WALIOHOJI KUHUSU SUALA LA KUKATIKA KWA UMEME NA KUCHELEWA KWA MRADI WA JNHPP NI HAWA HAPA SOMA SEHEMU YA TAARIFA YAO ALAFU NDIO MRUDI HAPA KUBISHA
TAARIFA YA MWAKA YA SHUGHULI ZA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KWA KIPINDI CHA JANUARI, 2021 HADI FEBRUARI, 2022
[Imetolewa chini ya Kanuni ya 136 (15) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020]
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mradi muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa ni Mradi wa Kimkakati.
Ni matamanio ya Kamati kuona kuwa Mradi huu unakamilika kwa wakati ili kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, Kamati hairidhishwi na kasi ya utekelezaji wa mradi huu kwani maeneo mengi yapo chini ya wastani wa utekelezaji kimkataba.
iv. Kukatika Umeme mara kwa mara
Mheshimiwa Spika, Kamati ilipokea Taarifa ya Wizara kuhusu changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini. Katika Taarifa hiyo ilielezwa kuwa, kukatika kwa umeme kuna sababu zifuatazo:
i. Kutokuwa na matengenezo ya kutosha kwenye miundombinu ya ufuaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme;
ii. Uchakavu wa miundombinu ya kufua, kusafirisha na kusambaza umeme; na iii. Kuzidiwa kwa vituo vya kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na kuongezeka kwa watumiaji ukilinganisha na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Spika, Kamati Ilielezwa kuwa ili kukabiliana na changamoto hizi, tayari TANESCO imeandaa mikakati mbalimbali ikiwemo ya muda mfupi, wa kati na mrefu; na ili iweze kutekelezwa kikamilifu zinahitajika takribani Shilingi Trilioni 2.
Mheshimiwa Spika, Kamati inasikitishwa na sababu zilizotolewa kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini kwani Kamati inaona kuwa kukatika umeme mara kwa mara ni jambo ambalo lingeweza kuzuilika endapo Serikali ingechukua hatua madhubuti kwa kutekeleza mpango wa ukarabati wa miundombinu ya TANESCO na kuipatia fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati.
Hii ni sehemu ya TAARIFA YA KAMATI YA NISHATI