Tani 216 za mahindi kutoka Tanzania zazuiwa mpakani upande wa Kenya
MONDAY MARCH 08 2021
Meneja wa Forodha Mkoa wa Kilimanjaro, Edwin Lwato
Summary
Magari 12 yenye shehena ya tani 216 za mahindi, yamezuiwa mpaka wa Holili, upande wa Kenya, kusubiri majibu ya vipimo vya sampuli zilizochukuliwa na mamlaka za Kenya.
ADVERTISEMENT
By Florah Temba
More by this Author
Moshi. Magari 12 yenye shehena ya tani 216 za mahindi, yamezuiwa mpaka wa Holili, upande wa Kenya, kusubiri majibu ya vipimo vya sampuli zilizochukuliwa na mamlaka za Kenya.
Akizungumza leo Machi 8, 2021, Meneja wa Forodha Mkoa wa Kilimanjaro, Edwin Iwato amesema mahindi hayo yamezuiwa kuanzia Machi 5, mwaka huu na mpaka sasa bado wanasubiri majibu ya sampuli zilizochukuliwa.
"Katika mpaka wa Holili, kumekuwa na mkwamo wa kibiashara wa mahindi na kuanzia Machi 5 hadi 8, mwaka huu,kuna shehena ya mahindi tani 216, kutoka kwa wakulima wa Tanzania ambayo yamekwama upande wa Kenya, kusubiri taratibu za majibu ya vipimo.
"Sampuli zimechukuliwa kwa ajili ya vipimo kwenye shehena hizo za mahindi tani 216, bado tunasubiri wenzetu wa Kenya wakamilishe utaratibu huo,na ni changamoto ambayo imejitokeza na imeathiri kidogo mzunguko wa biashara hiyo ya mahindi,” aliongeza.
Aidha amsema serikali inaendelea kushughulikia suala hilo ili kuweza kukwamua mkwamo huo na kuwezesha biashara kwa pande zote kuendelea kama kawaida.
Wakizungumza baadhi ya wafanyabiashara wa mahindi katika mpaka wa Holili, wameonyesha kushangazwa na kauli ya Kenya kudai kuwa mahindi yana sumu,wakieleza kuwa wamefanya biashara hiyo zaidi ya miaka 20 bila matatizo.
Ramadhani Bakari, amesema wamekuwa wakishirikiana vizuri na wafanyabiashara wa Kenya na wamefanya biashara ya nafaka kwa muda mrefu bila matatizo lakini leo wanashangaa kusikia mahindi ya Tanzania yana sumu
"Kuna magari yamezuiwa upande wa Kenya lakini ukiangalia pia hapa katika soko la kimataifa la nafaka la Holili, kuna shehena ya mahindi ina wiki, wapo wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini na tunapata hasara kubwa, hatujui kama ni ishu za kisiasa au kuna mgogoro wa chini kwa chini unaendelea,” aliongeza.
"Tunaomba sana serikali hizi mbili, ziweze kukaa kwa pamoja na kuona namna ya kumaliza tatizo hili, maana tumekuwa tukishirikiana vizuri, kwa muda mrefu na hatujawahi kusikia watu hawa wamefariki Kenya au Tanzania kutokana na kula nafaka zenye sumu,” alilalamika Bakari.
Magari 12 yenye shehena ya tani 216 za mahindi, yamezuiwa mpaka wa Holili, upande wa Kenya, kusubiri majibu ya vipimo vya sampuli zilizochukuliwa na mamlaka za Kenya.
www.mwananchi.co.tz