UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
"Wakulima kutambua kwamba kilimo sasa hivi ni biashara,” huu ni wito wa Afisa Kilimo wa Mkoa wa Geita, Mayunga John, ukibeba majibu ya mojawapo ya changamoto kubwa ambayo imeendelea kuwagharimu wakulima wa mkoa huo kwa miaka mingi, upotevu wa mazao ya chakula baada ya mavuno.
Katika sehemu mbili zilizopita za uchunguzi huu unaoangazia suala la upotevu wa mazao ya chakula kwa wakulima wilayani Geita, ilibainika jinsi uhifadhi usio bora unavyopunguza kipato cha wakulima, kuhatarisha usalama wa chakula wa kaya na kuchangia hasara zinazoweza kuzuilika. Uchunguzi huo pia ulionesha kuwa tatizo hilo halichochewi na sababu moja pekee, bali ni mchanganyiko wa upungufu wa elimu, uhaba wa maafisa ugani, utekelezaji usioridhisha wa sera, miundombinu duni pamoja na upatikanaji mdogo wa teknolojia za kisasa za uhifadhi.
Pamoja na ukubwa wa changamoto hizo, wakulima, wataalamu wa kilimo pamoja na viongozi wanaamini kuwa upotevu wa mazao unaweza kupunguzwa endapo kila mdau atatimiza wajibu wake.
Sheria Ndogo za Kilimo Kwanza na Usalama wa Chakula (Mamlaka za Wilaya), kifungu cha tisa, kimeweka wajibu wa moja kwa moja kwa Maafisa Ugani kuhakikisha wakulima hawafanyi kilimo kwa mazoea au kubahatisha. Sheria hizo zinawataka kuandaa programu ya kilimo ya kila mwaka inayozingatia hali ya hewa ya eneo husika, aina ya mazao yanayofaa kwa kila msimu, mbegu zinazopaswa kutumika, muda sahihi wa kupanda na kuvuna, pamoja na mbinu bora za kuhifadhi mazao baada ya mavuno.
Kwa mantiki hiyo, huduma za ugani ni wajibu wa kisheria unaolenga kuongeza tija, kupunguza hasara, na kuimarisha usalama wa chakula kwa kuhakikisha wakulima wanapata taarifa sahihi kwa wakati unaofaa.
Kwa baadhi ya wakulima, suluhisho linaanzia kwenye elimu, Kajina Kaisanga, mkulima wa mahindi kutoka Nyambugu, Manispaa ya Geita, anasema kuwa wakulima wengi bado wanahitaji kufikiwa na maafisa kilimo ili wapate maarifa ya mbinu bora za kuhifadhi mazao baada ya mavuno.
"Sisi tunawashauri muwe mnatutembelea mnatuelemisha ili tuelimike wote," anashauri Kajina.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Patrice Undole, mtaalamu wa kilimo kutoka mradi wa Kilimo Hifadhi unaosimamiwa na Kanisa la AICT mkoani Geita. Kwa mtazamo wake, hatua ya kwanza ya kupunguza upotevu wa mazao inaanzia kwa mkulima kuzingatia maarifa anayopatiwa kuhusu uvunaji na uhifadhi.
"Mkulima azingatie elimu tunayoitoa, anatakiwa azingatie kuvuna kwa wakati… Vilevile, kujitahifdi sana kukausha hayo mazao yake vizuri kabla ya kuyahifadhi. Kwa sababu asipoyakausha vizuri yanaweza kutengeneza sumu kuvu, yanakuwa bado yana unyevu unyevu. Pia, kusafisha yale mazao yake vizuri," anaeleza mtaalamu Patrice.
Patrice anaamini pia kuwa elimu hiyo haitakuwa na matokeo makubwa ikiwa itaendelea kuwafikia wakulima wachache, "Kuendelea kutoa elimu, na kuwafikia wakulima wote, kwa maana kwamba kuna wakulima wapo mbali sana na maeneo ya mjini ambao wana uhitaji mkubwa sana wa kutaka kufikiwa. Ni vizuri wakafikiwa wakapewa hii elimu ya uhifadhi wa mazao."
Afisa Kilimo wa kata ya Shiloleli, Matekere Mafuru anasema katika maeneo mengi ambayo wakulima wamepata elimu kuhusu matumizi ya mifuko ya kinga njaa, kiwango cha uharibifu wa mazao kimeanza kupungua.
"Kwa sababu sasa hivi tunawashauri wakulima wetu kutumia mifuko ya kinga njaa ambayo inakuwa na safu tatu za nailoni. Hiyo mifuko inakuwa na uwezo wa kuchukua debe sita, mkulima anapokuwa akivuna mahindi, yakikauka kabisa, yaani ule unyevu haupo kabisa, ndiyo anaweka kwenye hiyo mifuko ya kinga njaa. Huwa inauzwa Shilingi za Kitanzania 5,000. Yenyewe ni tofauti na kipindi kile walivyokuwa wanatumia hizi dawa za unga au za maji. Kwa hiyo wakulima baada ya kupata hiyo elimu, sasa hivi hiyo kitu huku kwetu imepungua," anazungumza Afisa Matekere.
Fortunatusi Zakayo, mkulima kutoka kijiji cha Rwamugasa, anapendekeza mfumo utakaowezesha elimu kuwafikia wakulima wengi zaidi hata katika vijiji ambavyo maafisa ugani hawafiki mara kwa mara.
"Ushauri wangu, yaani maafisa ugani wangepanua wigo, serikali ingewaagiza kila kijiji angalau waunde kamati ya wakulima hata watu watano. Yaani wale watano sasa ndiyo wanakuwa walimu wa humo kijijini, wanasaidiana na maafisa ugani," ushauri wa Fortunatusi.
Mathayo Kanyelema ni mmoja wa wakulima Geita wanaotumia mifuko ya Kinga Njaa ambayo imekuwa ikiwasaidia kuepukana na wadudu waharibifu wa mazao ya chakula.
Diwani wa Kata ya Shiloleli, Boniface Kaswahili anaona suluhisho linahitaji pia uwekezaji zaidi kwenye miundombinu ya kuhifadhi mazao, kwa kuweka shinikizo katika vikao vyao vya mabaraza.
"Ipo sasa sisi kama Madiwani kuweka hizo hoja kwenye vikao vyetu ili maghala haya yazidi kujengwa kwenye vijiji, kwenye Kata zetu ili wakulima wahifadhi mazao. Na hizi kinga njaa ziboreshwe vizuri," anasema Diwani Boniface.
Marcel Magayane, mkulima mwezeshaji kutoka kijiji cha Nyambogo anasema Tanzania ina sera nzuri ya kilimo, lakini changamoto kubwa ipo kwenye utekelezaji wake.
"Serikali iangalie kanda hizi zinaanza kilimo wakati gani. Lakini pia vyombo vya juu kidogo kama wilaya na mkoa, viweze kuteremka kuja chini kusaidiana na walioko chini, ilo kuangalia je, utekelezaji wa sera umekwenda vizuri. Sasa, viongozi wetu wa juu hapa hawateremki wamebaki pale pale. Utakuta hata suala la mbolea halifiki vijijini, viko mjini. Mkulima atoke hapa tulipo pembezoni kabisa mwa manispaa, aende Geita mjini kufuata mbolea, saa ngapi?" anasema Marcel.
Anaamini kuwa viongozi wa kisiasa nao wana nafasi ya kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakulima zinapewa uzito katika ngazi za maamuzi.
"Wabunge wanatakiwa kushiriki kwa wananchi masaa yote, na kama watashiriki vizuri, basi mkulima atajisikia vizuri, na mwananchi katika sekta zote atajisikia vizuri…Lakini baadhi ya Madiwani kweli wanafanya hivyo, na baadhi ya Madiwani hawafanyi," anasisitiza Marcel.
Gharos Riwa, mdau wa kilimo kutoka Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Geita, anaona viongozi, ikiwemo wabunge na madiwani wana nafasi muhimu ya kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakulima zinapatiwa ufumbuzi kupitia mijadala na maamuzi katika Bunge na mabaraza ya halmashauri.
“Hawa ndiyo wanaotunga hizi sheria, hata wanapoona kuwa kuna changamoto mahali, ni rahisi sana kwenda kutoa hoja Bungeni, kwenda kutoa hoja kwenye mabaraza ya halmashauri na kuweza kuwekewa mikakati ya kuweza kupata suluhisho la kudumu,” anasema Gharos.
Kwa upande wa serikali, Afisa Kilimo wa Mkoa wa Geita, Mayunga John, anasema tayari kuna mifumo inayotumiwa kuwasaidia wakulima kuhifadhi mazao yao, ikiwemo matumizi ya maghala ya serikali, vyama vya ushirika na taasisi zinazokusanya mazao.
"Changamoto kama hiyo kwa wakulima zipo, na njia kuu ambazo tunategemea ya uhifadhi wa mazao ya wakulima, ni hii njia ya kwanza ni ya asili, ile ya kutumia vihenge…pili, kwa kutumia hiyo mifuko inayozuia wadudu wasishambulie mahindi…kingine wanashirikiana na vyama vya ushirika, vina maghala ambavyo vinakusanya hayo mazao kwenye baadhi ya halmashauri, kama Geita vijijini," Afisa Mayunga akizungumzia juhudi zinazofanywa kukabiliana na upotevu wa mazao ya chakula.
Licha ya hatua hizo, anasema mafanikio ya kupunguza upotevu wa mazao yatategemea pia namna wakulima watakavyobadili mtazamo wao kuhusu kilimo na matumizi ya teknolojia za kisasa kwenye sekta hii muhimu na uti wa mgongo wa taifa.
"Wakulima kutambua kwamba kilimo sasa hivi ni biashara, pili, waweze kutumia teknolojia za uhifadhi zilizo rahisi kama matumizi ya hiyo mifuko ambayo imeboreshwa. Waweze kutumia vile vihenge vyao vya asili wanavyotengenezaga kwa ajili ya kuhifadhi chakula. Watumie miundombinu bora ya usafirishaji na kuvuna kwa wakati mazao, ili yasiweze kupotea," anashauri Afisa Mayunga.
Kutoka kwa wakulima hadi wataalamu wa kilimo, hakuna anayepinga kwamba upotevu wa mazao unaweza kupunguzwa. Kinachohitajika ni elimu inayowafikia wakulima kwa wakati, utekelezaji wa sera unaoendana na mazingira halisi ya vijijini, uwekezaji katika maghala na teknolojia za uhifadhi, pamoja na ushirikiano kati ya serikali, wadau wa maendeleo na wakulima wenyewe.
Kwa wakulima wa Geita, mafanikio ya kilimo hayapimwi tena kwa wingi wa mazao yanayovunwa, yanapimwa na kiasi kinachofika salama ghalani, kinachouzwa kwa bei nzuri sokoni, na kinachobaki mezani kuhakikisha familia inakuwa na chakula cha kutosha hadi msimu unaofuata. Jasho la mkulima litakuwa na thamani pale ambapo mavuno yake hayatapotea baada ya kutoka shambani.
Pia soma:
~ Uhifadhi mbovu unavyonyonya jasho la wakulima wa mkoani Geita
~ Jasho shambani, hasara ghalani: Chanzo cha upotevu wa mazao Geita
Andiko la: Dominic Allen
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.

Mkulima Herman Kehula akiwa katika eneo la kuhifadhia mahindi yake yaliyovunwa, akitumia vihenge kutunza mazao ya chakula, yakiwemo mahindi.