SoC01 Ifike hatua wanasiasa wetu wabadilike

SoC01 Ifike hatua wanasiasa wetu wabadilike

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Jul 20, 2021
Posts
5
Reaction score
13
Katika jambo linalotafakarisha sana ni kitendo cha wananchi kuburuzwa na wanasiasa kwa namna wanayotaka. Wanasiasa huwaona wananchi kama watu wasiojitambua wala kujielewa hivyo wanaamini wanaweza kuwaambia chochote na kuwafanyia chochote na wakakubali.

Ni jambo la kawaida sana kwa mwanasiasa kumuongopea mwananchi huku akifahamu wazi kuwa huyu anaemwambia hawezi kung'amua wala kuelewa kuwa hicho kitu anachoambiwa ni uongo. Kwa mfano katika kampeni za uchaguzi mwanasiasa huweza kuwaambia wananchi kuwa jambo fulani na fulani litakamilika muda mfupi tu baada ya kunichagua lakini ajabu ni kwamba inaweza kupita hata miaka 10 hakuna kinachofanyika. Huwa najiuliza sana kwa wanasiasa wanawachukuliaje wananchi wa kawaida.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba wananchi hawa ni wepesi sana kusahau madhila, ahadi za uongo na usaliti unaofanywa na wanasiasa. Bado nashindwa kuelewa Ni uchache wa fikra chanya au ni kitu gani, muda mwingine unaweza kwenda mbali zaidi ukahisi wanasiasa wanatumia uchawi kuwapumbaza wananchi kitu ambacho si kizuri kukiamini.

Profesa Noam Chomsky aliwahi kusema kuwa ukitaka kumtawala mtu kwanza mfanye mjinga kisha mtengenezee mazingira ajifaharishe kutokana na ujinga wake. Kauli hii inanipa wasiwasi zaidi kuwa huenda wanasiasa wanatumia fursa hii. Kwa mfano, ni jambo la kawaida wananchi kupoteza siku nzima katika barabara wakimsubiri mwanasiasa fulani ili tu awape maneno ya faraja, ajabu ni kwamba watu hawa husahau kuwa masaa wanayopoteza ndiyo mustakabali wao wa maendeleo yao lakini wenyewe huhisi fahari kwa jambo hilo.

Mwanafalsafa mmoja akiitwa Machiavelli aliwahi kunukuliwa akisema kuwa "watu wengi ni wajinga", akiwa na maana kuwa katika watu wengi au kundi la watu Ni wachache Sana wenye kujitambua. Hapa nazidi kupata mashaka na wasiwasi kuwa wanasiasa wameliona hili hivyo kutumia udhaifu huu kuwaburuza wengine.

Wanasiasa wetu kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakifanya vitendo ambavyo dhahiri shahiri ni dalili utwezaji wa wananchi. Hili halihitaji tochi kubwa kulimulika bali akili ya kuzaliwa tu. Mfano mzuri ni huu, siku za hivi karibuni kumekuwa na kile kinachoitwa kigeugeu cha wanasiasa katika misimamo yao, wapo ambao walikuwa wakiamini baadhi ya mambo katika kipindi cha awamu ya tano lakini ghafla tunaona leo wamebadili kauli ghafla bila sababu yakinifu. Hii ni kama kucheza na akili za wananchi kwamba hawawezi kuelewa kitu.

Nakumbuka kuna kijiji kimoja aliwahi kupita mwanasiasa mmoja mkubwa nchini, miongoni mwa kero zilizoibuliwa katika eneo hilo ilikuwa ni ubovu wa barabara ambayo iliahidiwa kuboreshwa kwa kiwango cha lami toka uongozi wa awamu ya kwanza. Cha kusikitisha ni kwamba mwanasiasa yule akatoa ahadi ambayo mpaka leo imekuwa hadithi tu. Mfano huu upo nchi nzima na hii ndiyo aina ya wanasiasa ambao tunao, watu ambao huhisi kuwa wananchi unaweza kuwaambia chochote na wakakubali.

Kuna mtu mmoja aliwahi kusema kuwa mwanasiasa ni wa pili kuingia motoni baada ya shetani hiyo siku ya hukumu kwani mwanasiasa ni vigumu sana kuwa mkweli na wengi wao hufanya kazi hiyo kwa lengo la kujinufaisha wenyewe. Licha ya utata wa kauli hii lakini kwa kiasi fulani inaakisi uhalisia wa mambo. Mwanasiasa kwake ni kawaida tu kutunga sheria Bungeni bila kuangalia ni jinsi gani wananchi wa kawaida wataathirika kwakuwa yeye mkono unaenda kinywani.

Imekuwa jambo la kwaida siku hizi katika nchi zetu zinazoendelea kuwa wanasiasa ndiyo wanaoishi maisha mzuri zaidi kuliko wafanyakazi wengine wote : Posho nzito, Mshahara na marupurupu ya kutosha. Lakini wakati haya yanaendelea kuna wananchi hata mlo mmoja unawashinda ila ajabu zaidi ni kwamba huyu anaeishi kifahari kwa pesa ya mlalahoi bado anataka kutengeza mbinu ya kuzidi kumnyonya yule asiye nacho.

NINI KIFANYIKE?
Kwanza kabisa wanasiasa hawana budi kuelewa kuwa nafasi wanazozipata ni kwa minajili ya kuwanufaisha wananchi na kuwaletea maendeleo na si kujinufaisha nakujipatia kipato au kugeuza siasa na uongozi kuwa chanzo cha ajira.

Pili, wananchi wanatakiwa kutambua kuwa wanasiasa ni watu wa kuwa nao makini hasa linapokuja suala la uchaguzi. Ni vema wananchi wakajitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kung'amua yupi anafaa na yupi hafai kupitia vitendo vyao na si maneno yao.

Aidha, wanasiasa ni vema wakajua kuwa zama zimebadilika, sasa sio kama zamani kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia watu wengi wamepata ufahamu juu ya tabia za wanasiasa na vitimbi vyao. Hivyo ile dhana kuwa wananchi ni watu wa kuburuza inaelekea kufutika.

Vilevile, wanasiasa wetu wanatakiwa kuzingatia kwamba binadamu wote ni sawa na hakuna ambaye yuko juu ya mwingine, hivyo itakuwa ni tusi kuwaona wananchi wa kawaida kama chanzo cha kujinufaisha na kujilimbikizia mali.

Mwisho kabisa, wananchi wanatakiwa kuwa na kauli moja ya kumkataa mwanasiasa yeyote watakapothibitisha kuwa hana manufaa kwao na yupo kimaslahi binafsi tu.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom