SASA ni dhahiri kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimenusa harufu ya kifo. Methali isemayo siku ya kufa nyani miti yote huteleza, inaendana sawasawa na hali ya CCM, si Igunga tu bali nchi nzima.
Kila kifanyacho hakielekei kufanikiwa. Sasa kinatumia hata uongo usio na nguo kwa kumtumia Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama, kudai eti CHADEMA imepeleka makomandoo 33 huko Igunga, baada ya kupata mafunzo katika nchi za Afghanistan, Libya na Palestina ili kufanya vurugu wakati kampeni za ubunge wa jimbo la Igunga zikiendelea jimboni humo!
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekanusha si kupelekewa orodha ya makomandoo hao tu bali hata kusikia kutoka kwa askari wao waliopo Igunga juu ya watu hao. Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Jeshi la Polisi nchini, Isaya Mungulu, amewataka wanasiasa kutoliingiza jeshi hilo katika propaganda za kisiasa.
Hii inathibitisha kuwa tangu Phillip Mangula alipoondoshwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, nafasi yake haijapata mwanasiasa mkomavu anayejua kuchambua mbivu na mbichi katika medani za siasa. Kwa kujua umuhimu wake, sasa CCM kimemwangukia na kumpeleka Igunga akapange na kusimamia mikakati ya ushindi.
Baada ya Mangula aliletwa mgosi Yusuph Makamba. Huyu alikuwa mwingi wa nahau za Kisambaa na nukuu za Biblia Takatifu na Kurani Tukufu lakini alishindwa kabisa kuendeleza pale alipoachia Mangula. Ilipoonekana CCM kinakwenda arijojo, Makamba akalazimishwa kujiuzulu na nafasi yake akapewa Wilson Mukama asiyejua lolote kuhusu fitna za siasa na badala yake amezua uongo wa karne.
Huko anakodai Mukama kuwa CHADEMA imepeleka makomandoo Afghanistan, Libya na Palestina ni nchi zilizo katika machafuko makubwa hivi sasa. Ni vipi nchi hizo zaweza kutoa mafunzo kwa makomandoo wa kigeni ilhali kwao kuna vita? Makomandoo ni wanajeshi wanaofunzwa mbinu za kupambana na mazingira magumu kama vile uokoaji au upelelezi.
Wakati Chama Cha Mapinduzi kikikilaumu CHADEMA kwa kuchochea vurugu na ubaguzi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja mstaafu, Bahati Matala, alimdhalilisha Diwani wa Kata ya Majengo, Bobson Wambura (CHADEMA), kwa kumtimua jukwaani wakati wa mkutano wa hadhara. Ilikuwa kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru mpaka pale Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, Andrew Masanje, alipompinga akisema maadhimisho yale ni kwa Watanzania wote na si ya wanachama wa CCM pekee.
Ili kuonesha jeuri ya kuwa juu ya sheria, Mbunge wa Tabora Mjini, kwa tiketi ya CCM, Aden Rage, alipanda jukwaani huko Igunga akiwa ameningniza bastola yake kiunoni mithili ya wale cowboys wa Marekani.
Kwa sheria za Tanzania, ni kosa la jinai kuonesha silaha hadharani hasa panapokuwa hapana machafuko. Rage alikuwa kwenye mkutano wa kampeni wakiwapo askari wengi tu lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake. Kitendo hicho kingefanywa na wapinzani ingekuwaje?
Mbunge wa Mtera kwa tiketi ya CCM na ambaye pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho, Livingstone Lusinde, kama kawaida yake ya kuwadharau na kuwatukana watu waliomzidi umri, alimtukana vilivyo katibu mkuu wa CHADEMA kwa kumwita mnafiki mkubwa. Mnafiki ni mtu mwongo mwenye matendo yaliyo kinyume na matendo yake.
Akasema: Kale kazee kagonjwa kale, ndiyo maana nimekuja (Igunga) kuwaambia inawezekana viongozi wa CHADEMA wanavuta bangi
zile ni bangi zile. Haiwezekani unatembea nchi nzima unahamasisha vurugu, unatangaza vita.
Lusinde amewafumbua macho Watanzania. Kumbe viongozi wa CCM wanapozunguka nchi nzima kutoa ahadi zisizotekelezeka huwa wamevuta bangi! Mwalimu Nyerere alipoacha kazi ya ualimu na kutembea Tanganyika nzima akihubiri ubaya wa ukoloni na umuhimu wa kujitawala wenyewe na hatimaye wananchi wakamwelewa na kupata uhuru alikuwa mvuta bangi? Kumbe kilichomtoa Mtera, Dodoma na kwenda Igunga, Tabora kutukana watu ni baada ya kuvuta bangi!
Lusinde hakuvuta bangi tu bali alichanganya na afyuni (dawa ya kulevya inayotengenezwa kwa uteute au nta ya maua; kasumba) iliyomfanya atoe siri za CCM kwenye mkutano wa hadhara akiwaambia waandishi wa habari kuwa: Nataka mkaandike kwa namna ambavyo tumezunguka
CCM tukishindwa, nakunywa sumu.
Lusinde alijiamini nini mpaka kusema maneno mazito kiasi hicho? Ni kutokana na kununua shahada za wapiga kura na kuhakikisha wamefaulu kuwatisha wapiga kura kutowapigia wapinzani kwani wao (CCM) ndiyo walioshika dola na kwa hivyo Jeshi la Polisi limo mikononi mwao! Hivi Lusinde anajua kuwa maneno yanaumba? Je, CCM kikishindwa, Lusinde atakuwa na ubavu wa kunywa sumu kama alivyowaahidi wananchi? Tunasubiri kuona msiba wake.
Kinachoshangaza ni kwamba wakati wa kampeni CCM imewaahidi wakazi wa Igunga mambo mengi mno. Kwani matatizo ya wananchi wa Igunga yamezuka kipindi cha kampeni? Wapiga debe wa CCM walikuwa wapi kabla ila wanajitokeza sasa wakijinadi kuwa watapeleka maji, umeme, chakula, elimu na matibabu ya bure Igunga?
Ili kujua CCM ni sawa na mfa maji, mbunge wao wa Ludewa, Njombe, Deo Filikunjombe amesema matumizi makubwa ya mamilioni ya fedha kwa ajili ya kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika ni sawa na usaliti.
Anasema wizara kuandaa maonesho ya sherehe ya miaka 50 ya uhuru huku Mtanzania wa kawaida aliye kijijini akiishi maisha magumu si sahihi.
Akapasua jipu kwa kusema hakuna haja ya kusherehekea miaka 50 ya uhuru wakati hakuna huduma muhimu za kijamii na watu wanaishi maisha duni kutokana na ahadi zisizotekelezeka.
Alilaumu tabia ya baadhi ya mawaziri wanaofanya sherehe kubwa za kujipongeza kwa kuteuliwa kuwa inachangia kuporomosha misingi na maadili ya taifa na hata wakati mwingine hufikia kutumia fedha za walipa kodi kwa ajili ya anasa. Filikunjombe anasema ni vema nafasi za uwaziri, ukuu wa mikoa na wilaya wapewe watu wenye mioyo ya uzalendo na uchungu wa nchi yao lakini imekuwa tofauti.
Mungu hamfichi mnafiki. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, Kikwete alizunguka nchi nzima akilalamika kuwa baadhi ya vyama (akimaanisha CHADEMA) vinafanya kampeni za udini. Akawatahadharisha Watanzania wajiepushe nao kwani ni hatari. Hakuwa na ujasiri wa kumtaja yeyote aliyekuwa akihubiri udini.
Sasa huko Igunga, baada ya kuona maji yamezidi unga, viongozi wa CCM waliwaita viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwenye Hoteli ya Peak Lodge ili kuomba msaada wa Waislamu kwa madai kuwa CHADEMA haiwapendi ndiyo maana wafuasi wake waliangusha hijabu ya Mkuu wa Wilaya, Fatma Kimario!
Ni CCM haohao walioeneza uongo kuwa CHADEMA inaeneza siasa hatari za udini na ni haohao CCM leo Mungu amewaumbua mchana kweupe wakiwaghilibu viongozi wa Bakwata waisaidie kuwahamasisha waumini wao kutokipigia kura CHADEMA. Je, hawa ni watu wa kuaminika?
Hili ni fundisho zuri kwa watu wa Igunga. Tunajua wengi wamepewa fedha, vyakula, fulana, vitenge, khanga, kofia. Wengi wameghilibiwa na kunyanganywa shahada zao za kura na wengine kuchukuliwa namba za shahada zao kwa lengo la kuzitumia wakati wa kuhesabu kura ili kuongeza kura za mgombea wa CCM ashinde. Wakazi wa Igunga wameambiwa uongo mwingi kama ule wa Wilson Mukama na wamepewa vitisho vingi kama Rage alivyopanda jukwaani akiwa kaninginiza bastola kiunoni kutisha wananchi ili wasiwapigie kura wapinzani!
Kama chama hicho kimeshindwa kuleta maisha bora kwa wananchi wa Igunga kwa miaka 50 iliyopita, kitawezaje kuleta maendeleo yasiyotekelezeka kwa miaka minne iliyobaki kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015?
Wananchi wa Igunga wasitishike kwani debe shinda haliachi kutika. Wawaangalie wenzao wa Malawi walivyoiondoa serikali kwa kura na sasa wale waliokuwa wapinzani sasa wanaitwa serikali.
Waliokula, hakuna kilichosalia matumboni. Waliopewa hela zimekwisha na waliopewa khanga na fulana ni vitu visivyoweza kuwashibisha leo wala kesho. Wakatae ghiliba zote hizo, wakinyime CCM kura kwani nyumba inapozeeka, usingoje ikuangukie ukiwa ndani. Jenga nyingine iliyo bora zaidi; na ujenzi wa nyumba nyingine ni kuachana na CCM na kuchagua upinzani.
Kama wapinzani watashindwa baada ya miaka mitano, watawekwa kando na kuchagua chama kingine. Wakati huo angalau CCM kitakuwa kimejifunza kutokana na makosa yake. Kazi kwenu wana Igunga. Kumbukeni kuwa uongo hauongoi na CCM kimewadanganya mno wananchi. Ni wakati sasa wa kukiweka pembeni ili kijifunze kutoka kwa wengine. Kura ni siri. Mkipewa fedha chukueni lakini chagueni upinzani.
Source :Tanzania Daima