Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, .Jakaya Kikwete akimnadi mgombea Ubunge Jimbo la Igunga, Rostam Aziz kwa wananchi wa jimbo hilo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Igunga, mkoani Tabora jana.
Ibrahim Bakari, Igunga
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete amemsifu mweka hazina wa zamani wa chama hicho, Rostam Aziz kuwa ni mtu safi na aliyeenea kila sehemu.Kikwete alisemna hayo wakati akimtambulisha Rostam, ambaye anatetea kiti chake kwenye Jimbo la Igunga ambako amekuwa mbunge tangu mwaka 1995.
Kikwete alitua Igunga baada ya kukamilisha mikutano ya kampeni katika Jimbo la Igalula na Tabora Kaskazini katika mkoa wa Tabora.
Akimnadi Rostam mbele ya halaiki kwenye mkutano uliofanyika Igunga Mjini, Kikwete alisema kuwa Rostam 'ameenea' na anaweza, hivyo wananchi wa Igunga hawana sababu ya kuacha kumpa kura.
"Rostam ni kama timu iliyoenea, timu iliyokamilika kila idara, sasa mnataka nini tena...mnamfahamu, anawasaidia ni mtu wa watu, anawapenda," alisema Kikwete na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho waliofurika kwenye mkutano huo.
Kikwete alisema pia kuwa angeshangaa kama wanachama wa CCM wasingempa nafasi ya kuwa mbunge wa chama hicho.
Kwa upande wake Rostam alimsifu Kikwete kwa uongozi safi na kueleza kuwa yuko tayari kuwatumikia wananchi wa Igunga katika kipindi kingine cha miaka mitano na kwamba Kikwete asisumbuke kuwaza kura za Igunga kwani zipo asilimia 99.99.
"Nimepita katika kata zote 26 za Igunga, wananchi wamenihakikishia kuwa kura zote ni za CCM, usiwe na wasiwasi... usihofie porojo za majukwaani," alisema Rostam huku akishangiliwa.
Pia Rostam aliahidi kusaidia ujenzi wa daraja la Mbuto linalounganishanisha Wilaya ya Igunga na Shinyanga.
Awali katika mkutano wa kwanza kwenye Jimbo la Igalula pamoja na Tabora Mashariki, Kikwete aliwataka wananchi kutochagua vyama alivyoviita vya wanung'unikaji na wanaohubiri kumwaga damu.
"Wenye vyama hivi hawana sera, wao ni wadandiaji sera na wanung'unikaji tu, hawana kipya wakati mwingine wanahubiri kumwaga damu. Sasa hakuna damu itakayomwagika kwa mtu wa kawaida na hata hao wanaohubiri," alisema.
Akizungumza hali za wakulima, Kikwete alisema kuwa serikali itabeba madeni yote ya vyama vya ushirika na kuwapa fedha ili kuwapa nguvu wakulima waweze kuuza mazao yao kwa kuwa vyama vya ushirika sasa vimeshapata uwezo na vinakopesheka.
Kwa upande mwingine, Kikwete alisema kuwa serikali imetoa ruzuku ya mbolea ya Sh40 milioni kwa wakulima wa tumbaku na mazao mengine. Hata hivyo alitoa ahadi mbalimbali za maji na barabara.
Akiwa njiani kwenda Kiomboi mkoni Singida, Kikwete alisimama katika Kijiji cha Makomelo na kuelezwa shida ya maji inayowakabili wananchi wa kijiji hicho.
"Haya nielezeni matatizo yenu, mnataka tuwafanyie nini," alisema Kikwete na baadaye akampatia kipaza sauti mama mmoja na kusema: "Sisi hapa kama unavyotuona, tunataabika kwa maji... tunaomba sana utupatie maji."
Kikwete alisema: "Nimeyasikia, sasa nachukua 'notebook' yangu na kalamu, ninaandika na matatizo yenu nitayashughulikia."
Kata ya Shelui, Kikwete alisimama tena na mwenyekiti wa Kijiji cha Mselebwe, Said Tunu alipewa nafasi azungumze matatizo yao na kuyataja kuwa ni pamoja na ukosefu wa maji katika vijiji sita, barabara na zahanati.
Hata hivyo, Kikwete alisema kuwa atakachofanya ni kuwasaidia kujenga kituo cha afya na kuwataka wananchi kukaa na halmashauri yao kwa ajili ya ujenzi huo wa zahanati. Leo atakuwa Singida mjini.
Chanzo:
Kikwete amtakasa Rostam, ASEMA NI MTU SAFI ALIYEENEA KAMA TIMU YA MPIRA