Huku kulialia kwa Waitara ni 'Presha' za Uchaguzi Mkuu 2025

Huku kulialia kwa Waitara ni 'Presha' za Uchaguzi Mkuu 2025

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Mjadala umeibuka kuhusu tabia ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kulia kila anapopata changamoto za utatuzi wa kero zake za kibunge, ambapo baadhi ya wanasaikolojia na wataalamu wa sayansi ya siasa; wakitilia shaka mtindo huo.

Hata hivyo, akihojiwa na Wasafi FM leo Mei 10, 2023, Waitara amesema kulia kwake siyo dalili za uoga bali ni ishara kwamba kakereheka na jambo fulani.

“Ni dalili kuwa jambo hilo limenikera…halijakaa sawa...limeniudhi…nikitoa machozi maana yake napata relief [ahueni] kwenye jambo ambalo naona hili limeniumiza sana…mie sijawahi kuwa muoga hata siku moja, na kimsingi siwezi kurudi nyuma katika mapambano,” amejitetea.

Mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri katika Wizara mbili tofauti toka 2018 – 2022, ameendelea kuaminisha umma kuwa kilichotokea ni sehemu ya namna alivyoumbwa, amesema: “…watu tumeumbwa tofauti tofauti…lakini ukienda kwa watu walisoma saikolojia na filosofia, utaelewa hiyo inamaanisha nini.”

Aidha, Waitara amekiri kuwa jambo hilo limemtokea mara mbili likimaanisha aliumizwa sana na jambo ambalo anaamini halikupashwa kutokea kwani ni kitu ambacho kilikuwa kinawezekana kufanyika.

Hapa ndipo msingi wa shaka za wanasaikolojia na wataalamu wa sayansi ya siasa unaposimama.

Kwa mfano, licha ya kwamba, Dk Edward Mushumbusi, mwanasaikolojia wa kujitegemea kukiri kuwa kuna ukweli usiopingika kwamba baadhi ya watu huachilia hisia zao za hasira kwa kulia, lakini anatilia shaka utetezi wa Mbunge huyo akisema ilipashwa kuwa ni tabia katika maisha yake.

“Ni kweli kuwa kuna watu pale ambapo hawaamini kile walichosikia, na wana hakika kuwa kisemwacho siyo kweli na si cha haki, hushikwa na hasira, na kwakuwa hawana namna nyingine ya kuiachilia hasira hiyo, hujikuta wanalia,” amefafanua mtaalam huyo mwenye makazi nchini Uingereza.

Ameongeza kusema: “Lakini jambo hili huanza toka wakiwa wadogo, hapo tabia hujengeka, siyo kitu mtu anaipata ukubwani. Na kwa asili ya harakati za Waitara, tungekuwa tumeliona hili, huyu alikuwa miongoni mwa washiriki wa mgomo wa wanafunzi mwaka 2002 uliosababisha Udsm kufungwa, lakini hatukuona akilia.”

Mushumbusi amehoji utetezi wa Mbunge huyo na kusema hauna mashiko kwani alipokosana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutimkia Chadema, hakuumizwa! Mbona hakuonekana akilia, lakini pia alipoondoka Chadema kurudi CCM, pia hakulia.

“Aliwahi pia kuwa Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa Tanga kwa nafasi hiyo hiyo na kupanda ngazi kuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga. Hata hivyo, alihamishiwa Dar es Salaama kama msaidizi wa Mwenyekiti UVCCM Taifa, kitu alichokiona kama ni udhalilishaji na kuhamia Chadema, huku nako hatukumuona akilia,” amehoji Dk Mushumbusi.

Aidha, mtaalamu huyo, anaamini kuwa ikiwa kulia ni tabia ya kiongozi huyo kama ishara ya kuondoa hasira zake na kupata ahueni, basi kwa maisha na harakati alizozifanya tangu akiwa shuleni mpaka kushika madaraka ya naibu waziri, staili hiyo ya ulizi isingeibua mjadala kwani lingekuwa ni jambo lililozoeleka.

Kwa upande wa Mwajuma Mwijalubi, mtaalamu wa sayansi ya siasa; anabainisha kuwa mtindo huu mpya wa kulia, ni mbinu itumiwayo na baadhi ya wanasiasa katika kuchochea, kushawishi ama kuhamasisha uungwaji mkono.

Japo anaamini pia kuwa machozi yaweza kumtoka mtu kutokana na hasira, pale anapohisi kuumizwa, kuaibishwa, kusalitiwa, au kutendewa isivyo haki. Hapa mchanganyiko wa hasira na huzuni husababisha machozi kutoka.

Hata hivyo linapokuja suala la Waitara, Mwijalubi amesema: “Hii ni mbinu ambayo kwayo, mwanasiasa hujaribu kupata uungwaji mkono, ni namna ya kupata huruma ya umma, unajaribu kuonyesha una uchungu sana na kwamba kuna vikwazo nje ya uwezo wako, hivyo umeamua kusimama upande wa umma.

Mawazo haya yanaungwa mkono na Fortunatus Mwita, Mkazi wa Tarime kwa kusema: “Binafsi ninaona haya ni machozi 'feki' (crocodile tears). Unajua watu wengi huchukulia watu wenye hisia za machozi, kuwa ni wakweli na waaminifu; sasa udhaifu huu ndiyo umesababisha wanasiasa kutuchezea akili hasa tunapotakiwa kufanya maamuzi.”

“Hata hivyo,” Mwita amesema: “Kadri siku zinavyokwenda, ufahamu unaongezeka na hivyo kuwa na uwezo wa kuyatambua machozi ya kweli. Huyu anajiandaa na siasa za 2025, hivi kipindi chote hicho alikuwa wapi kulia, ni mambo mangapi maovu yametendeka na amekuwa kimya?”

Mkazi huyu wa Tarime haungi mkono utetezi wa mbunge huyo na kusema: “Hii ni homa ya uchaguzi, jamaa anajua Mama (Rais Samia) ameleta mapatano, anajua uchaguzi ujao hakuna kubebwa, sasa afanyeje, wacha ajilize ili kupata huruma ya wananchi.”

Kwa mujibu wa Seif Ramadhan Mkazi wa Zanzibar anayejipambanua kama kama mdau wa siasa, amesema kuwa machozi katika siasa yaweza kuwa kweli au siyo kweli kutokana na tabia na hulka ya mtu mhusika.

Mdau huyu wa siasa anadhani katika matukio hayo mawili ya ya ulizi, Waitara anajaribu kutumia mbinu ya kutaka kuleta msukumo mahsusi na kuibua hisia za huruma toka ndani na nje ya chama kuelekea uchaguzi mkuu wa ujao.

Jana Mei 09, 2023 Mbunge huyo wa Tarime vijijini, alilia Bungeni akilalamikia Serikali kutoa majibu ya uongo kuhusu fidia kwa wapiga kura wake waliotakiwa kupisha mgodi wa Barrick North Mara.

Aidha, Mbunge huyo anayeonekana kutokuwa na msimamo, alilia hadharani pale alipokuwa akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, akipinga kitendo cha Meja Jenerali Suleiman Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Mara kusimamia uwekaji vigingi kwenye mpaka baina ya vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika wilaya ya Tarime bila ushirikishwaji wa wananchi, jambo linalopingwa na Mkuu Mkoa huo.

MWANANCHI
 
Hakika kabisa hilo halina ubishi, anatafuta huruma za chama na wananchi
 
Back
Top Bottom