STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 50
SONGA NAYO............
Laurian Cosmas alikuwa amechanganyikiwa ndani ya kituo hicho cha runinga akiwa anaonekana kwenye matangazo ya moja kwa moja. Kauli yake ya kudai kwamba anataka kuuawa iliwatia wasiwasi wote ambao walikuwa humo ndani japo wengine walihisi kwamba huenda mtu huyo alikuwa ana matatizo ya akili. Kilicho washtua sana ni baada ya kutamka kwamba alikuwa anaomba msamaha kwa kuchukua mali za ndugu yake kwa nguvu na kudai kwamba alikuwa tayari kuzirudisha muda wowote ule kuanzia wakati huo kwani kama asingefanya hivyo basi kuna mtu ambaye alikuwa anayahitaji maisha yake kwa nguvu kubwa sana.
Miguu yake yote ilikuwa butu baada ya kutolewa vidole vyote ambavyo vilikuwepo hapo lakini hata nguo zake hazikueleweka ni kwa namna gani zilikuwa zimechakazwa namna hiyo, mwanamke mmoja alimmwagia maji ya baridi na kumtuliza kisha akamsogelea pale alipo na kumuuliza kistaarabu sana.
“Kimekukuta nini?” alimuuliza huku akiwa kama anamkanda kanda kwenye mwili wake, kitu ambacho kilimfanya aheme kwa nguvu sana. Baada ya hapo aliangaza huku na huku kama labda ataona mtu ambaye alihisi kwamba alikuwa anamfukuza. Baada ya akili yake kukaa sawa aliweka sauti yake vyema ikiwa inatoka kwa maumivu makali ambayo yalikuwa yamechanganyikana na ubaridi wa maji ambayo alikuwa amemwagiwa. Maumivu hayo yalikuwa yamesababishwa na ule mkato ambao alikuwa ameupata kwenye vidole vya miguuni kwake.
“Miaka kadhaa ambayo ilipita nyuma kidogo nilikuwa na ndugu yangu ambaye alinisaidia sana tena sana na sio mimi tu bali ndugu wote ambao tulikuwa tunamzunguka, kila ambaye angehitaji msaada wake alijitolea kwa kila kitu na tulipewa kila kitu kulingana na mahitaji yetu wenyewe. Mimi ni miongoni mwa watu ambao walisaidiwa sana na huyo ndugu yangu, ilifika wakati nilienda kabisa kukaa kwake japo moyoni mwangu nilikuwa nina mipango yangu tayari”
“Kufika kwake alinisaidia kana kwamba tulikuwa ndugu wa tumbo moja kabisa kumbe ni baba zetu ndio walikuwa ndugu. Kwa muda ambao nilikuwa nimekaa pale kwake mipango yangu ilikuwa ni kuyasoma mazingira niweze kuzichukua mali zile kwenye himaya yake na kuziweka kwenye himaya yangu na hilo nililifanikisha kwa asilimia miamoja”
“Nilimuwekea mkewe sumu ili afe baada ya kujua nyaraka za mali zilipo maana alibaki yeye tu nyumbani na hiyo niliotaka kuitumia kama nafasi ya pekee kufanya hivyo japo kwa bahati aliishi tena. Niliondoka na kila kitu kisha nikawatafuta ndugu zangu wengine watatu ili tusaidiane kumshtaki na kumpoteza kabisa kwenye dunia yetu tumuache akiwa kapuku wa kutupwa. Hilo tulilifanikisha baada ya kumnunua mwanasheria na maaskari na kweli tukafanikiwa hilo ambapo aliishia kupata ukichaa na kutoweka na familia yake ambayo mpaka sasa hivi sijui iko wapi” alielezea kwa kifupi lakini ilitosha kueleweka kwamba alikuwa anamaanisha kitu gani. Kila ambaye alikuwa humo ndani alikuwa anamshangaa mwanaume huyo kwa namna alivyokuwa na roho ngumu mithili ya paka yaani mtu ambaye alikubali kufanya kila kitu kwa ajili yako na bado unawaza kumfanyia malipo ya ubaya wa namna hiyo? Dunia haikuwa sawa.
“Sasa imekuwaje mpaka useme kwamba kuna mtu anakuua? Na hiyo hali imekufikaje wewe?” mwanamama huyo ambaye alikuwa karibu yake aliendelea kumshawishi huku akiwa anamkanda kanda. Hapo kwake kulikuwa na mambo makuu mawili, jambo la kwanza yeye angeonekana kama ni mtu bora sana kuweza kumtuliza mtu kama huyo ambaye alikuwa kwenye taharuki kubwa na akafanikiwa kuongea ukweli. Lakini jambo la pili yalikuwa ni mambo mawili ambayo yangeunganishwa na kuwa jambo moja. Kwanza chombo chao cha habari kilikuwa kinaenda kupata jina kubwa na kuendelea kwenda mbali zaidi kwa kupata kisa cha kusisimua kama hicho lakini pia kwenye kila sehemu ambayo tukio hilo lingeonyeshwa moja kwa moja naye angehusishwa kwani yeye ndiye ambaye alikuwa akimhoji mwanaume huyo.
Laurien Cosmas alimtazama mwanamke huyo huku akiwa anatikisa kichwa chake kwa masikitiko sana.
“Naomba maji ya kunywa” aliongea kwa sauti ya mkwaruzo kwaruzo, sauti yake ilikuwa inamkauka kwa nguvu sana kwa muda mwingi ambao ulikuwa unaendelea kumpatia wasiwasi kubwa sana kwenye nafsi yake kwa ujumla. Alikunywa maji yote kwenye kikombe ambacho alipatiwa, akaivuta hewa kwa nguvu sana na kutoka hapo chini alipokuwa amekaa na Kwenda kukaa kwenye sofa, akili ilikuwa imemkaa vyema sasa na presha ilimshuka kabisa kwenye nafsi yake.
“Kwa majina wengi wananijua kama Laurien Cosmas, ila mimi naitwa Laurien Hashim na hili ndilo jina ambalo mimi nilipewa na wazazi wangu, hili ni jina la ukoo wetu ambalo alikuwa analitumia hata kaka yangu. Nilibadili hili jina baada ya kuzipata zile mali ili nisije nikapata usumbufu kutoka kwa mtu yeyote yule nikaamua kujipachika jina la Cosmas ambapo ukinitaja mahala popote pale basi watu wengi sana watakwambia kwamba mimi ni miongoni mwa matajiri wakubwa sana ndani ya hili jiji na nchi kwa ujumla. Hayo mambo siyo uzushi ni ukweli kabisa lakini katika zile mali basi mali zangu sina hata moja zote ni mali halali za kaka yangu” alimeza mate na kuendelea.
“Baada ya kuzipata mali kwakweli maisha yangu yalibadilika sana maana hata wale ndugu zangu ambao niliwashirikisha kwenye zile mali niliwakataa baadae na kuwatishia kuwaua kama wangeenda kunichafua sehemu yoyote ile, kama unavyojua ikiwepo pesa mahali basi asiyekuwa nayo huwa anakuwa mnyonge na mtumwa na ndivyo ilivyokuwa kwa hao ndugu zangu niliishia kuwapatia pesa za mboga tu huku mimi nikiitawala dunia na wanawake”
“Hakuna mwanamke mzuri kwenye jiji hili ambaye anajulikana mimi sijalala naye, hakuna mwanamke mzuri ambaye alikuwa na uwezo wa kunikataa, kwa sababu nilikuwa na vyangu, nilikuwa naweza Kwenda mahala popote pale ambapo ningetaka Kwenda basi hilo lilimtamanisha kila mwanamke akijikuta ana ndoto za kulala namimi hata kwa usiku mmoja tu kwa lengo kubwa la kujichumia mali na mimi sikulaza damu niliwanyoosha sana”
“Ila maisha yangu ya starehe na raha kubwa sana yameishia usiku huu wa leo ambao umenifanya mpaka mimi nimekuja kuomba msaada hapa baada ya kuona naweza kuishia kufa vibaya sana kama nikienda kinyume na matakwa ya mhusika mwenyewe. Majira ya jana nilikuwa hotelini na mwanamke, kwenye simu yangu iliingia meseji ya kunipatia masaa 12 niweze kurudisha mali zote kwa wahusika na kama sina uwezo wa kuwapata basi nilipaswa Kwenda kwenye vyombo vya habari kuwatafuta na kuwaomba msamaha hadharani kwa kile ambacho mimi niliwafanyia ili kama wanaweza kunisamehe basi itakuwa ni wao ila nisilale na zile mali zikiwa ni zangu kwa usiku wa pili yake. Nilipuuzia sana nikijua ni vijana wa mjini ambao huwa wanatumia njia za hii mitandao kwa ajili ya kuwatapeli watu hivyo sikujali nikaendelea na maisha yangu ya kuponda starehe sikujua kwamba kufa kwaja”.
“Leo jioni nilikuwa nipo nyumbani kwangu na walinzi wangu, pembeni yangu nilikuwa na moja ya mwanamke ambaye ni maarufu sana hapa mjini, geti limegongwa kwa fujo sana kitu ambacho kimenifanya kuwa kwenye hasira na kuhitaji moja ya walinzi wangu akafungue na kumpatia adabu yake huyo mjinga ambaye alikuwa anafanya huo ujinga kwenye nyumba za watu ambazo hajui hata thamani ya tofali lake, lakini mambo yamekuwa tofauti sana. kwani baada ya mlinzi yule kufungua tu mlango sikujua kama niliona vizuri au nilikuwa ndotoni, alibamizwa kichwa chake ukutani mpaka kichwa kikapinda” aliacha kwanza kuelezea akainama chini kama anavuta hisia ya kile kitu ambacho alikuwa amekishuhudia kisha tena akainua kichwa chake.
“Nilihisi ni jini lakini baadae nimekuja kujua kwamba ni mtu tu wa kawaida japo usoni kwake alikuwa amejifunika na mask nyeusi na kumfanya kutoonekana kabisa sura yake. Yule mlinzi alikuwa tayari amekufa, nilikuwa na walinzi watano ambao nadhani kwa yule mtu walionekana kama ni wabeba vyuma wasiokuwa na chochote cha kukifanya mbele yake zaidi ya kupoteza muda tu. Walikuwa wamebaki walinzi wanne, wawili walinizunguka na wawili walimfuata pale alipo. Wale watu wameuawa kifo cha kikatili ambacho sijawahi kukiona kwenye maisha yangu, ukiingia ndani ya geti langu kubwa la gari kwa pembeni kuna nondo ambazo zimechomwekwa karibu na bustanini hizo zinazuia uwanja wa kawaida na bustani. Yule mtu amechomoa nondo moja na kuizamisha kwenye shingo ya kijana wangu mmoja ambaye hakuzungumza neno lolote tena, na yule mwenzake alivyo ona ile hali alikuwa anataka kukimbia baada ya kuona ule unyama ambao alikuwa ameushuhudia kule lakini alichelewa baada ya kudakwa shati yake nyuma. Nadhani kile kilikuwa ni kiganja kimepitishwa kwenye shingo yake kwa nyuma, sijajua kimetokea nini ila nadhani kuna mishipa ilipishanishwa.”
“Ile hali imenifanya niogope sana tena sana, yule mwanamke amekimbia na hata wale walinzi wawili waliokuwa wamebaki namimi wamekimbia kwa kuruka mageti kuokoa uhai wao huku nyuma nikibaki mimi mwenyewe kuyatetea maisha yangu” Laurien, aliacha kwanza kuelezea, akaanza kutoa machozi kwenye uso wake, mwili ulikuwa unamsisimka sana kwa kile ambacho alikuwa anaenda kukielezea kwa wakati huo.
“Sijafanikiwa kabisa kumuona sura yake ila nahisi yule sio mwanadamu kama walivyo wengine bali ni jini ambalo linaishi ndani ya ngozi ya mwanadamu. Amefika sehemu ambayo nilikuwa nimekaa, maelekezo ambayo amenipa ni kwamba ameona kwamba kwenye simu hatukuelewana vizuri ndiyo maana sikufanya aliykuwa ameniagiza hivyo amekuja mwenyewe kunipa nafasi ya mwisho Kwenda kufanya hivyo”
“Sidhani kama alikuwa na nia mbaya na mimi kwa wakati ule maana kama ningekubali moja kwa moja nadhani angeniacha salama lakini mdomo wangu umenipoonza kuhisi naweza kumtisha yule mtu nimefeli sana na mdomo ndio ulio nifanya mpaka nikaishia hapa ambapo nipo mpaka wakati huu, nimefanywa kitu ambacho hata mnyama hana uwezo wa kumfanyia mwanadamu, nimetamani ni bora angetokea mtu wa kunipiga hata risasi ili nife, nimetamani nipate nafasi nijiue lakini hiyo nafasi sijapewa kabisa. Nimehangaika sana, nimeteseka sana na hiki ndicho kimenipata, nimetolewa kucha bila ganzi, nimekatwa vidole bila ganzi, baada ya kumaliza ndipo akanichoma sindano za ganzi ili nije huku na kuniacha hai ili nitubu niliyo yafanya pamoja na kurudisha mali za watu” alikuwa anaongea akiwa anatoa machozi kwenye uso wake, wakati anaelezea hayo matukio mwili ulikuwa unamsisimka sana mwanaume, kila akiwaza namna alivyofanywa alihisi kama vile amechanganyikiwa.
"Sasa imekuwaje akakuacha hai na kwanini haukuripoti polisi haraka mtu huyo akamatwe?” kauli ya huyo mwanamke ambaye alikuwa anamuuliza maswali ilimfanya amwangalie sana.
“Leo ndo nimegundua kwamba kwenye maisha ya mwanadamu uhai ndicho kitu bora zaidi kuliko kitu chochote kile, vijana wengi wanasema kwamba pesa ndiyo kila kitu huo ni uongo mkubwa sana, mimi nimeshukuru tu kuachwa hai basi. Swali lako ni la hovyo sana kuniuliza kwamba ni kwanini ameniacha hai, maelezo yake amesema kwamba ameniacha hai kwa sababu mimi sikusababisha kifo chochote kwenye ile familia ila kama kuna mtu angekufa basi muda ule ule na mimi ningeuawa. Sitaki tena maswali naombeni hifadhi hapa hapa sitaondoka mpaka pale ambapo nitakabidhi kila kitu kwenye ile familia” aliongea kwa msisitizo akiwa ananyanyuka kwenye sofa, alihitaji sehemu ya Kwenda kupumzika kwanza.
“Umemwamini vipi kama anayo yasema ni kweli?”
“Acha maswali ya kijinga kwahiyo unahisi mimi kuja kusema nilichukua mali za watu ni mjinga au?” alijibu kwa hasira sana kuonyesha kwamba alikuwa amechoka na hayo maswali.
“Jina lake anaitwa nani?”
“Ametaja alama moja tu kwamba yeye ni T” hilo ndilo lilikuwa jibu la Laurien Cosmas, hiyo T ilikuwa imesimama kwa niaba ya Team Leader kwenye ile Toxic, bila shaka mhusika wa hilo tukio alikuwa ni Jason yeye mwenyewe.
Unahisi ndiyo yale majina ambayo alimhitaji mama yake na Nayrah amwandikie kwa watu walio husika kuchukua mali zao ameanza nayo au kuna mambo ya hovyo tu kayafanya? Bila shaka ni yale majina aliahidi kwamba watarudisha kila kitu mapema sana. Acha niweke kalamu chini kwanza hapa nipate maji kidogo.
50 inafika tamati, panapo majaaliwa tukutane wakati mwingine tena.
Wasalaam
Bux the storyteller.
View attachment 2698818
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app