Mwanakijiji,
Binafsi kwa muda sasa nimekua nikiasa kuwa kuna haya ya `kumfufua` kambona katika historia ya nchi hii. Upotoshwaji uliofanywa kwa makusudi ni lazima usahihishwe. Kuna mengi chanya ambayo ni funzo kwa vizazi vya leo na hata kutoka kwa kiongozi huyu mzalendo.
Kwanini kumfufua?
Kambona ni miongoni mwa viongozi ambao vijana wa leo hawawafahamu kabisa. Hata pale anapotajwa,yanayofahamika kumuhusu ni hasi mno. Lakini ni wazi kuwa, alikuwa na ujasiri wa kupingana na nyerere. Aliweza kusimamia alichokiamini. Hii ni sifa muhimu sana ya kiongozi hasa ambaye anapaswa kuongoza nchi yoyote ya dunia ya tatu. Nyerere ana nafasi yake ya msingi na ambayo hakuna anayeweza kumpokonya. Hata hivyo, Kambona anapaswa kupewa nafasi yake katika historia ya nchi hii. Ni haki yake kwa utumishi na juhudi alizotia katika harakati za ukombozi na hata baada ya hapo.
Mwanakijiji, napingana na wewe kuhusu imani ya Kambona juu ya `demokrasia ya chama kimoja`. Kambona hakuliamini hili kama unavyopendekeza hapo juu. Kwanza,ushahidi pekee wa hiyo hotuba kwa kuitaja `demokrasia ya chama kimoja` katika hotuba yae,haitoshi hata kidogo kuonyesha kuwa alikua na imani nayo. Kama tukifikiria kwa muktadha ule wa baada tuu ya uhuru,ukichanganya na euphoria ya kupata uhuru,ni wazi kuwa Kambona hakua na nafasi na ushawishi wa kutosha wa kupinga pendekezo la Chama kimoja. Nyerere alikua kileleni kiushawishi. Lakini tunaona kadri muda ulivyokwenda Kambona alijenga ushawishi na ufuasi na hili linajionyesha wakati wa uasi wa 1964. Role ya kambona katika utatuzi wa uasi ule ni ishara tosha kuwa alikua kwenye nafasi tofauti kiushawishi. Na ni baada ya uasi ndipo tofauti kubwa kati ya Kambona na Nyerere zilipoanza kuonekana. Kwa mtizamo wangu, ni wazi kuwa Nyerere alianza kuona Kambona ni tishio.
Sababu ya pili ya kwanini kambona hakua anaamini katika `demokrasia ya chama kimoja` inatokana na uamuzi wake wa kutoroka nchini baada ya azimio la Arusha kutangazwa. Kama aliweza kuamini katika demokrasia ya Chama kimoja,ilimshinda vipi kuvumilia ujamaa? Ni wazi kuwa katika wakati huu,alikua na sauti ya kupinga tofauti na kipindi maamuzi ya chama kimoja yanapitishwa. Na hata baada ya kupinga, aligundua kuwa tayari alikuwa anaonekana tishio na kwa usalama wake ikampasa kuondoka.
Na tofauti yao kubwa haikuwa kuhusu chama kimoja tuu bali itikadi kwa ujumla. Na ni wazi kuwa waliokua na imani juu ya itikadi tofauti na ile ya Nyerere walikuwa wengi,siyo kambona tuu. Mzee Edwin Mtei ni mfano. Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alihojiwa na Issa G Shivji (Jarida, ChemiChem 2010) kuhusu sababu za kushindwa kwa ujamaa na akiwa anamjibu alisema tatizo walishindwa kujenga ufuasi. Ujamaa ulikuwa ukitekelezwa na watu wenye fikra za kibwanyenye.
Shukrani.