezi kwa wataalam kutoka nje.

Ukosefu wa Mahitaji ya Uendeshaji: Huduma hizi zinahitaji mazingira safi, mashine za kisasa za matibabu (nyingi zinapatikana nje ya nchi), vifaatiba (vingi hutoka nje ya nchi na hutumika mara moja pekee), madawa, na timu kubwa ya wataalam. Hii inafanya gharama za uendeshaji kuwa juu sana.

Gharama za Matibabu kwa Wanufaika: Katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania, gharama za huduma ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi zipo juu sana kutokana na uchache, gharama kubwa za uendeshaji na hali duni za maisha, japo gharama katika nchi hizi ni ndogo ukilinganisha na nchi za Ulaya, Asia na Marekani.

Mbinu za Kupata Matokeo Chanya

Rasilimali-Watu Wenye Maono:
Ili huduma ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi iwe endelevu na yenye matokeo chanya, lazima iweze kujitegemea. Katika eneo la wataalam, kila idara lazima iwe na wataalam wazawa wenye maono, utayari na waliopata mafunzo rasmi katika fani husika wanaojifunza kutoka kwa timu ya wataalam wageni. Lazima uwepo mpango wa utekelezaji wa maono haya, unaoshahabiana na hali na mazingira ya Tanzania. Ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Hospitali za serikali, binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali ni muhimu katika kuanzisha na kuendesha huduma hizi kwa ufanisi.

Kuimarisha Huduma za Uchunguzi: Ili kupata matokeo chanya katika huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, ni muhimu kuimarisha huduma za uchunguzi wa mapema kwa mama wajawazito kabla ya kujifungua, watoto wadogo na utambuzi wa mapema wa dalili za awali kwa watu wazima.

Kuimarisha Mfuko wa Bima ya Afya na Kuanzisha Mifuko Midogomidogo: Sambamba na juhudi zinazoendelea za kuimarisha mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Serikali inapaswa kuanzisha mifuko maalum ya kugharamia huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi itakayosaidiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Mifuko hii inaweza kuendeshwa kutokana na kuweka sera itakayoruhusu kukusanya mapato yatokanayo na kuongeza asilimia kidogo ya kodi kwenye huduma za starehe kama vile utalii, michezo ya kubashiri, vinywaji vyenye kileo, sigara, na huduma za simu na mitandao. Pia kuboresha sera za makampuni za kutoa misaada kwa jamii na kutoa motisha wa punguzo la kodi kwa kampuni zinazofanya vizuri.

Kuimarisha Maslahi ya Wataalam: Maslahi ya wataalam waendeshaji wa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi yaboreshwe kutokana na vyanzo vya fedha tajwa hapo juu. Hii itawapa motisha wa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na weledi hivyo kuleta matokeo chanya na maendeleo ya haraka.

Kuimarisha Huduma Baada ya Kuruhusiwa Kutoka Hospitali: Huduma za matibabu ya kibingwa mara nyingi huhitaji wagonjwa kulazwa au kupumzika nyumbani baada ya kuruhusiwa. Katika kipindi hiki, ni muhimu wagonjwa wapate uangalizi mzuri majumbani ili matibabu yawe na matokeo chanya. Kuwashirikisha na kuwaelimisha familia na ndugu kunaweza kusaidia kuendeleza huduma bora nyumbani. Matumizi ya program za simu yanaweza kusaidia kutoa elimu ya huduma, kutuma taarifa mbalimbali za mgonjwa katika mfumo wa hifadhidata, na kuripoti dalili hatarishi.

Uimarishwaji wa Mfumo wa Hifadhidata:
Mfumo imara wa hifadhidata utasaidia kupata takwimu sahihi kwa wakati sahihi, zinazosaidia kufanya maamuzi sahihi ya uboreshaji. Mfumo huu uwe shirikishi kwa makundi yote yanayohusika kwenye huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi kuanzia ngazi ya vipimo vya mwanzo hadi ngazi ya huduma baada ya matibabu.

Wajibu kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Mashirika haya yana wajibu mkuu wa kuisaidia serikali katika kuhudumia wananchi. Hii ni pamoja na kuleta wawekezaji, wataalam, na kutengeneza mpango-fedha wa kupunguza gharama za huduma hizi.

Mikutano ya Mara kwa Mara: Mikutano ya mara kwa mara kati ya waendeshaji wa program za Matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi itasaidia kufanya tathmini ya matokeo yaliyopo, na kupanga mikakati ya maboresho.

Kuongeza Programu za Wataalam Kujiendeleza Kitaaluma: Wataalam wazawa waongezewe nafasi na ufadhili katika kujiendeleza kielimu kwenye eneo la matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi. Taasisi za elimu ya juu zianzishe/ziboreshe utolewaji wa programu hizi kwa kushirikiana na Taasisi za elimu za kimataifa.
Sambamba na hili, ni muhimu kuimarisha zaidi eneo la watoa huduma (nurses).
Pia, wataalam wanafunzi washirikishwe maono na uzoefu tangu wakiwa masomoni kwa usimamizi bora wa program kwa siku za baadaye.

Uwajibikaji, Uadilifu na Uwazi:
Ni lazima kuwepo uwajibikaji, uadilifu na uwazi katika uendeshaji wa huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi ili kuleta ufanisi na kuongeza ari kwa wananchi kuchangia huduma hizo.

Hitimisho

Ili Tanzania ifanikiwe katika matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, ni muhimu kuandaa maono yaliyo wazi, kuweka mpango thabiti wa utekelezaji, na kuweka sera zitakazoboresha vyanzo endelevu vya fedha kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni na wananchi.

Kwa kufanya haya, huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi zitakuwa endelevu na zitatolewa kwa gharama nafuu na hivyo kuwa suluhisho kwa watanzania kama Dkt. Devi Shetty alivyosema, "Ikiwa suluhisho si la bei nafuu basi sio suluhisho".
 
Upvote 3
Ukosefu wa Mahitaji ya Uendeshaji: Huduma hizi zinahitaji mazingira safi, mashine za kisasa za matibabu (nyingi zinapatikana nje ya nchi), vifaatiba (vingi hutoka nje ya nchi na hutumika mara moja pekee), madawa, na timu kubwa ya wataalam. Hii inafanya gharama za uendeshaji kuwa juu sana.
Hili ndo unaweza kuta ni tatizo kubwa zaidi. Maana baadhi ya kada unakuta wataalamu wapo lakini wanakosa vitendea kazi tu.

Matokeo yake kiuhalisi inakuwa ni kama hata hao wataalamu ni hawapo tu aani. Masikitiko.
Mifuko hii inaweza kuendeshwa kutokana na kuweka sera itakayoruhusu kukusanya mapato yatokanayo na kuongeza asilimia kidogo ya kodi kwenye huduma za starehe kama vile utalii, michezo ya kubashiri, vinywaji vyenye kileo, sigara, na huduma za simu na mitandao.
Lakini ni kwa nini kwenye afya kukagharamiwa na wanaotumia huduma hiyo hata kwa cost sharing? Nauliza kwamba je? Ni haki kweli mtu awe anabeti na hapo hapo anamlipia azuma mtu mwingine?🤯


Kuimarisha Huduma Baada ya Kuruhusiwa Kutoka Hospitali: Huduma za matibabu ya kibingwa mara nyingi huhitaji wagonjwa kulazwa au kupumzika nyumbani baada ya kuruhusiwa. Katika kipindi hiki, ni muhimu wagonjwa wapate uangalizi mzuri majumbani ili matibabu yawe na matokeo chanya. Kuwashirikisha na kuwaelimisha familia na ndugu kunaweza kusaidia kuendeleza huduma bora nyumbani. Matumizi ya program za simu yanaweza kusaidia kutoa elimu ya huduma, kutuma taarifa mbalimbali za mgonjwa katika mfumo wa hifadhidata, na kuripoti dalili hatarishi.
Hii point nzuri sana. Na kama mtu hana simu basi apewe hata vijarida kuhusiana na ugonjwa aliouugua akajisomee nyumbani. Vipeperushi vya elimu au app ni muhimu.
 
Back
Top Bottom