ushauri wangu, uchambuzi wangu na matusi na hata kumfanyia maskhara, hawajibiki kusikiliza ninachosemana anaweza kukipuuzia maana si kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Ama kwa mtaji huo huo, si ushauri na lawama za Mchungaji pekee, bali ni za kila mtu, Mzee Mwanakijiji, Dr. Slaa, Lipumba hata Mzee Mwinyi, Kikwete ana hiari ya kutusikiliza au kutokutusikiliza. Aidha hata ushauri kutoka kwa watendaji wa Serikali na washauri wake, kama si sheria na kwa mujibu wa katiba, Kikwete hana ulazima wa kusikiliza na kutimiza ushauri anaombiwa na kuaswa.
Kwa mtaji wa kinga hii, ndio maana nakuja na hoja mpya, tena baada ya yeye Kikwete kuamua kugombea tena na nasema wazi, ningekuwa mimi Kikwete, nisingeligombea Urais kwa uchaguzi huu wa mwaka 2010, ningejichukulia muda wangu nikaka pembei nifurahie mafao na marupurupu ya Urais nikijipanga upya.
Sina maan aya kusema kuwa Kikwete ni mtu bora au kafanya kazi bora na anastahili Urais mara ya pili, la hasha! Bali ni jitihada zangu za kumshawishi asikie ushauri na maoni ya watu ili aweze kuwa kiongozi bora na kuheshimika.
Leo hii kama Kikwete angejionda kugombea urais kwa sababu yeyote ile anayotaka, angeheshimika sana na tena kuogopeka hata kama ukweli ni kuwa angekuwa anaficha udhaifu na kuikimbia aibu ya utendaji mbaya wa Serikali yake na maamuzi yake yasiyoeleweka na yasiyo na manufaa kwa Taifa.
Sababu ya kumrudi aleo Kikweta siku anayoanza rasmi kufanya kampeni yake ni kuonyesha wazi kuwa ni wapi ule ushindi wake wa mwaka 2005 wa Tsunami haukuwa na manufaa yeyote kwa Mtanzania na haukuleta tija au ufanisi kama alivyodai kwenye kile kiitikio chake cha Ari, Kasi na Nguvu Mpya.
Kuna Mmarekani mmoja anaitwa James Carville, ambaye alikuwa meneja wa kampeni za uchaguzi kwa Bill Clinton alipokuwa akigombea Urais mwaka 1992 na alitoa kauli moja ninayoipenda na ndiyo ilitumika kwa kampeni ya Clinton an akamshinda Rais aliyekuwa madarakani Geroge Bush wa kwanza. Kauli mbiu aliyoileta James Carville kwenye ule uchaguzi ilikuwa ni hii "its the economy stupid"
It's the economy, stupid - Wikipedia, the free encyclopedia
Hi kauli mbiu, ndio nitaitumia leo hii kueleza na kufafanua kuwa kwa nini Kikwete ilimpasa asigombee tena na akae kando mwaka huu.
Katika mahubiri ya" Ari, Kasi na Nguvu Mpya" Kikwete aliwatamanisha Watanzani kuwa katika utawala wake, wataina nuru ya maendeleo na kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania yatafanikiwa.
Mimi ni mpenda takwimu, uchumi na hisabati bandia, si mtaalamu bali ni mbwabwajaji ninayependa kusoma magazeti, hotuba vitabu na utundu wa kupekenyua vitu na kuvichambua na kuvijengea maana.
Ukisomayale ya Utopia na S Cre w Muungwana, utabaini wazi kuwa nilitoa ushuhuda wa kiuchungaji kuwa Kikwete hawezi kuliongoza Taifa na kutufikisha katika mafanikio. Mbaa i lile la Utopia nililolito asiku moja baada ya yeye kuapishwa.
Alipoigia madarakani, hazina ya Serikali na deni la Taifa halikuwa hatika hali mbaya ambayo leo hii pamoja na kujigamba kuwa kajenga shule za kata kila kona, kajenga Chuo Kikuu Dodoma na ahadi nyingi, leo hi hali ya Mtanzania kimaisha na mapato na deni la Taifa vinaendeleakuwa vibaya na vinatishia usalama na uhai wa Taifa letu.
Je Kikwete alitufaa kuwa Rais wetu mwaka 2005, jibu ni rahisi sana, hapana kwa kuwa Kikweta si Rais wa kutufaa Tanzania ya leo ambayo inabidi tupige hatua marudufu kujijenga kiuchumi ili tujitegemee na kuondokana na Ujinga, Maradhi na Umasikini.
Labda kwa mtindo wake wa uongozi, labda Kikwete angefikirika kuwa labda anafaa miaka 500 kutoka leo hii ikiwa Tanzania ingekuwa na mfumo wa uchumi na kiutendaji ulio na ufanisi kama wa Marekani, China, Japan, India, Brazil, Ujerumani na hata sayari ya Zebaki.
Tanzania baada ya Mkapa ilitakiwa kupata Micro manager President na si Macro manager the delegator, the unethical, the inneficient, the unmotivated, lazy, laid back President who can not follow up or demand accountability (mnisamehe kwa kuongea Kimombo).
Katika miaka mitano ya Kikwete, ameshindwa kusukuma gurudumu la maendeleo la Taifa kwa manufaa ya Taifa na Watanzania wote. Kasukuma kwa juhudi gurudumu la maendeleo la Wawekezaji wa nje wanaotunyonya hazina yetu na mbaya zaidi kasukuma kwa bidii gurudumu la maendeleo ya wahujumu wa ndani mafsidai na wahujumu wa nje kwa kushindwa kuwa Rais mwenye kufanya maamuzi magumu na kwa manufaa ya Watanzania.
Alipokuja, alianzakutumbua zile ziada ya Hazina kwa kuunda Serikali kubwa mno, akidanganya Watanzania kuwa anataka kila kabila, dini na jinsia ipate wawakilishi, huku ukweli alikuwa analipa fadhila za wale waliokuwa kwenye mtandao wa kumfanya awe Rais.
Katika kulipa fadhila hizi, udhalimu wake wa kuchekea kila mtu na kujifanya mtu wa watu ukaanza tangu Januari ya mwaka 2006, kwa kutokea mpasuko na mgawanyiko katika Serikali yake na kugombea madaraka kwa makundi mawili huku kila kundi likifanya jitihada kuhujumu lingine na kuvuna kwa bidii hazina za Taifa kwa kutumia madaraka na dhamana ya kuongoza.
Alichofanya Kikwete kama Rais au Mwenyekiti wa CCM ni kukaa kando akitafuta uluhisho la win win situation kwa kila kundi na akiyachekea makundi yote bila kusimika mguu wake chini na kufuta mvurugano huo au kukosekana kwa udailifu na umakini kutoka Chama na Serikali yake.
Hivyo hapo tunagundua kuwa pamoja na kuwa anadai yeye ni mchumi, lakini ni mfujaji mkubwa na madai kuwa alitumia miaka 10 kujifunza Urais na ukiongezea ile mingine tangu akiwa Katibu wa Chama Singida, bado hakuwa amejifunza kitu chochote cha kuwa iongozi mahiri bali ni kiongozi ambaye amedhihirisha kuwa ni mwepesi wa kukwepa kazi, ajukumu na lawama na kuachia wengine wabebe huo mzigo.
Je tutaendeleaji kumuamini yeye kuwa atakuwa Jemedari mwenye busara na ukomavu wa kufanya maamuzi yenye kuleta maana na msingi tukiwa vitani? Kama yeye ni kama Kunguru mwoga, kazi kuficha ubawa, iweje leo kwa akili zetu timamu tumpe Urais kwa miaka mingine mitano?
Wala sitapoteza muda kuongelea Ufisadi zaid ya kusema kwa Watanzaiakuwa kumchagua Kikwete, ni kukiri wazi kuwa mmeridhika na maisha ya shida, ya umasikini yaliyojaa maradhi, ujinga ufukara na mmeridhika na mfumo wa kifisadi ambao unawahujumu kila siku nanyi mwabakia kusema liwalo liwe, n imapenzi ya Mungu!
Nitarudi kwenye Uchumi. Takwimu za mwezi uliopita za Benki Kuu, zinaonyesha deni la Taifa likiongezeka marudufu huku uwezo wetu wa kulilipa ukipungua kwa kazi ya hali ya juu, mapato yetu yakiendelea kupungua na matumizi yetu yasiyo ya kimaendeleo yakiongezeka kwa ari, kasi na nguvu mpya na za ajabu na hakuna anayeliona hili kama ndilo tatizo kuu la Tanzania kushindwa kupiga hatua mbele za kimaendeleo kiuchumi.
Katika miaka yake minne ya Kwanza, Rais Kikwete alitumia muda huo kutalii kuiona dunia na kuiza Tanzania kwa wawekezaji. Katika kipindi hicho, kwa maoni yangu ametumia si chini ya dola za kImarekani Milioni 50, kuzunguka dunia kutafuta wawekezaji, huku akisahau kuwa alipaswa kuanza kazi kule vijijini ambako alikuja na kuzunguka nchi nzima akiahidi maisha bora kwa kila Mtanzania.
Inafahamika kuwa Kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa na wakulima na waishio vijijini ni takriban asilimia 75 ya Watanzania na karibia asilimia 85 ya hawa waishio vijijini kama wakulima, wavuvi ,wahunzi, wafuaji na kazi nyingine za mashambani, wanaishi maisha duni kwa kipato cha cha sikukuwa chini ya Dola moja ya kimarekani na ni hawa ambao hufanya na kuishi maisha ya kujikimu, huku wakiwa hawana huduma bora za afya, elimu, miundombinu, maji na hata uwezo wa kuuza mazao na wanachozalsha.
Ni karibu na katikati ya mwaka 2009, ndipo Kikwete akazinduka na kuanza kutembelea nchi yake kila kona akidai Kilimo Kwanza na kuwakimbilia tena Wawekezaji wa nje waje kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwa ahadi zile zile za wachimba madini za kuruhusiwa kuvuna wanachokitaka kwa malipu finyu kwa kipato cha Taifa.
Ni Kikwete huyu huyu alilyeingia madarakani na kusema angerekebisha mfumo wa mapato utokanao na sektta ya madini lakin baada ya miaka miwili ya kamati na kutafakari, kaongeza kipato kwa asilimia moja tu, huku nchi zingine maato yao ni mpaka asilimia 40 kwa kila udongo au kimiminika kinachichimbwa.
Bajeti yake imeendelea kuwa ni tegemezi kwa wafadhili na kwa vituko, mwaka huu 2010 baada ya kukosa msaada kutoka wka Wafadhili, Serikali yake imekwenda kwa Mabenki binfasi na kukopa dola Milioni 250 kukidhi mapungufu ya Bajeti, lakini hapo hapo, tunanunua magari mapya na samani mpya kwa kila Mbunge na Waziri!
Kikwete anaahidi vitu vingi sana, na kajenga shule nyingi sana lakini thamani ya ahadi au alichokifanyia kazi, hakionekani si leo tuu hata huko mbeleni haiwezekani kuonekana labda katika miaka 100 baada ya deni la Taifa kulipwa.
Kiuwajibikaji na kuwajibisha watu na watendaji, huko alikaa likizo. Kikwete katika miaka yake mitano, ametuachia taswira ya Rais ambaye hakuwepo nchini mwake wala kujua linaloendela nchini mwake. Ni sawa na Baba au Mama asiyejua knachoendela nyumbani kwake na wala hana nia ya kujua kinachoendelea.
Amefanya maamuzi na teuzi ambzao hazikuwa na tija, kaliingiza Taifa hasara kutokana na maamuzi mabaya ambayo badaa ya kukiri kufanya makosa, aliyasukumiza kwa wengine na kujiosha mikono.
Kaonyesha udhifu wa hali ya juu kushughulikia suala la Uhujumu, Rushwa na Madawa ya kulevya. Kawakumbatia watendaji wambao kwa makusudi au kwa kiburi wamelitia Taifa hasara kubwa kutokana na uzembe wa kikazi na tamaa binafsi.
Maisha ya Mtanzania iwe ni mjini au vijijini ni ya kubahatsha kwa sehemu kubwa. Dar Es Salaam maish ani mdongamano kila siku, bei za chakula zinaongezeka, gharama za umeme zinaongezeka maradufu, magonjwa yanaongezeka, mafisadi wanaendelea kutamba na kuendeleza mikakati ya kuhujumu na zaidi yeye mwenywe kwa mdomo wake alikiri kuwa asilimia kubwa ya Bajeti ya Serikali yake hupotea kwa rushwa na hakuna udhibiti wa kutosha.
Ninachojiuliza ni hili, zile mbwembwe za kudai yeye na Serikali yake ni ya kwanza kutoa taarifa hadharani za mdhibiti mkuu wa mahesabu zilikuwa za manufaa gani ikiwa mapendekezo ya mdhibiti mkuu hayajafanyiwa kazi na kila mwaka tunaona kuongezeka kwa kuvunjwa kwa kanuni za kibajeti na mahesabu?
Je tutasema tuna kiongozi hodari, shupavu, mkakamavu na mchapa kazi? au tunafurahia kuwa na kiongozi goigoi, zezeta, zuzu, zobwe, zembe, bangaizaji na mwoga?
Alichokifany acha maana sana na hiki sitasita kumsifia ni kutupa uhuru wa kutoa maoni na kubwabwaja, iwe ni ukanjanja au la, lakini tumeweza kujifunza mengi na kujifahamu kama Taifa kwa kuwepo kwa "uhuru" huu bandia usio na mafanikio kwa yeye kuwa msikivu na kujituma, maan akifungu cha 37.1 kina mlinda!
Kama mimi ningekuwa mgombea urais wa chama chochote dhidi ya Kikwete, ningewauliza Watanzania swali kuu moja "je wanaridhika na maisha yao, mfumo wa kiuchumi, utendaji wa Serikali na hatima ya Taifa lao?
Kama wakinijibu, ndio, nitawaambia waendelee na maisha yao ya kufurahia dhuluma, dhiki, ufisadi na umasikini kwa kumchagua Kikwete na kukipa CCM dhamana ya kuongoza Taifa kwa kuwachagua wabunge wa CCM.
Kama wakijibu hapana, ndipo ningewaambia kwa nini basi wanaendelea kuikumbatia CCM?
Lakini lengo langu si kuanza kampeni bali ni kuhalalisha kwa ni ni Kikwete alipaswa kutogombea mwaka huu.
Ni aibu kubwa kwa mtu yeyote makini kudhani kuwa miaka mitani ya kwanza ya Kikwete ilikuwa ya manufaa kwa Taifa na Watanzania. Ni aibu kubwa kwa Kikwete mwenyewe kudhani kuwa amefanya kazi nzuri sana na anastahili apewe miaka ya nyongeza papo hapo baada ya kutumia miaka mitatu kujifunza kazi, kitu ambacho alipokuwa anagombea mwaka 2005, aliliambia Taifa kuwa ametumia miaka 10 kujifunza kazi an alikuwa tayari.
Kama anekuwa msikivu wa ushauri, ningeandika hili mapema sana, tena mwanzo ni mwa mwaka kwa kumtaka asigombee mwaka huu, achukue likizo, akae chini atafakari na kufanya tathmini ya kweli, kama nafsi yake ina dhamira ya kweli na ajiulize ni kitu gani cha msingi na manufaa alikifanya katika miaka mitano yake aliyokuwa Rais.
Kama leo umasikini unaongezeka, hujuma na ufisadi unaongeeka, deni la Taifa linaongezeka, matumizi yasiyo ya msingi au kimaendeleo yanaongezeka, ukosefu wa tija, ufanisi, uwajibikaji, nidhamu ya kazi na kuheshimu dhamana kunaongezeka, ujinga na maradi yanaongezeka, tabu, shida, karaha, kutokuaminiana kunaongezeka, iweje leo akimbilie kusema nipeni miaka mingine mitano, tena kwa kiburi cha kuwaambia wengine sihitaji kura zenu?
Wala suala la Muafaka sitaki kilitaja maana kalifanya bila busara sasa linamlipukia kwa Zanzibar kudai Utaifa wao.
Narudia tenza ningekuwa mimi Kikwete, ningempisha mtu mwingine ndani ya CCM agombee, nigeachia Upinzani ushike hatamu, nirudi kwenye maabara kujifunza makosa ya miaka mitano ya kwanza na kisha nitakapokuwa tayari na nimejizatiti na kuamini kuwa sasa nakwenda litumikia Taifa kwa dhati na nitaketa mabadiliko, ndipo ningetumia nafasi yangu kikatiba kugombea kwa mara ya pili hapo mwaka 2030!