Nadhani uko sahihi kuuliza, japo JF au Google isichukue nafasi ya kwenda hospitali. Kuna vitu ambavyo ni rahisi ku google, kama side effects za dawa, lakini sio kutaka kujua waumwa nini. Hiyo ni kazi ya daktari ambayo aghalabu kasomea angalau miaka mitano na kuendelea. Si kwamba nasema huruhusiwi ku google, ila naogopa usije ukaanza kutibu dalili (kama maduka ya dawa mengi yafanyavyo hapa Tanzania) wakati kuna vitu vingi ambavyo daktari akiviunganisha pamoja hufikia kutambua tatizo ama ugonjwa.
Mimi sio daktari bingwa wa watoto, lakini kitu cha kwanza ambacho mzazi anatakiwa kukijua je, maji anayosema anakunywa mengi ni kiasi gani? Litre 2, litre 3, litre 1? Maana waweza ukasema anakunywa maji mengi wakati ni kiasi sawa kwa umri kama huo. Hivyo kabla hatujasema anakunywa maji mengi lazima tujue kiasi anachokunywa.
Lakini pili kunywa maji mengi kunaweza kukawa ni dalili ya kuwa na kiu kubwa (kwenye magonjwa kama Diabetes Insipidus, Diabetes Mellitus n.k) au ni tatizo la kisaikologia (kama Stress, Anxiety, n.k na pia kama dalili za mwanzo za autism). Hivyo utaona dalili ya kunywa maji mengi yenyewe haiwezi ikakupa jibu la tatizo, ila labda kutakuwa na dalili muambata ambazo zitakusaidia kujua kama kuna tatizo fulani kama vile je, mtoto anakojoa kitandani usiku, je ana hamu sana ya chakula, je anapungua uzito n.k.
Kwa hayo yote, mwisho wa siku ukienda hospitali ukakutana na daktari na kumweleza kila kitu, hakika utasaidiwa. Kufuatana na utakavyomweleza daktari, mtoto anaweza pimwa sukari kwenye mkojo na damu na vipimo vingine kadhaa ili kujua tatizo.
Kama mtoto wako ametoka sehemu ya baridi na kahamia sehemu ya joto pana uwezekano mkubwa asiwe na tatizo (ikiwa tumethibitisha anakunywa maji mengi zaidi ya itakiwavyo kwa umri wake), zaidi ya kuzoea mazingira ya joto. Mwone daktari wa watoto.