RIWAYA : MPANGO WA CONGO
SEHEMU YA 23
Zahanati ya Rorya ndio iliowapokea majeruhi wa ajali iliotokea karibu na kiwanda cha samaki cha Nile perch.
Walikufa watu watatu akiwemo ofisa mmoja wa Polisi aliekuwa ndie dereva wa gari ile.
Miongoni mwa majeruhi wale alikuwamo Remi ambae alipata majeraha kichwani na baadhi ya sehemu mbalimbali za mwili.
Kitu pekee alichokumbuka kukihifadhi ni mkoba wake mdogo ambao alitembea nao kila sehemu.
Alitamani kutoka kwenye kitanda hasa baada ya kukumbuka jinsi alivyonusurika kuangukia mikononi mwa Mwendesha pikipiki.
Na ilikuwa ni kukosea hesabu labda upande wa wabaya wa Remi mana ajali ilitokea hatua mia kutoka kilipo kituo kidogo cha polisi cha Mwatex.
Na kwa kuwa gari lililopata ajali lilikuwa ni la Polisi; haikuchukua lau dakika mbili kabla askari Polisi hawajajaa pale hivyo kufanya mwendesha pikipiki akose lengo lake na kutimka.
Remi mwili haikurusu kabisa kuinuka na kuendelea na shuguli zake.
Akaamua kutulia tu..
Upande mwingine Mtega nyoka bado alikuwa hajapata la kuamua kabisa.
Aliona anahitaji kumpata Malima lakini pia aliona ni vyema akimpata Remi. Wote walikuwa muhimu kwake kwa wakati huo na aliwahitaji.
Akanyanyuka na kuligawa gazeti kwa mtu mwingine kisha akaita pikipiki alihitaji kwenda Kasuku Contractors haraka iwezekanavyo.
.
Haikupita hata dakika kumi akawa amefika zilipo ofisi za Kasuku Contractors.
Alimlipa dereva wa Pikipiki na kuelekea ulipo mlango wa utawala..
Alifika kwa binti aliekuwa amekaa mapokezi..
Hakukaa sana ni baada ya kuelekezwa nyumbani kwa mkurugenzi wa kampuni bwana Kindo Selemani na msanifu mkuu bwana Malima ambao wote hakuwakuta ofisini.
Akachomoka kuwahi ilipokuwa zahanati ya Rorya.
Nusu saa tu ilitosha kumfikisha mbele ya zahanati ile ya Rorya.
Ila alichokuwa amekifuata hakukikuta!!
Eba eeh!!
***
Mwasu alizipata taarifa za Remi kupelekwa kwenye zahanati ya Rorya. Vile alipata taarifa haijulikani ama ni kwa kusoma gazeti ama kwa mtu tofauti!
Alijua yeye!!
Baada ya kukamilisha taratibu za kulipia malipo ya huduma aliopokea Remi; Mwasu akapewa nafasi ya kwenda kuonana na mgonjwa wake ambae alijitambulisha kwenye uongozi wa zahanati kama ni Dada yake.!!
Tabasamu lilijijenga usoni mwa Remi baada ya kuomuona Mwasu na Mwasu nae alijawa na tabasamu lisilosemekana baada ya kumuona Remi.
Ilikuwa ni furaha baina yao!!.
"Nimekutafuta sana Dada yangu!!" alisema Remi baada ya kujaribu kuinuka na kuweza kukaa japo kwa shida kidogo.
"Usijali mdogo wangu,tumekwisha kuonana!!" alisema Mwasu huku akienda kumkumbatia Remi.
Walikumbatiana zaidi ya dakika tatu huku kila mmoja akiwa na hisia zake juu ya mwenzake kisha wakatengana.
Remi alijifuta machozi na kumshuhudia Mwasu nae akifanya vivyo hivyo.
Ilikuwa ni furaha iliochanganyikana na huzuni.
"Pole sana mdogo wangu!!" alisema Mwasu huku akikaa karibu na kitanda cha Remi.
Lakini kwa dakika chache tu Remi alizokaa na Mwasu alitambua mabadiliko makubwa kwenye mwili wa Mwasu.
Hakuwa Mwasu yule waliotengana miaka kadhaa kwenye kambi ya wakimbizi. Mwasu ambae alikuwa legelege na nyama uzembe nyingi.
Huyu alikuwa ni Mwasu alietengeneza mwili wake na kuwa wa kuvutia sana huku nyama zote zikiwa zimekaa pahala sahihi.
Mazoezi yalimjenga.
Remi hakujua ni mazoezi ya kawaida ama ni zaidi ya mazoezi ya kawaida.
Lakini pia Remi aliisikia mikoni imara ya Mwasu wakati wakikumbatiana.
Kwanini!? Hakutaka kujua hilo.
"Ahsante Dada" Hatimae alisema Remi.
"Jana nilipata taarifa zako,ila nilipofika pale nilipoambiwa upo sikukuta, nilihangaika hadi niliposoma gazeti ahsubuhi hii ya kuwa upo hapa na Majeruhi wengine kwenye ile ajali" alisema Remi huku bado akimtizama Remi.
Remi alitizama pembeni,kumbukumbu mbaya ya kilichotokea usiku ule ilimrudia, akajikuta chozi la uchungu linamtoka.
"Usijali mdogo Wangu,pumzika kwanza kisha utanisimulia tu!!" alisema Mwasu huku akimfuta machozi kwa upande wa Kanga aliokuwa amevaa.
Mwasu alitoka kidogo na baada ya dakika kadhaa alirejea.
"Mdogo wangu inabidi hapa tuondoke ukatibiwe sehemu nyingine! Huduma za hapa ni chini ya kiwango" alisema Mwasu.
Remi alishukuru kwa ukarimu wa ndugu yake huyo.
Kwa msaada wa matabibu wawili waliomsaidia kutembea kwa kumshika huku na huku,walifanikiwa kumuingiza ndani ya gari iliokuwa imesimama nje ya uzio wa Zahanati ile.
Wakati gari ile inaondoka pale ni wakati huohuo ambao pikipiki iliombeba Mtega nyoka iliingia ndani ya zahanati ile.
"Dakika chache zilizopita kuna mtu kasema ni Dada yake, amemchukua kwenda kwenye matibabu zaidi" alieleza Tabibu mmoja..
"Kasema ni hospitali gani wataelekea?" aliuliza Mtega nyoka.
"Hapana!!" alijibu Tabibu.
"naombeni kuona taarifa zake huyo aliemchukua mgonjwa!" aliongea kimamlaka Mtega nyoka.
Tabibu alibabaika kidogo! Ila baada ya kukutana na jicho kavu la Mtega nyoka; alitoa kitabu cha wageni.
Mtega Nyoka alisoma vyema namba za simu na mtaa alioishi Dada wa Remi;Mwasu.
.
Akaondoka kurudi Kasuku Contractors.
****
"Ni nani anahusika na usajili wa magari ya kampuni!" alihoji Mtega nyoka punde tu alipofika kwenye meza ya mapokezi.
"Kila kitu hufanywa na mkurugenzi!" alijibu binti aliekuwa mapokezi.
Ndilo jibu alilohitaji Mtega nyoka.
Akapitiliza hadi ofisi iliokuwa imeandikwa "MKURUGENZI" huku nyuma hakuzijali kelele zilizopigwa na dada wa mapokezi aliehitaji aombwe ruhusa y kuelekea huko ofisi za utawala.
Baada ya kugonga mlango na kuruhusiwa kuingia; Mtega nyoka akasukuma mlango na kuingia ndani.
Alikutana na sura ya Mzee wa makamo na kibao kilichokuwa mbele yake kilichokuwa na jina la Kindo Selemani.
"Kilichonileta kwako ni jambo dogo ila linaweza kuchukua muda kidogo kama..." alisema Mtega nyoka ambae alikatishwa na sauti ya majivuno ya Kindo.
"Sema shida yako moja kwa moja kijana tusipotezeane muda"
"Naomba kujua idadi ya gari zinazomilikiwa na kampuni yako tafadhali" alisema Mtega nyoka.
Kindo alishituka baada ya kusikia swali hilo.
Mshituko ambao Mtega nyoka aliuona dhahiri shahiri.
"Wewe ni nani! Polisi?" aliuliza kwa jaziba Kindo.
"Ni polisi ndio na ninayo ruhusa ya kukuhoji kuhusu umiliki wa magari ya kampuni" alisema Mtega nyoka huku akisimama kutoka alipokuwa.
"Unatakiwa kuongea na mwanasheria wa kampuni na si mimi!" alisema Kindo huku akianza kupeleka mkono ilipokuwa simu ya mezani.
Mtega nyoka aliwahi kumzuia.
"Nisingependa tusumbuane kwa jambo dogo hili ndugu!" alisema kwa upole Mtega nyoka.
Kindo akagwaya!
"Tatizo hujui unaongea na nani bwana mdogo nita..." hakumaliza kauli yake akajikuta akipokea bonge la Mkofi, uliomfanya aone shilingishilingi na kufumba macho na alipofungua hakuziona.
"Nisingependa tufike huko unakotaka ndugu" aliongea tena Mtega nyoka.
Kindo alibaki akitetemeka tu.
"Unajua unalofanya litakugarimu kijana" alisema Kindo huku sauti ikimkwama.
"Haya naomba kujua unamiliki magari mangapi" alihoji tena Mtega nyoka.
Kindo akainama kwenye droo na kutoa karatasi moja iliokuwa imenakishiwa na karatasi nyingine kwa juu yake.
Mtega nyoka aliichukua na kuisoma.
Alikutana na orodha ndefu ya magari ya kampuni ile na wanaoyatumia.
Hakuona gari namba T117DHJ.
Sijaona gari lilioungua moto huko Kitangili. Au halimilikiwi na kampuni yako." alihoji Mtega nyoka huku akimtizama usoni Kindo ambae alianza kutokwa jasho jepesi licha ya kuwa na kiyoyozi ndani ya ofisi ile.
"Afu kuna nini huko Dekuku!" alihoji tena Mtega nyoka.
Ilikuwa ni kabla ya jibu likatokea tukio moja matata lililohitaji akili na uwezo kulikwepa.
Mlango ulisukumwa kwa nguvu huku ukifuatiwa na mvumo wa kitu kilichokua kimemlenga katikati ya uti wa mgongo Mtega nyoka ambae bila kujiuliza alijipinda na kuangukia ubavu na kuacha kitu kile kiende kujikita kwenye kifua cha Kindo ambae alitoa mguno wa uchungu.
Kutoka alipoangukia; Mtega nyoka aliona mtu akiingia kwa kasi na bastola mkononi huku akiwa ameziba uso wake kama ninja.
Mtega nyoka nae kwa utalamu akawahi kuinuka pale chini na kutaka kumvaa mvamizi.
Mvamizi nae akaona kitendo kile haraka akarudi nyuma na kumpisha Mtega nyoka kisha akaachia risasi moja ilioenda kutua kwenye paji la uso la Kindo na kisha haraka akamgeukia Mtega nyoka.
Alichelewa!
.
Mvamizi alijikuta akipaa juu na kusukumwa kwa nguvu hadi ukutani na alipotaka kuanguka alijikuta akipokea mateke mengine mawili ya harakaharaka yaliomtia kiwewe.
Akataka kuinuka ajipange zaidi ila hakupewa nafasi na Mtega nyoka; akajikuta akipokea mateke mengine mawili chini ya magoti na kujikuta akitepweta kama aliepigwa na denda na kichaa.
Mvamizi alihusudu uwezo wa Mtega nyoka kwa vile alivyojua kucheza na nafasi alioipata.
Akagwaya!!
Mtega nyoka alijikuta amesimama peke yake baada ya kuona mwenzie aliepambana nae akienda chini bila upinzani zaidi.
Aliona damu ikimwagika.
"*****, what the fuc...!!" alisema mtega nyoka baada ya kuona adui aliechukua uhai wa Kindo nae uhai wake umechukuliwa.
Akabaki amesimama peke yake katikati ya chumba kilichokuwa na maiti mbili.
Haraka haraka akamkagua mvamizi,mfukoni alikuta kadi iliomshangaza kidogo!!
"inakuwaje hii!!"
Hakukuwa na wa kumjibu.
****
Wengine wanaendelea kujipatia uhondo wa riwaya hii na nyingine tatu kwa pesa ya Tsh3000/=
Yani unapata riwaya nne zilizokatika ubora kwa Tsh 3000/=tu.
Walionunua sasa wote wamejipatia nakala zao kwa email ama whatsapp.
Hujachelewa lipa hapa 0758573660 jina Bahati Mwamba upate riwaya.
Karibuni na ahsanteni kwa sapoti yenu