Chief Mrisho
New Member
- Jul 27, 2022
- 1
- 1
Hakuna maisha kamili pasi na sheria za kuyaongoza, sheria za Mungu waamini tunamini kuwa zimekamilika lakini nijiulize mimi na wewe je sheria wanazoandaa wanaadamu zitakuwa na ukamilifu milelee? Naomba utunze swali hilo utanijibu wakati ukifika.
Hayati Rais Julius Kambarage Nyerere akihutubia wananchi. PICHA NA UHURU MEDIA GROUP
Naomba mimi na wewe tuitazame kidogo karne ya 20 kwa shujaa wa Kiafrika Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa jijini Dododma mwaka 1995 alinena machache yenye faidha milele..
“Watanzania wanataka mabadiliko, wakiyakosa ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM”
kuanzia hapa nikuombe uungane nami katika Makala haya yakimulika kwa undani Jicho la Mtawala na mtawaliwa ndani ya Katiba Mpya.
Dhana Ya Katiba.
Katiba ndiyo sheria kuu ama sheria mama kwenye taifa lolote ulimwenguni, Tanzania imeendelea kutumia katiba ya mwaka 1977 ikiwa ni mabadiliko ya katiba tano zilizopita yaani ya katiba ya uhuru mwaka 1961, kisha 1962, 1964, 1965 na hatimae katiba ya mwaka 1977 ikawa ni katiba ya kudumu ikipitia marekebisho 14 hadi sasa.
Chimbuko La Katiba Mpya.
Vuguvugu la Mchakato wa katiba mpya limeanza tangu mwaka 2010 wakati wa Rais Jakaya Kiwete.
Jambo likapamba joto zaidi mwaka wa 2011 baada ya kutungwa kwa sharia ya mabadiliko ya Katiba Na.83/2011, ambayo ilitaka kuanzishwa kwa Tume ya mabadiliko ya Katiba ambayo ilianzishwa chini ya Waziri mkuu wa zamani Jaji Joseph Warioba, kisha sheria nyingine ya kura ya maoni Na.11/2013 ikaundwa.
Waziri mkuu wa zamani Jaji Joseph Warioba akishika nakala ya Rasimu ya Katiba.
Tume hii ilifanya kazi kubwa kukusanya maoni ya wananchi kisha kuunda rasimu ya kwanza ya katiba iliyohaririwa vyema na Mabaraza ya Katiba hatimaye ikaundwa Rasimu ya Pili ya katiba maarufu kama Rasimu ya Warioba ambayo iliwasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Bunge hili liliongozwa na Mwenyekiti Samwel Sitta huku makamu wake akiwa Samia Suluhu Hassan ambaye hivi sasa ndiye Rais wa Tanzania.
Kutokana na mivutano mbalimbali Mwaka 2014 mchakato huu ukakosa tija na hatimaye pamekuwa na mkwamo usiopatiwa ufumbuzi mpaka wakati huu.
Je Baadhi Ya Watanzania Wanatazamaje Suala la Katiba Mpya?
Ni wazi kusema kuwa baadhi ya Watanzania hawana uelewa kabisa na katiba mpya na pengine miongoni mwa hao huisi jambo la katiba mpya ni ajenda itakayoleta vurugu, chuki na hatimaye kuingiza taifa kwenye myororo wa machafuko ya kisiasa.
Lakini pia wapo wenye uelewa na suala la katiba mpya. Nikizungumza na Gabriel Mgata Mkazi wa kata ya luchelele, Wilayani Nyamagana Jijini Mwanza akianza kwa kusitasita kueleza, anafumbua kinywa chake na kunijuza..
"Katiba mpya inaumuhimu tu!.." hakuhitaji kunieleza mengi zaidi ya hapo.
Mkazi mwingine Christina Laithon, akiwa na uso ulio na tabasamu linaloashiria hana hakika na jibu analonipa ananieleza kuwa "Katiba mpya itafanya nchi kuwa na mabadiliko, mimi naamini hivyo..." naye pia hakuhitaji kueleza mengi.
Nikichagua Mwanza kuwa eneo langu la utafiti wa awali , Nakutana na Mkazi mwingine Andrew John Nkii ambaye amenieleza kuwa Tanzania imefikia wakati wa kupata katiba mpya, ili kusukuma maendeleo ya kisiasa japo upande wake hafahamu kwanini viongozi hawajalipa kipaumbele jambo hilo.
" kama kweli katiba ndiyo inatuongoza, nadhani kuna kipengele kimeelekeza mabadiliko na sijui kwanini viongozi hawazingatii hili, hili ni kwa mabadiliko yetu na kuimarisha siasa za nchi yetu..." Nkii.
Video ya mwanamuziki Vitali Maembe ikizungumzia Katiba Mpya.
Mwisho nikakunjua shingo yangu kuangaza kwa wadau wengineo , nikidurusu nakala ya Policy forum nakutana na haya niliyohitaji kukutanabaisha, naomba nawe uyadurusu kisha msomaji wangu nakuomba uendelee kusalia nami.
Kwanini Vuguvugu la Katiba Mpya Linazidi Kupamba Moto nchini Tanzania?
Katiba inayoongoza Tanzania kwa sasa ni ilee ya mwaka 1977 wakati huo nchi ilikuwa ndani ya mfumo imara wa chama kimoja, lakini hivi sasa Taifa limo ndani ya mfumo wa vyama vingi.
Hivyo kuna mitazamo mipya, changamoto mpya, na utendaji mpya wa kisiasa, pia katiba huundwa na wananchi na si Mungu, hivyo binadamu si mkamilifu. Adha, kero, na mahitaji yaliyokuwepo mwaka 1997 ni tofauti na haya ya miaka ya 2020's
Video ya Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu akizungumzia rasimu ya katiba.
Jicho La Mtawala Ndani Ya Katiba Mpya.
Mwaka 2010 Wakati wa uongozi wa Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho kikwete katiba mpya nipo imeanza kuzungumziwa, Watanzania wakaahidiwa kupewa katiba itakayowafanya wafike mbali kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Jicho la kikwete lilidaiwa kuona mazuri ya katiba mpya kwanza na ndiyo maana alionesha nia juu ya ujio wa katiba hiyo ijapokuwa hakukamilisha hilo.
Awamu ya tano ndani ya Uongozi wa Hayati Rais John Magufuli jicho lake halikutazama zaidi juu ya kuleta katiba mpya nchini badala yake alihitaji kujikita na maendeleo ya nchi ili kuifanya Tanzania iwe na uchumi imara.
Mbali na Mema mengi aliyoyafanya lakini pia Mengi yamezungumzwa wakati wa uongozi wake, ikiwa ni pamoja na kuongoza kimabavu, kufinya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza sambamba na kupunguza ari ya siasa za kambi pinzani, hatimaye Wananchi wakaiona haja ya katiba mpya.
Katiba inayopiganiwa ikatoa mwanga kwa Samia Suluhu Hassan kutoka kwenye Umakamu wa Urais hadi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni mara baada ya kufariki kwa Rais Magufuli mnamo Mwezi Machi, 2021.
Nikijijita kumulika katib mpya, Rais Samia akihusishwa na Lugha nyepesi iliyopambwa na hekima ya kimatamshi sambamba na sifa za kuiishi demokrasia, Watanzania wameketi mkao wa kusubiri mabadiliko kikatiba ili kuziba kila ufa utakaoweza kubomoa nyumba yao kisiasa, kichumi na kijamii. Lakini bado mustakabali chanya haujapatikana katika hili..
Jicho la Rais Samia bado halijaonesha njia sahihi kwa Watanzania ili waifuate kupata katiba mpya, badala yake wameendelea kuaswa kusubiri ili mengine ya msingi yafanyike kwa ajili ya Taifa.
Nirejee kwako Msomaji wangu nakuomba unipe maoni yako kuhusu hili...
Je Unafikiri Katiba Mpya italeta mabadiliko gani nchini Tanzania..?
Naomba unijuze mengi lakini usisahau hilo.
Nikuombe usisahau kunipigiia kura yako, ili niwe miongoni mwa watakaoshinda tuzo hizi, zinazokwenda kubadilisha fikra za jamii zetu kuelekea mrengo chanya zaidi.
Ahsante kwa muda wako.
VYANZO.
Dw, BBC SWAHILI, LHRC, POLICY FORUM,ONLINE TUITION BLOGSPORT, KAHOLA TZ BLOGSPORT UHURU MEDIA GROUP, MASOUD KIPANYA.VOA, IKULU MAWASILIANO.
Attachments
-
Screenshot_20220727-225230_Google.jpg29.8 KB · Views: 6 -
Tundu_Lissu_alivyo_fyatuka_Bunge_la_Katiba(360p).mp418 MB
-
Screenshot_20220801-012843_Chrome.jpg14.6 KB · Views: 5 -
MAJIBU_ya_RAIS_SAMIA_Kuhusu_KATIBA_MPYA_na_MIKUTANO_ya_KISIASA___NIPENI_MUDA_NIJENGE_NCHI_KIUC...mp416.3 MB
-
Screenshot_20220801-015759_Chrome.jpg15.5 KB · Views: 6 -
Screenshot_20220727-223147_Chrome.jpg133.8 KB · Views: 6 -
Screenshot_20220727-223746_Google.jpg29.3 KB · Views: 7
Upvote
1