Sugu apewa saa 72 kuomba radhi
na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI wa Kampuni ya Kupromoti na Kuendeleza Vipaji vya Wasanii (THT), Ruge Mutahaba, amempa saa 72, msanii maarufu nchini, Joseph Mbilinyi Sugu ili amwombe radhi kwa kumchafulia jina.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mutahaba alisema amefikia uamuzi huo baada ya Sugu kumhusisha na masuala ya kitapeli.
Nimeamua kumpa Sugu saa 72 aniombe radhi kwa kunichafulia jina na kazi yangu, ambayo ndiyo ninayofanya kila siku, kwa vile maneno yake yanaonekana dhahiri kuniharibia heshima mbele ya jamii, alisema Mutahaba.
Yaliyosemwa yameniathiri sana kikazi, namuomba Mr. II na William Mungai waniombe radhi kwa kunichafua katika vyombo vya habari, nawaomba wafanye kwa uzito ule ule, alisema Mutahaba.
Alisema, kama Sugu hatafanya hivyo katika muda aliotoa, atawasiliana na wakili wake na kuona hatua za kisheria za kuchukua.
Alifafanua kuwa Kampuni ya Round Trip ndiyo iliyompa kazi ya kutengeneza jukwaa, taa pamoja na kupeleka wasanii wa THT kwenye uzinduzi wa mradi wa Zinduka Malaria Haikubaliki uliofanyika Februari mwaka huu kwenye viwanja vya Leaders Club na si vinginevyo.
Hivi karibuni mara baada ya mradi wa Zinduka kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, yameibuka malalamiko ya Sugu kuibiwa mawazo yake aliyoyaandaa na taasisi ya Malaria No More ya Marekani, huku watu kadhaa wakihusishwa na sakata hilo.
Kwa uamuzi huo, Mutahaba anakuwa wa pili kutoa kusudio la kumshitaki Sugu, baada ya hivi karibuni Malaria No More nao kutangaza azima hiyo.
Source: Tanzania Daima 13/03/2010