Didask89
New Member
- Jul 14, 2021
- 1
- 1
Na Didas Patrick
Rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela aliwahi kusema, nanukuu, "Elimu ndio silaha pekee na yenye nguvu unayoweza kuitumia kuibadilisha dunia".
Katika historia ya dunia sijapata kushuhudia mtu aliyeaminiwa na kupewa fursa ya kuilea jamii kuanzia utotoni mpaka ukubwani zaidi ya mmoja tu ambaye dhamana ya maisha ya watoto, vijana na hata watu wazima imekabidhiwa kwake. Mtu huyu ambaye jamii ya wazazi na walezi imemwamini kiasi cha kumkabidhi kundi la watoto alilee, ambaye kauli zake, mienendo ya fikra na vitendo vyake imempa heshima na kipaumbele cha kuisaidia jamii katika nyanja anuai anaitwa Mwalimu.
Huyu ni mtekelezaji mkuu wa mchakato mzima wa elimu. Ni mpiga makasia katika jahazi la elimu na ndiye taswira halisi ya elimu.
Solomon Ortiz, mwanasiasa mkongwe wa Marekani aliwahi kusema msemo ambao ni maarufu mpaka leo, nanukuu, "Elimu ni ufunguo wa kufaulu maishani, na waalimu ndio wasababishi wa mabadiliko yasiyo na mwisho katika maisha ya wanafunzi wao".
Nukuu hii imekuwa ikisemwa kwa kifupi, 'Elimu ni ufunguo wa maisha' na imekuwa maarufu mitaani na katika taasisi mbalimbali za elimu ndani ya nchi yetu japo nasikitika kusema, kwamba watu wengi wamekuwa wakiutumia msemo huu tofauti na maana halisi ya msemo wenyewe.
Elimu ya kweli huonekana pale ambapo ujuzi uliopatikana unatumika katika kutatua changamoto za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Ujuzi ukibaki kwenye vichwa vya watu bila kutumika popote itakuwa sawa na kunoa shoka na kuliweka ndani huku kukiwa na mti mkubwa unaotakiwa kuangushwa kwa shoka hilo.
Lakini pia matumizi mabaya ya elimu huonekana pale inaposhindwa kutatua changamoto za kijamii ambapo si tofauti na kisu butu kisicho na makali tunachotaka kukitumia kukata nyama inayotarajiwa kuliwa na halaiki ya watu. Loh! Nani anayependa kutumia kisu butu kungali na nyama nzuri inayosubiri kisu kikali?
Changamoto tulizo nazo karne ya 21 zinahitaji mabadiliko makubwa sana katika mfumo wa elimu na matumizi yake. Zinahitaji jamii yenye maono makubwa na mtazamo chanya.
Mfumo wa sasa wa elimu una mapungufu gani?
Siku moja katika shughuli zangu za ufundishaji niliwapa wanafunzi mtihani. Nilipomaliza kusahihisha nilisoma matokeo mbele ya wanafunzi na kumgawia kila mmoja karatasi yake ya matokeo. Mwanafunzi mmoja ambaye kila mara alikuwa akifanya vizuri darasani alishtuka kuona mabadiliko katika matokeo yake. Alama alizopata zilikuwa za chini mno kuliko alizozoea kupata. Basi alipofika nyumbani, baba yake alimwomba karatasi ya matokeo na alipoona alama si zile alizotarajia alikasirika na kumpa adhabu kali ya viboko.
Nilisikitika, si kwa sababu mwanafunzi yule alipata alama za chini, ila niligundua mfumo wa elimu tulio nao - haukidhi mahitaji ya kielimu tuliyo nayo.
Wazazi wanapompeleka mtoto shuleni, humwambia, 'Kazana kusoma uwe wa kwanza usipitwe na fulani'. Kumfundisha mwanafunzi kuwa wa kwanza si jambo baya sana lakini kwa upande mwingine ni kumfundisha kutoshirikiana na wenzake, na kuona hakuna anayestahili kuwa wa kwanza isipokuwa yeye. Humfanya ajione bora kuliko wenzake. Mtazamo huo utamfanya awapuuze wenzake na kuficha kila kizuri alicho nacho ili afaidi peke yake.
Je, tunategemea nini kwa mwanafunzi huyu pindi atakapomaliza shule na kuishi na wenzake mtaani? Kama ni mtu tuliyetarajia aisaidie jamii kutatua changamoto mbalimbali, je ataweza vipi kushirikiana na wenzake il hali hakufundishwa namna sahihi ya kushirikiana na wenzake?
Dosari nyingine ninayoona ni kipimo cha uwezo na uelewa wa mwanafunzi.
Katika mfumo wa elimu tulio nao kipimo cha uwezo na uelewa wa mwanafunzi ni kimoja tu - Mtihani.
Darasa moja huwa na wanafunzi wengi ambao kwa asilimia kubwa ni wa jinsia tofauti, wenye tabia na mienendo tofauti, uwezo tofauti wa kufikiri na kutenda lakini pia vipawa tofauti. Kipimo kinachotumika kuwapima wanafunzi hawa ni kimoja tu - Mtihani, tena wa aina moja.
Je, ni kitu kinachowezekana tukiwaweka pamoja tembo, samaki, chui na nyoka halafu tukawataka waukwee mbuyu? La hasha! Ni jambo la kushangaza na lisilowezekana kabisa. Nafikiri si sahihi kimantiki kumuuliza mwanafunzi ndoto yake ni ipi akasema anataka kuwa rubani halafu tukampa adhabu kwa sababu tu ameshindwa kuandika neno 'Cytoplasm'.
Aina za mitihani tunazowapa wanafunzi wetu si sahihi tukizingatia utofauti unaoonekana katika uwezo na vipawa vyao.
Kipimo cha mtihani wa aina moja hakimfanyi mwanafunzi kutumia kipawa chake wala kuonesha uwezo wake na kumwongezea uwezo wa kufikiri, bali kwa kiasi fulani humwongezea uoga wa kushindwa na kupokea adhabu kutoka kwa waalimu na wazazi wake.
Mwanafunzi hapaswi kuchaguliwa nini cha kufikiri. Cha kufikiri tayari anacho (yani kipawa chake na uwezo wake). Anachostahili kufundishwa ni jinsi ya kufikiri sawasawa.
Kasoro nyingine ambayo nisingependa kuwa kimya dhidi yake ni mtazamo hasi katika kushindwa.
Katika maisha, kushindwa ni sehemu ya kufanikiwa. Watu wengi hutafsiri kushindwa kama kinyume cha kufanikiwa. Hii si sawa.
Kushindwa humpa mtu uzoefu, na fursa ya kujaribu tena na tena, humfunza kujitathmini na kuangalia ni wapi alikosea ili asikosee tena. Kushindwa ni kipimo cha uwezo na ujasiri katika kujaribu mambo mbalimbali.
Katika mfumo wa elimu tulio nao, kushindwa huonekana kama kitu kibaya na huambatana na adhabu kali. Mtazamo hasi katika kushindwa umewafanya watoto na vijana wengi wajenge hisia ya kutojiamini na hivyo kushindwa kutumia vema vipawa walivyo navyo.
Nakumbuka nilipokuwa kidato cha pili niliwekeza juhudi kubwa sana katika somo la muziki. Nilifanya bidii kiasi kwamba siku ilikuwa haipiti bila kufanya mazoezi ya muziki. Rafiki yangu mmoja aliona juhudi yangu lakini akaniambia, "angalia usiwekeze muda mwingi kwenye muziki, utafeli masomo mengine"
Sikumsikiliza, niliendelea kujifunza zaidi na zaidi na sikushindwa masomo mengine kama alivyotarajia. Leo somo la muziki limenifanya kupata fursa nyingi ambazo ni tofauti na masomo mengine niliyosoma shuleni, pia muziki umenikutanisha na watu wengi ambao wamenifanya kujenga jina na kufungua milango ya fursa zaidi.
Najiuliza, ingekuwaje kama ningesikiliza maneno ya rafiki yangu? Hizi fursa za kufanya kazi za muziki ningezipata wapi?
Katika miaka hii kuna kundi kubwa la vijana waliohitimu elimu ya juu lakini maisha wanayoyakuta mtaani ni tofauti na yale waliyoishi shuleni na vyuoni. Wakiwa shuleni na vyuoni hawakufundishwa stadi mbalimbali zitakazowapa ujasiri wa kupambana na changamoto ya ajira. Kutokana na woga wa kushindwa, vijana wengi wanashindwa kuanza biashara ndogo ndogo, wanashindwa kufanya kazi zinazosemekana ni za watu wasiokwenda shule.
Yote hayo yakitokana na uoga wa kushindwa waliofundishwa tangu wakiwa shuleni. Wengi hujiuliza 'Hivi ndugu zangu na marafiki zangu watanionaje nikiwa nafanya kazi fulani?' Au 'Hivi nikishindwa kufanikiwa kwenye biashara hii si nitachekwa hata na wale niliosoma nao!'
Ni muhimu kujiuliza, ni kizazi cha aina gani tunachokiandaa kwa kutumia mfumo wa elimu tulio nao nchini mwetu.
Nini kifanyike?
Waswahili husema, 'Samaki mkunje angali mbichi'. Ushauri wangu upo zaidi katika marekebisho ya mfumo wa elimu kuanzia ngazi ya chini.
Ushauri wa kwanza ninaopenda serikali iufanyie kazi haraka ni kubadilisha mfumo wa ajira za waalimu. Waalimu wanaoajiriwa sasa hupewa jukumu la kufundisha masomo yote hata yale wasiyo na uwezo nayo. Hii si sawa kwa sababu umahiri katika ufundishaji hutegemea sana uwezo wa mwalimu katika somo husika.
Nitapenda sana pia kama serikali itaanza kuajiri waalimu mahiri wa teknolojia mbalimbali zinazoendana na wakati tulio nao, waalimu wa stadi mbalimbali, mfano, waalimu wa upishi, walimu wa sanaa na michezo n.k kuanzia ngazi ya shule za msingi ili stadi za maisha zianze kufanyiwa kazi tangu utotoni. Mtoto akiwa na kipaji cha uchoraji akabidhiwe kwa mwalimu wa uchoraji na vipaji vingine kadhalika.
Ushauri wa pili ni kurekebisha dhana ya mashindano katika mchakato wa ujifunzaji. Mtoto asifundishwe kushindana dhidi ya wengine, bali mtoto afundishwe kushindana dhidi yake mwenyewe. Mfano, mwezi uliopita alipata alama 60%, kwa hiyo mwezi huu asaidiwe apate alama kubwa zaidi ya hiyo na sio kushindanishwa na waliopata alama kubwa kuliko yeye. Hii iambatane na nasaha kwa watoto ili kuwaongezea mtazamo chanya kwamba wanaweza kuwa bora kuliko jana.
Ushauri mwingine ninaopenda ufanyiwe kazi ni elimu iwe ya vitendo zaidi kuliko nadharia.
Mabadiliko chanya katika maisha huletwa na vitendo sahihi. Elimu yetu ikiwa nadharia kwa 25% na vitendo kwa 75% italeta matokeo chanya katika maisha ya vijana baada ya masomo.
Nahitimisha kwa kusema, taifa letu linahitaji watu makini, wenye maono na fikra chanya kuhusu elimu. Ni ngumu kuibadilisha dunia kama hatutakuwa na kizazi chenye kukubali mabadiliko katika mfumo wetu wa elimu.
Mungu awabariki nyote na awafanikishe katika majukumu ya kulijenga taifa letu.

Upvote
1