Maeneo ya Buza, hususan Mwembeyanga, yamegeuka kuwa kitovu cha changamoto kubwa za kimazingira.
Mtaro wa maji machafu unaoanzia Mwembeyanga hadi karibu na Kituo cha Daladala cha Usalama unasababisha adha kubwa kwa wakazi na wapita njia wa eneo hilo.
Mtaro huu, ambao kwa kawaida unapaswa kusafirisha maji ya mvua, umekuwa tatizo sugu. Maji yaliyotuama ndani ya mtaro huo yamekuwa yakitoa harufu kali isiyovumilika, hali inayosababisha uvundo kila kona ya eneo hilo.
Tatizo hili limekuwa sugu kutokana na mtaro huo kuwa na miundo mbinu mibovu inayoshindwa kusafirisha maji ipasavyo.
Eneo hili linapakana na biashara nyingi, hasa za vyakula, jambo linaloongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa kutokana na mazingira duni.
Hali hii inawafanya hata wapita njia na abiria wanaopitia Mwembeyanga kulazimika kushika pua ili kukwepa harufu mbaya.
Malalamiko ya Wakazi na Wafanyabiashara
Nilipozungumza na baadhi ya wenyeji wa eneo hili, wakiwemo waendesha bodaboda kutoka Kituo cha Gereji, walionyesha kusikitishwa sana na hali hiyo.
Wanasema harufu kali kutoka kwenye mtaro huo inawakera, lakini hawana namna ya kurekebisha tatizo hilo kwa sababu mamlaka zinazohusika hazijachukua hatua stahiki.
Kwa mujibu wa wakazi hao, maji yanayotoka kwenye mtaro huo ni ya mvua ambazo hunyesha mara kwa mara, lakini hayawezi kupita kwa sababu mtaro umejaa uchafu na ni mbovu.
Ingawa hivi karibuni kulionekana juhudi za kuchimba na kusafisha mtaro, kazi hiyo ilikatizwa kabla ya kuzaa matunda.
Athari za Kiafya na Mazingira
Harufu inayotokana na maji yaliyotuama kwenye mtaro huu si tu inakera, bali pia ni hatari kwa afya ya watu wanaoishi na kufanya kazi katika eneo hilo.
Biashara za vyakula zinazofanyika karibu na mtaro huo zinaongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, huku hali ya mazingira ikizidi kuwa mbaya.
Wito kwa Mamlaka Husika
Ni dhahiri kuwa hali ya mtaro wa Mwembeyanga inahitaji kushughulikiwa haraka. Mamlaka za Manispaa ya Temeke zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mtaro huo unasafishwa na kurekebishwa ili kudhibiti maji yaliyotuama na kuondoa harufu kali.
Afya za wananchi na usitawi wa biashara za eneo hilo vinategemea juhudi za dhati kutoka kwa mamlaka husika.
Bila hatua za haraka, eneo hili linaweza kuwa kitovu cha mlipuko wa magonjwa na changamoto kubwa za kimazingira.
Nihitimishe Kwa kusema Mwembeyanga ni mfano hai wa Changamoto zinazotokana na miundombinu mibovu na ukosefu wa usimamizi thabiti.
Natoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hii na kuhakikisha mazingira rafiki kwa wananchi na wajasiriamali wa eneo hilo.