Tunaanzia hapa
WIKI iliyopita tulianza kuchapisha sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu kipya “Mateka Mpakani” kilichoandikwa na kachero wa Tanzania, Frowin Kagauka, kumuenzi mwenzake aliyeuawa mpakani mwa Tanzania na Uganda. Leo tunaendelea na sehemu ya pili.
…………………….
“AMESEMAJE wakati mlipomuuliza juu ya bastola hiyo? Amekubali ni yake lakini amekataa katakata kuwa yeye ni askari wa Idi Amin,” alinijibu Sajin Mkuu wa Kituo.
“OK. Sajin Binda wajulishe Bukoba ili waje kumhoji.” Niliamuru haraka. Sajini Binda alinipigia saluti nami nikaijibu kwa kubana mikono kwa vile sikuvaa sare za kijeshi na baadaye akaondoka haraka.
“Msimtoe humu mahabusu mpaka wakubwa zangu wafike kutoka Bukoba, sawa?” niliagiza. “Sawa afande,” alijibu Sajini ambaye ndiye mkuu wa kituo hicho kidogo cha polisi hapo kijijini Murongo.
Niliondoka hapo kituoni na ilipofika saa sita na nusu mchana nikijua wakubwa zangu watakuwa wanakaribia kufika hapo kituo cha polisi lakini hawakutokea mpaka saa nane na dakika kumi. Walifika kwa gari aina ya Landrover na wote walivalia sare za kijeshi isipokuwa dereva na mtu mwingine mmoja ndiyo walivaa kiraia.
Hao watatu waliovaa kijeshi mmoja alikuwa luteni na wawili makapteni. Waliovaa kiraia niliambiwa ni Luteni Emir wa Idara ya Usalama wa Jeshi ambaye ndiye aliyeendesha gari hiyo na Meja Stephen kutoka Idara ya Usalama wa Taifa mkoani Kagera. Wakuu hao waliamuru Kafumba atolewe mahabusu na alipotolewa wakamchukua na bastola yake kwenda naye Bukoba.
Sikumuona rafiki yangu Kafumba kwa zaidi ya wiki mbili ndipo siku moja bila ya kutarajia nikakutana naye sokoni hapo Murongo akizungumza na yule mpenzi wake.
“Ah! Rafiki wewe ni mbaya, umenipeleka polisi ili nifungwe bila kosa,” alilalamika. “Siyo hivyo, mimi nilishangaa kuona rafiki tangu una bastola na wewe ni bwana shamba. Naogopa sana askari ndiyo niliipeleka bastola yako polisi. Sasa wamekwambiaje?”
“Walinipeleka Bukoba nikaingizwa kwenye nyumba moja sijui ya nani, nikaulizwa maswali mengi ya Uganda na watu wawili ambao hawakuvaa kiaskari. Lakini watu wale walikuwa wema sana hawakunipiga wala kunisumbua na waliporidhika waliniachia nirudi lakini bastola yangu wamebaki nayo,” alinieleza huku akinikazia macho.
“Sawa bwana, basi tutaonana siku nyingine au leo kama bado upo hapa kwetu” nilimjibu kwa unyonge baada ya kuhisi yeye ni jasusi wa Idi Amin na ameweza kuwahadaa wakubwa zangu hadi wakaridhika kumuachia.
Wiki moja baadaye nikaletewa mwaliko kutoka kwa mzee niliyekuwa namheshimu sana, mzee Idris wa Green Hotel nikahudhurie sherehe yake aliyopanga ifanyike Jumamosi kuanzia saa tano asubuhi hapo hapo Green Hotel. Nikamjulisha Koplo Sudi na Sajin Binda juu ya mwaliko huo, kwa hiyo tukaondoka Murongo hadi Kivukoni. Tulipofika Kivukoni kama kawaida tukapanda boti na kuvuka mto Kagera ambao maji yake yanakwenda kasi sana kiasi cha kuwafanya wenyeji kushindwa kuvuka kwa kuogolea.
Baada ya boti kutuvusha tukatembea kwa miguu kilomita mbili na nusu hivi tukafika kijiji cha Kikagati ambacho kwa kweli ni kizuri kidogo kuliko kijiji chetu cha Murongo. Hapo Kikagati kuna kituo kidogo cha polisi ambacho kimejengewa badi tupu chini hadi juu, wengine huita mtindo huo ‘full suit’, vile vile kuna nyumba ya mkuu wa wilaya ambaye wenyewe walimwita DC na jengo moja kubwa la kampuni ya uchimbaji madini inayoitwa BMC.
Ilipotimia saa tano na dakika tano tulikwenda hapo Green Hotel huku tukiwa tumejaa shauku ya kunywa bia na kuvunja mifupa ya nyama ya kuku na mbuzi ya kuchoma. Kwa mshangao hapo Green Hotel hatukuona dalili yoyote ya sherehe na wala hakukuwa an watu wanaokula au kunywa kama ilivyokuwa kawaida. Kkilichonishangaza zaidi ni kutowaona hata watoto wake wakicheza nje ya hoteli hiyo ambayo mwenyewe mzee Idris anaishi humo humo kwenye vyumba vya uwani.
Kabla hajaamua kuuliza alifika mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa kati ya miaka sita na nane ambaye alituambia ameagizwa na mzee Idris atukaribishe ndani tumsubiri. Bila ya hofu tuliongozana na kijana huyo hadi kwenye sebule yam zee Idris ambayo kwa kweli hata siku moja hakuwahi kunikaribisha. Mtoto huyo alitutolea bia tatu za baridi kutoka kwenye hokofu, akatuwekea glasi kisha akaondoka. Dakika kama tano baadaye mzee Idris alifika na kutusalimu lakini hakukaa alituambia ana shughuli itakayochukua kama robo saa hivi lakini alitupa uhuru wa kujichukulia vinywaji kwenye jokofu. Wakati tunaanza kunywa bia huku bado nikitafakari jinsi ya sherehe hiyo tuliyoitiwa ilivyo, ghafla tukasikia mlio wa gari kubwa likisimama nje ya nyumba hiyo, bila shaka wote tulielewa huo ulikuwa ni mlio wa gari la kijeshi maana tulitazamana kwa mshangao.
Kabla hatujahamaki nini kinafanyika tukasikia vishindo vya hatua nzito za viatu vya kijeshi vikiizunguka hoteli hiyo. Tulipotazamana tena bila ya kusema lolote mlango ulifunguliwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aina ya AK47 kila mmoja, wakatuzunguka. Moyo ulinilipuka, mate yakanikauka kinywani, bia yote niliiona chungu na balaa tupu.
“Simama juu.” Aliamuru mmoja wa askari hao ambaye alikuwa na cheo cha Sajini. Wote tulisimama huku mikono yetu ikiwa juu kuomba amani. “Songa mbele haraka.” Aliamuru tena. Tulitoka nje ambako tulikuta askari wengine wanane waliovalia kivita wakiwa na bunduki mikononii wameizunguka hoteli hiyo. Raia wa kijiji hicho au niseme kimji hicho walisimama kwa mbali sana wakishuhudia tunavyokuwa MATEKA MPAKANI.
Tuliingizwa katika lori moja la kijeshi aina ya Liaz na safari ya kwenda tusikokujua ikaanza. Tulipofika njia panda ya kwenda Kabale ambayo ipo upande wa kushoto na Mbarara ambayo ipo upande wa kulia, lori hilo lilitimua vumbi kuelekea kushoto yaani Kabale.
Baada ya mwendo wa kama kilomita nne hivi kutoka hapo Kikagati tukaingia katika kambi ndogo ya jeshi inayoitwa Kabiyanda. Tuliteremshwa katika kambi hiyo ndogo na kuingizwa katika kijumba cha mabati matupu ambapo ndani hakukuwa na lolote mbali ya joto na hewa nzito kwa vile hakukuwa na dirisha bali vitundu vidogo vipatavyo sita tu.
“Tunakuwa mateka mpakani, sijui watatufanyaje. Nahisi hizi ni njama za Kafumba, Kafumba lazima ni jasusi, alikuwa anatupeleleza. Sijui Idi Amini ana nia gani na sisi au nchi yetu…niliwaeleza wenzangu huku nikitetemeka. “Ni dhahiri Kafumba amelipiza kisasi. Lakini nahisi mpango huu ulikuwa ni wa muda mrefu,” alijibu Koplo Sudi.
Saa tisa tulitolewa humo kwenye kijumba na kukalishwa chini kwenye uwanja niliohisi ni wa kufanyia kwata. Koplo Sudi na Sajini Binda walikuwa wananitazama mara kwa mara kama vile wananiulaumu kwa kuwaingiza katika janga hili, lakini sio kosa langu bali ni tamaa yetu ya kunywa bia na kumuheshimu mzee Idris.
“Nani mkubwa kati yenu?” aliuliza Luteni mmoja mweusi mwenye sura mbaya. Hakuna aliyejibu hivyo akaona tumemdharau kaamua kumwita koplo mmoja aliyekuwa amesimama kwa mbali akituangalia.
“Funsa adabu hawa” alimwamuru koplo huyo aliyevalia kivita kwa Kiswahili kibaya kisha akaondoka zake kwa hasira.
“Ah! Mnataka ‘kufunswa’ heshima, hebu simameni.” Tuliinuka kwa hofu huku tukimwangalia nini anachodhamiria kutufanyia. “Nyinyi ni askari?” “Hakuna askari hapa kati yetu” nilimjibu haraka kwa hasira. “Eh! Wewe ndiyo mkubwa enh!” “Mkubwa wa nini?” nilimjibu na kumfanya acheke kidogo.
“O.K nyinyi mnajua Kiswahili kingi sana, hebu chuchumaeni chini huku mkishika masikio yenu.” “Tuonyeshe mfano,” nilimwambia bila hofu.
“Eh! Nyinyi jeuri sana, hebu laleni chini kifudifudi niwachape kidogo fimbo,” alitamka huku akitabasamu. Wakati tunalala kifudifudi ghafla alikuja askari mmoja asiye na cheo na kumwambia mwenzake kwamba tunatakiwa tuingie ndani ya gari tupelekwe katika kambi ya Mbarara. Tuliingizwa ndani ya Landrover moja ya jeshi la Idi Amin huku tukilindwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aian ya AK 47 mikononi. Landrover ikapigwa moto na safari ya Mbarara ikaanza. Ilibidi turudi tena mpakani Kikagati kisha tufuate barabara inayoelekea Mbarara ni kama kilomita 150. Tulipofika Mbarara giza lilikuwa limekwishaingia, dereva akasimamisha gari nje ya lango kuu la kambi kubwa ya jehsi ambayo baadaye niliitambua inaitwa Simba Battalion. Taa kubwa ya usalama ikawashwa na kuzimwa kama ilivyo kawaida katika kambi nyingi za jeshi kisha sauti kali ilitaka utambulisho.
“Tumeleta mateka kutoka Kabale” alijibu askari mmoja aliyekaa mbele. Taa iliwashwa tena na kuzimwa halafu mlango ukafunguliwa. Niliona sanamu mbili za samba zilizokuwa upande wa kulia na kushoto mwa lango hilo ambazo zilinifanya nielewe maana ya kambi hiyo kuitwa Simba. Gari iliingia na kuegeshwa nje ya jengo dogo ambalo hata mtu asiyekuwa askari angegundua ni mahabusu.
Tuliamriwa kuteremka na mlango wa mahabusu ukafunguliwa, tukaingizwa. Mahabusu hiyo ilikuwa karibu na lundo la kuni na kwa mbele kidogo kulikuwa na msikiti mdogo. Ndani ya mahabusu hiyo hakukuwa na taa kwa hiyo ilibidi tutulie kimya bila kuongea wala kutembea.
Ulikuwa usiku mgumu sana kwetu hasa kwa mimi kiongozi kwa vile wenzangu walionyesha wamekata tamaa kabisa. Kama kawaida ya usiku ni lazima uche hata kama unapata taabu au raha ni lazima asubuhi ifike. Asubuhi ilipofika tulitolewa nje na kupelekwa katika ukumbi mmoja mdogo ambapo tulikalishwa chini. Dakika kama kumi baadaye waliingia wanajeshi wanne, watatu wakiwa na cheo cha meja na mmoja alikuwa kanali. Kwa jinsi walivyoonekana, walikuja kutuhoji.
“O.K Watanzania, tunaanza na wewe, inuka ujibu maswali yetu.” Alitamka kanali huyo huku akimuonyesha kidole Koplo Sudi. Koplo Sudi aliinuka wima huku akigwaya. “Unacho kitambulisho chochote hapo ulipo?” aliuliza meja mmoja ambaye ni mrefu zaidi ya wenzake. “Sina kitambulisho.” “Sawa, vua shati na suruali yako,” aliamuru kanali huyo.
Koplo Sudi akavua suruali na shati lake na kuviweka mbele yake. “Wewe unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza meja mwingine ambaye ndiye aliyekuwa akinukuu maelezo yetu.
“Nafanya biashara ya kuuza vitabu sokoni,” alijibu Koplo Sudi huku akigwaya.
Ukisema kweli utapona, lakini ukitudanganya ujue hutaiona tena Murongo,” alitamka kanali huyo kwa Kiswahili kizuri. “Kwani sisi tumewakosea nini? Kosa letu ni nini mpaka mnataka kutuhukumu?” “Hamjafanya kosa lolote, lakini tunataka majibu y kweli,” alisisitiza kanali huyo.
“Unajua sisi tunawaelewa nyinyi vizuri sana, na kuonya tena. Usiseme uongo” alifoka kanali. “Sisemi uongo,” alisisitiza Koplo Sudi. “Jina lako nani?” aliuliza kanali huyo mweusi tii. “Abdallah Salum,” alidanganya. “Hatuna jina la Abdallah katika orodha tuliyoletewa.” “Kama mnayo orodha ya majina yetu kwa nini mnaniuliza jina?”
“Nyinyi wote ni wanajeshi, hiyo tunajua kwa hakika, sasa wewe unajifanya mfanyabiashara. Nakwambia mara ya mwisho, sema ukweli wako vinginevyo huwezi kurudi kwenu. Hatupo hapa kufanya mchezo,” alifoka kanali huyo.
“Umeelewa sasa, yajibu maswali yetu kwa ukweli” aliongeza meja anayeandika.
“Jina lako nani na unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza meja huyo. Swali hilo lilimfanya Koplo Sudi aanze kutoa mchozi ambao uliniumiza sana moyo.
“Unalia kabla hujateswa, sasa ukiteswa si utakufa kabisa” alitamba meja. Maneno hayo hayakupunguza kasi ya machozi ya Koplo Sudi, kwa hiyo kanali akamwambia arudi aka echini.
“Zamu yako wewe, inuka kuja hapa” alitamka kanali huku akinielekezea kidole. Niliinuka nikapiga hatua tatu na kusimama. “Wewe ujibu maswali yetu kwa ukweli, hatutaki uwongo wala kilio hapa.”
“Sawa,” nilijibu kisha nikakohoa kidogo ili kusafisha koo. “Jina lako nani,” aliuliza kanali. “Nelson,” nilijibu. “Jina lako lingine” “Njata, Nelson Njata. “Yah! Jina la Njata lipo hapa” alidakia meja aliyekuwa anaandika. “Unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza kanali. “Mimi ni bwana shamba.”
“Tunajua ni bwana shamba, lakini una kazi nyingine pale?” alidakia meja mwingine. “Kazi gani nyingine?” niliwauliza bila wasiwasi. “Unamjua Dan Kafumba?” aliuliza kanali na kunifanya nishtuke. “Namjua ni Mganda na pia ni rafiki yangu.” “Nani alimfikisha polisi?” aliuliza kanali huku akinikazia macho.
“Alijipeleka mwenyewe baada ya kupoteza bastola yake.” “Unaonyesha wewe ni mtu jasiri na mjuba, bila shaka wewe ni mwanajeshi, tena mwenye cheo kikubwa au sivyo? Alidakia meja anayeandika.
“Sivyo, mimi ni bwana shamba, hata Kafumba angekuwapo hapa angenisaidia kuwathibitishia.” “Pale Murongo kuna kituo chochote cha jeshi?” aliniuliza kanali. “Mimi sijui na wala sioni umuhimu wa kujua mambo ya jeshi.”
“Naona wewe nmi mwerevu sana kwa hiyo itabidi uhojiwe kwa nguvu, nenda ukakae,” alitamka kanali kwa ukali.
Nilirudi nyuma polepole na kukaa chini. Sasa ilifia zamu ya Sajini Binda kusimama, lakini maofisa hao walinong’ona kidogo kisha ghafla waliinuka na kuondoka zao. Kwa jinsi walivyoonekana walivyokuwa, kwa vyovyote ni maofisa wa Idara ya Ujasusi wa Kijeshi au ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kama nusu saa baada ya maofisa hao kuondoka mlango ulifunguliwa na askari mmoja asiye na cheo akiwa amebeba chano iliyokuwa na bakuli tatu zilizokuwa na uji, akatugawia kila mmoja bakuli lake, tukaanza kunywa huku akituangalia.
Uji huo wa unga wa mahindi ulikuwa wa moto sana na haukuwa na sukari, hata hivyo hiyo haikutuzuia kunywa kutokana na njaa tuliyokuwa nayo. Baada ya kama robo saa hivi tulishamaliza kunywa uji huo na askari huyo akachukua bakuli zake na kuondoka.
“Sijui wanataka nini kwetu?” aliuliza Koplo Sudi kwa unyonge. “Hii yote ni kazi ya yule rafiki yangu Kafumba ni lazima ni jasusi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi hii yaani State Research Bureau” lakini kwa vyovyote itakavyokuwa asitokee mtu kati yetu akavunja kiapo chetu” nilitamka huku nikiwakazia macho.
Wakati Koplo Sudi anavaa nguo zake alizokuwa amezivua, mlango ulifunguliwa na askari mmoja aliyekuwa na bunduki aina ya AK 47 mgongoni, akatuamuru tutoke nje. Tulipotoka nje tulikuta askari zaidi ya kumi wenye silaha wakitusubiri. Tulipekuliwa kama tuna silaha na walipoona hatuna walitunyang’anya saa zetu na viatu. Baadaye wakatuamuru tuingie katika lori moja aina ya Benz lililoegeshwa mita kama kumi kutoka hapo. Humo ndani ya lori tulifungwa kamba mikononi na miguuni na safari ya tusikokujua ikaanza lakini njiani askari mmoja aliripoka kwa mwenzake kwamba tutafika katika kambi ya Makindye saa kumi na mbili jioni.
Kambi ya Makindye niliwahi kuisikia kutokana na sifa zake za utesaji na uuaji na ni maalumu kwa kutesea mateka wa vita au askari waasi. Kambi hii niliambiwa ni ya Polisi jeshi tupu (Military Police).