Ama kweli pombe si chai, kauli hiyo ilijithibitisha mwishoni mwa wiki iliyopita pale msanii wa filamu anayevuma Bongo, Elizabeth Michael Lulu alipopelekeshwa na kilaji kwa kulewa tilalila kiasi cha kuwa kero kwa wazungu aliokaa nao sanjari.
Tukio hilo lililoshuhudiwa na Risasi Mchanganyiko lilijiri Desemba 17, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ambako shindano la kumsaka Msanii Mwenye Kipaji, (Bongo Star Search) lilikuwa likifanyika.
Msanii huyo mdogo kiumri, alitinga ukumbini humo akionekana mwenye busara zake na hajalewa na kuketi sambamba na watasha hao.
Alianza kupiga nao stori huku akiwa ameshahudumiwa kilauri ambapo alikuwa akinywa taratibu huku akiendelea kubadilishana mawazo na majirani zake hao.
Lakini kadiri muda ulivyosonga mbele, ndivyo utulivu wa staa huyo ulivyoanza kutoweka na kufikia ziro kwani alianza vituko ambavyo bila shaka majirani zake walimshangaa.
Baada ya muda, Lulu ambaye amekuwa akisemekana anapenda kulewa aliwehuka hasa pale ambapo kila mshiriki wa BSS alipopanda jukwaani, yeye alishangilia kwa kusimama akinyoosha mikono juu, wakati mwingine akiruka na kuiacha sakafu kwa futi moja achilia mbali kinguo alichovaa kuonesha sehemu kubwa ya mapaja yake.
Msanii huyo alizidi kufanya vituko kiasi cha kuwapa kibarua kizito wazungu hao kumtuliza mzuka huku wakiendelea kumshangaa na kutaka kujua hasa anamshabikia nani kati ya washiriki wa shindano hilo.
Baadhi ya wadau walisikika wakiwalalamikia wauza pombe ambao wanakubali kumpa huduma hiyo msanii huyo mtoto kiumri.
Lakini na hao wauzaji nao jamani, sasa mtoto kama huyu wanamuuziaje pombe, si ana miaka kumi na saba huyu? Walihoji wadau hao.
Hadi shughuli hiyo inamalizika, Lulu alikuwa amegida ulabu vilivyo ambapo aliungana na wahudhuriaji wengine na kutimka eneo hilo.
Siyo mara ya kwanza kwa Lulu kulewa chakari hadi kuzima gari, hivi karibuni aliripotiwa na gazeti hili kukutwa na tukio kama hilo akiwa ndani ya Club Bilicanas Posta jijini Dar.