Lembrus Mchome katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA wilaya ya mwanga iliyopo mkoani Kilimanjaro ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho BAVICHA mkoani humo.
Februari 18, 2025 mmoja wa makada wa chama hicho,
Lembrus Mchome aliwasilisha
pingamizi la kupinga
uteuzi wa viongozi watendaji wa juu wa sekretarieti na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho uliofanywa na Mwenyekiti Tundu Lissu Januari 22, 2025 akidai kuwa umekiuka katiba ya chama hicho.
Mnamo tarehe 24 Februari 2025 Mchome
alichapisha kupitia mtandao wa X akitoa taarifa ya kufanya
mkutano na waandishi wa habari siku moja baadaye mkoani Arusha.
Kumekuwapo Chapisho linalosambazwa mtandaoni likiwa na kichwa cha habari
'mchome asema lissu aigawa chadema' likidaiwa kuchapishwa na JamiiForums likihusisha mkutano wa Mchome na waandishi wa habari.
Je, ni upi uhalisia wa Chapisho hilo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa chapisho hilo si la kweli, limetengenezwa na wapotoshaji kwani halijachapishwa na
JamiiForums kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Kwa kutumia QR-CODE iliyopo katika chapisho hilo JamiiCheck imebaini kuwa lilihaririwa kutoka kwenye
chapisho lililokuwa na habari iliyohusisha
tamko la ACT- Wazalendo la kutaka kuachiwa kwa mwenyekiti wa umoja wa walimu wasio na ajira NETO, aliyekamatwa mkoani Geita.
Uwepo wa QR-CODE katika machapisho yanayotolewa na JamiiForums kupitia mitandao yake ya kijamii unamuwezesha mtumiaji kupata kiunganishi cha taarifa husika kuelekea majukwaa yake hivyo kurahisisha kufanya uthibitishaji wa machapisho hayo yanapopatikana sehemu nyingine yoyote.