UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
Baada ya kufuatilia namna ambavyo uhifadhi duni unavyoendelea kusababisha upotevu wa mazao na hasara kwa wakulima katika mkoa wa Geita, swali linalobaki ni kwa nini tatizo hili linaendelea kujirudia mwaka baada ya mwaka? Licha ya kuwepo kwa sera ya kilimo, maafisa kilimo pamoja na teknolojia za kisasa za uhifadhi wa mazao.
Uchunguzi huu unaonesha kuwa jibu halipo kwa mkulima mmoja mmoja pekee, badala yake tatizo hili limejengwa na mnyororo wa changamoto unaoanzia kwenye ngazi ya utoaji wa elimu kuhusu masuala ya kilimo, utekelezaji wa sera, upatikanaji wa wataalamu wa kilimo, miundombinu, hadi namna rasilimali zinavyopangwa na kutumika kuwafikia wakulima.
Marcel Magayane, ambaye ni mkulima mwezeshaji kutoka kijiji cha Nyambogo, Manispaa ya Geita, anasema kuwa wameshawahi kufika kwenye moja ya kata ambayo hakutaka kuitaja jina, walikuta wakulima wakiwa dhoofu kwenye kilimo kutokana na changamoto ya kutofikiwa na maafisa kilimo katika maeneo yao.
“Tumekwenda kata ‘X’ (jina la kata limehifadhiwa) kwenda kupeleka elimu sisi wenyewe pale, mpaka wakawa wanashangaa, bwana shamba huwa hatumuoni, tulichokuja kukigundua hawapati mazao mengi kwa sababu hawapati elimu ya kilimo,” anazungumza Marcel.
Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna (2019–2029) unabainisha kuwa ukosefu wa miundombinu sahihi ya kuhifadhi mazao ni miongoni mwa sababu kuu zinazochochea upotevu wa mazao nchini, hususan kwa mazao ya matunda, mboga na yale ya jamii ya mizizi.
"Upotevu mkubwa unatokea kwenye mazao ya matunda, mboga na mazao jamii ya mizizi. Upotevu huo husababishwa na kukosekana kwa miundombinu sahihi ya uhifadhi wa mazao hayo." Mkakati huo unasema.
Mkakati huo unaeleza kuwa madhara ya upotevu wa mazao hujitokeza katika mnyororo mzima wa thamani, kuanzia kwa mkulima hadi kwa mlaji. Pia unaonya kuwa kuongeza uzalishaji pekee hakutoshi ikiwa mazao yataendelea kupotea baada ya kuvunwa.
"Tija ya kilimo kwa mkulima haitakuwa na faida iwapo masuala ya upotevu wa mazao baada ya kuvuna hayatapewa kipaumbele kinachostahili kupitia programu na mikakati mbalimbali. Hii itaathiri usalama wa chakula, lishe, ukuaji wa uchumi na pato la taifa," unabainisha Mkakati huo.
Kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2026/27 iliyowasilishwa Bungeni jijini Dodoma mnamo Aprili 28, 2026 na Waziri wa Kilimo, Daniel Godfrey Chongolo, sekta ya kilimo iliendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania mwaka 2025.
"Katika mwaka 2025, Sekta ya Kilimo imekua kwa asilimia 4.0. Aidha, imechangia asilimia 24.6 katika Pato la Taifa."
Akizungumzia mafunzo yaliyotolewa kwa maafisa ugani, Waziri Chongolo alisema kuwa Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa Mazao (COPRA) lilitoa mafunzo kuhusu viwango vya uzalishaji na ubora wa mazao ya ufuta na mikunde kwa maafisa 3,214 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Hata hivyo, miongoni mwa maafisa hao, Geita ilikuwa na afisa ugani mmoja tu aliyepatiwa mafunzo hayo, idadi ambayo ilikuwa ndogo ikilinganishwa na mikoa mingine kama Mtwara iliyokuwa na maafisa ugani 693 na Lindi 691.
“COPRA imetoa mafunzo kuhusu viwango vya uzalishaji na ubora wa mazao ya ufuta na mikunde kwa maafisa ugani 3,214 katika mikoa ya Mtwara (693), Lindi (691), Ruvuma (418), Morogoro (353), Kilimanjaro (153), Tanga (150), Arusha (133), Rukwa (109), Pwani (102), Katavi (94), Singida (77), Manyara (73), Dodoma (60), Kigoma (49), Simiyu (27), Mwanza (13), Shinyanga (8), Mara (6), Tabora (4) na Geita (1).”
Hali hii inaibua swali kuhusu uwajibikaji wa kiutawala, ikiwa huu ndiyo uwiano wa mafunzo yanayotolewa kwa maafisa ugani na mahitaji ya wakulima, hususan wale wa vijijini. Kama ni afisa ugani mmoja tu kutoka Geita ndiye aliyepatiwa mafunzo hayo, inakuwa muhimu kujiuliza ni kwa kiwango gani elimu hiyo inaweza kuwafikia wakulima wengi wanaohitaji maarifa kuhusu uzalishaji bora na uhifadhi wa mazao.
Waziri wa Kilimo, Daniel Godfrey Chongolo akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2026/27.
Fortunatusi Zakayo anasema katika kata anayoishi kuna afisa mmoja wa ugani anayehudumia vijiji vitano, jambo analosema linaifanya kuwa vigumu kwa wakulima wote kufikiwa na huduma za ugani.
"Maafisa ugani hawatufikii, kwa sababu wanakuwa labda mmoja kwenye kata, sasa akiwa mmoja maana yake ni kazi sasa kueneza kata nzima ili elimu iwafikie wakulima. Kata niliyopo mimi ina vijiji vitano, halafu kuna afisa ugani mmoja," anasema Fortunatusi.
Afisa Kilimo mkoa wa Geita, Mayunga John anakiri kuwepo kwa tatizo la upotevu wa mazao ya chakula, akisisitiza kuwa maafisa ugani wasiotekeleza wajibu wao huwajibishwa kwa mujibu wa sheria za kiutumishi.
“Kuna mfumo maalumu unaotumika kumpima mtumishi yoyote, ambapo afisa kilimo anaweka majukumu yake mle na anapimwa na na kiongozi wake anayemsimamia ngazi ya halmashauri. Kwa hiyo kwamba ametekeleza hiki na hiki. Lakini pia kuna motisha ambayo huwa inatolewa kwa watumishi wanaofanya kazi vizuri…Anayeshindwa kutekeleza majukumu yake, maana yake huyo automatiki hafai, anawajibishwa kwa mujibu wa sheria za kiutumishi,” anabainisha Afisa Mayunga
Mayunga anasema ufinyu wa bajeti katika idara husika, pamoja na vipaumbele vya halmashauri, vinaweza kuchangia na maafisa kilimo kutotekeleza majukumu yao vizuri au kuongeza ugumu katika mapambano dhidi ya upotevu wa mazao ya chakula.
“Changamoto za kiutawala, inawezekana ikawa ufinyu wa bajeti kama idara, lakini na vipaumbele kwenye halmashauri kwamba wanata wawekeze nini, pia na sera iliyopo kwa msimu huo mtahala wanataka wafanyiwe nini.”
Kwa mujibu wa Afisa Mayunga, mahitaji ya maafisa ugani mkoani Geita huwasilishwa kila mwaka kupitia utaratibu wa utumishi, huku serikali ikiendelea kuajiri wataalamu wapya na kuwapeleka kwenye halmashauri mbalimbali.
“Hilo sasa lipo chini ya Utumishi, mahitaji kama mahitaji ya maafisa ugani huwa yanawasilishwa kila mwaka na inafahamika, lakini mpaka sasa juhudi ya serikali wanaendelea kuajiri, ukifuatilia hata kwenye vyombo vya habari utaona kuna watu walioajiriwa wengi na wamesambazwa kwenye halmashauri mbalimbali,” anafafanua Afisa Mayunga.
Wakulima Bw. na Bi. Masumbuko Mungate wakiwa wamesimama nje ya ghala lao la kuhifadhia chakula, wakionesha jitihada za kutunza mazao baada ya mavuno ili kupunguza upotevu na kuhakikisha usalama wa chakula katika kaya yao.
Mbali na idadi ya wataalamu, hata elimu inayowafikia wakulima wakati mwingine hukumbana na changamoto nyingine, ambapo baadhi ya wakulima huwa hawapo tayari kupokea elimu inayotolewa na maafisa kilimo au wakulima wawezeshaji.
“Mimi pale kijijni ilikuja kampuni ya kilimo hifadhi, nikachaguliwa mimi kwenda kufundishwa kilimo hifadhi, lakini sasa changamoto unapoileta elimu kwa wakulima wanaokuzunguka, wao wanaona wewe unapoenda unalipwa au unafaidika, wanaona kama haina maana kukusikiliza,” anaeleza Fortunatusi.
Hata hivyo, kwa Marcel Magayane, mzizi wa tatizo haupo kwa wakulima pekee, anaamini kuwa pengo kubwa lipo katika utekelezaji wa sera, akisema pamoja na kuwapo kwa sera zinazolenga kuboresha sekta ya kilimo nchini, manufaa yake hayawafikii wakulima kwa wakati unaostahili.
“Sera yetu ni nzuri lakini utekelezaji ndiyo unalegea. Kwa mfano sera ya kwamba tulete mbegu ya mihogo ambayo inakingana na magonjwa ya mihogo. Lakini mbegu ile inaletwa mwezi tatu/nne unategemea hiyo mbegu inakwenda wapi? Haifiki kwa wakati,” anazungumza Marcel.
Pia soma
~ Uhifadhi mbovu unavyonyonya jasho la wakulima wa mkoani Geita
~ Jasho lisipotee ghalani: Njia za kuokoa mazao ya wakulima wa Geita
Mtaalamu wa kilimo kutoka mradi wa Kilimo Hifadhi unaosimamiwa na Kanisa la AICT mkoani Geita, Patrice Undole anasema changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika maeneo wanayotekeleza mradi wao.
“Sisi kuna sehemu ambazo tunatekeleza huu mradi, ukija kuangalia wengi wakulima wanalalamika kwamba wataalamu wengi hawafiki. Tunachokiona sisi, labda cha kwanza ni ile miundombinu, halafu vilevile, labda kutokuwezeshwa usafiri. Utakuwa mtaalamu wa kilimo anaishi kijiji hichi, ili aweze kufika kwenye kijiji kinachofuata, kuna kilomita 10, 15 au 20,” anasema Mtaalamu wa kilimo, Patrice.
Boniface Kaswahili, ni Diwani wa Kata ya Shiloleli, anasema kuwa kwa kiasi kikubwa ubovu wa baadhi ya barabara huathiri hata utoaji wa huduma za ugani, hasa nyakati za masika.
“Ni kweli kabisa, lakini ukiangalia hasa labda niseme nyakati za mvua…kwa mfano kama kwetu huku kutoka Kasamwa kuja Shiloleli ni changamoto sana kwenye masika…Niseme kwamba marafiki zetu TARURA waongeze bidii ya kuona miundombinu kama barabara kuziboresha kuziwekea madaraja, kuna barabara zingine zimeharibika mno mtaalamu hawezi kufika kwa changamoto hiyo,” maelezo ya Diwani Boniface.
Mkulima Herman Kehula akiwa katika eneo la kuhifadhia mahindi yake yaliyovunwa, akitumia vihenge kutunza mazao ya chakula, yakiwemo mahindi.
Wakati serikali ikieleza kuwa inaendelea kuimarisha huduma za ugani na kuongeza idadi ya wataalamu wa kilimo, ushahidi uliokusanywa katika uchunguzi huu unaonyesha kuwa bado kuna pengo kati ya sera na utekelezaji wake katika ngazi ya vijiji. Pengo hilo linaonekana katika upatikanaji wa huduma za ugani, ubora wa miundombinu, upatikanaji wa teknolojia za uhifadhi na uwezo wa wakulima kuzifikia kwa wakati.
Katika sehemu ya tatu ya mfululizo makala hii, uchunguzi huu utaangazia hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali, wataalamu wa kilimo, wadau wa maendeleo na wakulima wenyewe, ili kupunguza upotevu wa mazao ya chakula baada ya mavuno, pamoja na suluhisho linaloweza kuimarisha uhifadhi wa mazao na kulinda kipato cha wakulima wilayani Geita.
Andiko la: Dominic Allen
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.