Wale wasipamini kuwa kuna mbinu za kuufuta ushahidi wa EPA na kusafishana wasome hii...
Mafisadi EPA wafanya vikao
2008-06-23 12:26:48
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Siku chache baada ya Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Bi. Anne Kilango Malecela, kuwaasa wabunge wenzake kuwa kitu kimoja katika kuwabana mafisadi waliochota fedha za Benki Kuu Tanzania (BoT), kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), kuna taarifa kwamba, watuhumiwa hao wa ufisadi nao kwa upande wao, wamekuwa wakikutana kupanga mikakati ya pamoja ya namna ya kulizima suala hilo, Nipashe imebaini.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika zimeeleza kwamba, mafisadi hao wamekuwa wakikutana mara kwa mara katika moja ya hoteli maarufu mjini hapa ambapo pamoja na mambo mengine, hupanga namna ya kujinasua na kadhia hiyo.
Kwa mujibu wa habari hizo, mafisadi hao wamekuwa wakionekana nyakati za usiku baada ya vikao vya Bunge katika hoteli hiyo ili kujadili masuala mbalimbali lakini kubwa likiwa ni suala la wao kuhusishwa na tuhuma za kuchota Sh. bilioni 133 za EPA pamoja na kashfa ya zabuni ya kampuni ya Richmond.
``Mara kwa mara wamekuwa wakikutana katika hoteli hiyo, kwa ujumla huonekana wakijadili masuala mazito mno, bila shaka ni la wao kuhusishwa na ufisadi,`` kilibainisha chanzo hicho ambacho pia hupendelea kufika katika hoteli hiyo ya kifahari kwa lengo la kujipatia chakula na vinywaji.
Chanzo hicho kilifafanua kuwa, kuhusishwa kwao na kuzungumzia sakata la ufisadi, kunatokana na ukweli kwamba, vigogo hao ni miongoni mwa watuhumiwa wakubwa wa suala hilo.
``Hapana shaka kwamba vigogo hao hujadiliana suala la ufisadi kwani ni miongoni mwa watuhumiwa wa sakata hilo na hupenda kukutana wao tu na kila anayewaona, kwa kweli huwatilia mashaka wanachokijadili,`` chanzo hicho kilizidi kueleza.
Wiki iliyopita wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2008/09 kama ilivyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo, Mbunge wa Same Mashariki, Bi. Kilango alitoa wito kwa wabunge wenzake kutokuwa waoga katika kuwakemea mafisadi wanaotuhumiwa kuchota fedha za EPA.
Mbunge huyo machachari, alisema yeye binafsi yuko tayari kufa akitetea ukweli na haki na kujifananisha na mwanafalsafa wa Kigiriki, Socrates ambaye alisema pia alipoteza maisha kutokana na kusimamia ukweli na haki.
Siku iliyofuata, Mbunge wa CCM (Viti Maalum), Bi. Anna Abdallah kwa kile kilichotafsiriwa na baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa, kuwa ni kujibu kauli ya mbunge mwenzake, alisema kimsingi hakuna mbunge yeyote anayeogopa kulijadili suala hilo.
Bi. Abdallah alisema kila mbunge yuko tayari kupigia kelele uovu huo isipokuwa wanachotofautiana na namna ya kuwasilisha ujumbe huo ndani ya Bunge.
``Baadhi ya wengine wanalisema kwa madoido lakini wengine tunalisema kwa upole, lakini lengo letu sote ni moja na hakuna anayeogopa,`` alisema.
Lakini, akihitimisha mjadala wa wabunge kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya serikali, Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mkulo alisema fedha za EPA hazikuwa za serikali wala BoT bali zilikuwa za wafanyabiashara mbalimbali.
Bw. Mkulo alisema hata hivyo, wafanyabiashara hao kwa sasa ama wamekufa au wako nje ya nchi.
Kauli hiyo ya Waziri, ilionekana kuwashtua baadhi ya wabunge hasa wa kambi ya upinzani ambao pia imedaiwa kwamba, wanajipanga kikamilifu kulizungumzia suala hilo bungeni kwa mapana zaidi katika hotuba ya Waziri Mkuu inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo.
Kikao cha Bunge la Bajeti kinaendelea tena leo mjini hapa baada ya mapumziko ya mwishoni mwa wiki.
Baada ya wabunge kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2008/09 Ijumaa iliyopita, leo asubuhi, kitaanza kipindi cha maswali na majibu na baadaye kufuatiwa na hotuba ya Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake na zilizo chini yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2008/09.
Kama ilivyokuwa kwa hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi, pia hotuba ya Waziri Mkuu itajadiliwa kwa siku tano kuanzia leo hadi Ijumaa ijayo.
Wakati huo huo, Simon Mhina anaripoti kuwa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amedai kwamba kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge, wanajiandaa kutaja hadharani majina ya mafisadi waliochota fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).
Alidai kuwa wengi wao ni vigogo wanaokiunga mkono Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe mwishoni mwa wiki iliyopita, mwanasiasa huyo alisema wanachosubiri sasa ni kuipa serikali muda wa kuweka bayana watu wanaodaiwa kurejesha fedha hizo.
Hata hivyo, Mchungaji Mtikila alidai kwamba hakuna mtu yeyote aliyerejesha fedha hizo, kama serikali inavyotangaza.
``Hakuna fedha yoyote ya EPA ambayo imesharudishwa, maneno ya Waziri wa Fedha na Uchumi kwamba watu wanarejesha fedha, ilikuwa ni aina nyingine ya ufisadi wenye lengo la kuwalinda,`` alidai.
Alizidi kudai kwamba kwa mujibu wa orodha aliyonayo ya waliochota fedha za EPA kinara wao wamemgundua kuwa ana hati mbili za kusafiria.
Alisema fisadi huyo ambaye ni miongoni mwa vigogo matajiri wanaoisaidia CCM, licha ya kumiliki hati ya kusafiria inayomuonyesha kwamba ni Mtanzania, lakini anayo nyingine inayomtambulisha kwamba yeye ni raia wa Iran.
Alisema kigogo huyo mwenye asili ya Kiasia licha ya kwamba anajitapa kuwa ni Mtanzania, lakini wazazi wake wote wawili, hadi sasa wanaishi Iran.
``Ngoja tuangalie kwamba kwa siku mbili hizi serikali itasemaje, vinginevyo sisi tumejiandaa kutaja hadharani majina yote ya wahusika wa EPA, hakuna atakayesitirika wala wasijidanganye,`` alidai Mchungaji Mtikila.
Mwanasiasa huyo alisema moto aliouwasha Mbunge wa Same Mashariki, Bi. Anne Kilango Malecela, hauwezi kuzimika kwa hoja nyepesi za vigogo wa CCM ama kwa vitisho vya wabunge wenzake.
Mchungaji Mtikila alisema kauli za Bw. Mkulo kwamba fedha za EPA sio za serikali na kwamba wanajiuliza kuwa watazifanyia nini, inasikitisha na inalenga kuwatetea waliozipora.
Tuma Maoni Yako