Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 9
…………………..
WIKI iliyopita tuliona namna kachero wa Tanzania alivyokaribishwa nyumbani kwa mwanadada Elizabeth. Tuliona pia wakati kachero huyo anakwenda kuoga, akasikia mwanadada huyo akipiga simu na kunyata karibu yake ili kumsikiliza, akihisi alikuwa akiwasiliana na majasusi wa shirika la ujasusi la aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin, (State Research Bureau- SRB). Endelea
……………
HARAKA nikatoka kwenye dishi hilo la kuogea nikanyata kuusogelea mlango ambao niliusindikiza huku moyo wangu ukienda kasi kutokana na kuhisi kwamba ananichongea. Hapo nyuma ya mlango nilitulia kama vile mamba anasubiri mawindo ndani ya maji, nikimsikia Elizabeth akieleza habari zangu, moyo wangu ukazidi kulipuka na mate yakanikauka.
Baada ya kugundua hivyo nikarudi haraka kwenye dishi la kuogea, nikaoga haraka haraka lakini ghafla Elizabeth alifungua mlango. “Hujamaliza kuoga tu? Njoo bwana tulale.” Aliniambia huku akitabasamu. “Nakuja sasa hivi,” nilimjibu huku nikitoka kwenye dishi.
Moyoni nilikwishamtilia shaka Elizabeth kwamba ni mfanyakazi wa serikali mwenye cheo cha juu na pia amepewa nyumba nzuri ya kuishi inayofanana na nyumba za serikali za Oysterbay (Dar es Salaam). Wakati nilipotoka chooni nilimkuta Elizabeth amekwishajilaza kwenye kitanda chake cha futi sita ambacho kwa kweli ni kitanda cha gharama kubwa.
Mapigo ya moyo yakaongezeka kwa kasi lakini siyo kwa ajili ya hofu bali kwa ajili ya tamaa ya ukware. Mwili ulinisisimka na mishipa kutanuka, nikajitupa katika kitanda hicho bila kukumbuka kwamba amekwishanichongea.
“Karibu” alitamka Elizabeth kwa sauti nyororo yenye kuonesha kwamba tayari akili zake zimekwishaingia katika dimbwi la mapenzi. Alinikumbatia na kunigeuza nikawa juu yake… lakini kabla sijachukua hatua yoyote simu ikaita. Eliza akakurupuka kitandani na kuinua mkono wa simu iliyokuwa juu ya meza ndogo nzuri ya vioo tupu.
“Hello, hello” aliita Elizabeht huku akiinua simu hiyo na kwenda nayo sebuleni ili nisisikie anayotaka kuongea. “Yes, yes, o.k” alisikika akiitikia. Aliporudi alionyesha ni mwenye wasiwasi kidogo kwa hiyo sikusita kumuuliza. “Kuna nini?” “Hakuna wasiwasi ni rafiki yangu amenipigia simu,” alijibu kunitoa hofu. “Mbona hizi nyumba kama za serikali?” lilinitoka swali bila kutegemea. “Kwa nini unauliza hivyo?” “Naona zinafanana na nyumba za serikali za Tanzania na hata zile za Kenya. Si unajua Waingereza walitutawala kwa hiyo vitu vingi vinafanana.” Nilitamka na kumfanya Elizabeth anikazie macho.
“Wewe uliwahi kufanya kazi serikalini?” aliniuliza lakini kabla sijajibu nikasikia kengele ya mlango inagonga. “Vipi nani tena usiku huu?” nilitamka huku nikibabaika. “Sijui ngoja nikaone,” alijibu huku naye akitweta kwa hofu.
Wakati Eliza anakwenda kufungua mlango, haraka haraka nikachukua nguo zangu na viatu nikavaa na baadaye nikamfuata mlangoni. Aliponiona nimemfuata mlangoni huku nikiwa nimekwishavaa nguo zangu alibabaika sana kuufungua mlango wa pili ambao ni wa grill. “Ah! Imekuwaje?” aliniuliza lakini sikumjibu kitu, wakati huo huo nikasikia mlio wa gari kwa nje nilioutambua ni wa Landrover ikisimama nje ya nyumba hiyo.
Kwa kweli niliogopa sana nikajua sasa nimepatikana. Hata hivyo kwa kutumia uaskari wangu nikapata mbinu ya haraka ya kujiokoa. Haraka haraka Elizabeth akafungua mlango huku mimi nikiwa nimejibanza nyuma ya mlango wa ndani karibu naye.
Wanaume wanne waliovaa suti nyeusi waliingia ndani kama umeme huku wakiwa wameshika bastola mikononi lakini kabla hawajatahamaki mimi nikazima taa na kuwapiga kikumbo.
Wawili walianguka ndani na mmoja aliyekuwa karibu na mlango aliangukia nje pamoja na Elizabeth na mwingine akabaki ameduwaa. Hapo nje nikaikuta gari aina ya Landrover ya rangi ya bluu iliyochanganyika na nyeusi kidogo, nikaigundua ni gari ya State Research Bureau (SRB).
Dereva wa gari hiyo alipoona kizaazaa hicho cha wenzake kuanguka chini na mimi natoka akahamanika, akafungua mlango wa gari akitaka kuniwahi lakini hakuweza.
Nilikimbia kama swala anayemkimbia simba huku milio ya risasi ikivuma nyuma yangu. Sikusimama wala kugeuka nyuma niliongeza kasi mpaka nilipofika kwenye uwanja mkubwa ambao niligundua ni wa mpira wa miguu.
Huku nikiwa natweta kwa nguvu nilikaa chini nikaangaza macho huku na huku kuthibitisha usalama wangu. Hakukuwa na kitu chochote cha kutilia shaka, usiku ulikuwa tulivu lakini wa kutisha sana kwa sababu kulikuwa kimya sana na hakukuwa na mtu yeyote anayetembea barabarani mbali na magari ya jeshi yaliyokuwa yakipita mara kwa mara. Nilihisi magari hayo yalikuwa katika harakati za vita si kunitafuta mimi.
Nilijilaza chali huku nikijaribu kuwaza namna nilivyoponyoka kwa maofisa wale wa Usalama wa Taifa wa Uganda lakini sikupata jibu ulikuwa ni muujiza wa Mungu tu. Hali ya hapo kiwanjani ilikuwa ya baridi sana lakini sikushangaa kwa sababu najua mstari wa Ikweta umepita Uganda na Kenya, kwa hiyo hali hiyo ni ya kawaida.
Joto huwa joto na baridi huwa baridi. Labda kilichonifariji kidogo ni kutokuwapo mbu katika eneo hilo kwa hiyo nikajigeuza na kulala kifudifudi ili kuizuia baridi isinishambulie hadi kuamsha ule ugonjwa wa pwani, ngiri. Kwa kweli usingizi wangu ulikuwa wa mang’amung’amu.
Hata hivyo, pamoja na adha yote niliyoipata mahali hapo usiku haukuchelewa. Sauti za jogoo zilizosikika kwa mbali zilinisaidia kunijulisha kwamba mawio yanakaribia. Baadaye kidogo sauti ya adhana na za ndege zikasikika vizuri masikioni mwangu nikajua siku mpya imeanza.
Wazo la kuufuata mzigo wangu kule katika nyumba ya kulala wageni ya Owino lilinijia lakini nikalipuuza kwa vile nilihisi nikiendelea kuzubaa hapa mjini wanaweza kunitia mbaroni. Nikajipapasa mfukoni kuthibitisha kama dola zangu za Kimarekani alizonipa Padre Franz zipo na nilipothibitisha zipo nikafikicha macho na kuangaza huku na huku ili kuthibitisha kama nipo salama.
Baada ya kuthibitisha nipo salama nikainuka na kujinyoosha mgongo kisha nikaondoka eneo hilo bila kuwa na uhakika hasa wapi ninakoelekea ingawa azma yangu ni kuondoka katika jiji hilo siku hiyo. Nilitembea njiani bila kukutana na askari yeyote na hata watu wachache niliopishana nao hawakuwa na habari na mimi. Kwa kweli nilishukuru sana Mungu.
Katika tembea yangu hiyo ghafla nikajikuta nimetokea katika barabara iliyokuwa na kibao kilichoandikwa Naguru. Nikaifuata barabara hiyo na kujikuta napita karibu na uwanja mzuri wa michezo ulioandikwa K.C.C Sports Ground wa eneo hilo linaloitwa Lugogo ambao ulikuwa upande wa kulia na upande wa kushoto kulikuwa na nyumba zilizojengwa vizuri kwa mpangilio kama za Shirika la Nyumba (NHC).
Baadaye nikaiacha barabara hiyo inayoenda katika eneo la viwanda na kukatiza hadi kwenye stendi ya mabasi iliyopo karibu na soko linaloitwa Nakawa ambalo lipo karibu na barabara kuu ya Jinja. Hapo stendi nikakuta hekaheka kubwa utafikiri ni mchana. Watu walikuwa wanapanda mabasi, wengine walikuwa wanashusha mizigo na wengine kupandisha mizigo ili mradi mahali hapo palionekana kumekucha.
Muda mrefu baadaye nikajitumbukiza katika mgahawa mmoja ulioandikwa Super K Tea Room ambao kwa kweli nilipoingia ndani sikuamini macho yangu kama kweli mgahawa huo unastahili kuitwa super kwa jinsi ulivyokuwa shaghalabaghala sana kwa sababu kwa kawaida migahawa mingi inayozunguka eneo la soko na stendi ya mabasi mara nyingi inakuwa michafu kutokana na idadi kubwa ya wateja wanaoingia ambao wengi wao wanakuwa na haraka.
Nilipomaliza kufungua kinywa nikanunua mswaki na dawa ya meno aina ya Signal kisha nikanunua maji ya chupa ambayo niliyatumia kupigia mswaki na kunywa. Baadaye nikasimama kidogo hapo stendi ya mabasi nikishangaa jinsi watu wanavyoingia na kuteremka katika mabasi bila kugombea ingawa idadi yao ilikuwa kubwa ukilinganisha na ile ya mabasi. Ghafla macho yangu yakatua katika basi moja aina ya Isuzu lililoandikwa Mengo Jinja Express ambalo lilikuwa linaelekea Jinja hadi Tororo. Bila kufanya ajizi nikajitumbukiza katika basi hilo kwa nia ya kuondoka Uganda kupitia Kenya.
Tororo ni mji wa mpakani kati ya Uganda na Kenya lakini upo upande wa Uganda. Humo ndani ya basi zilibaki nafasi kama sita tu ili basi lijae. Nikakaa katika kiti cha pili kabla ya kufikia nyuma kabisa. Abiria watatu wanaume waliokuwa wameketi kiti cha mbele yangu walikwua wakizungumzia vita iliyoanza katika mpaka wa Tanzania na Uganda. Basi lilipoondoka hapo Nakawa tulipita Mukono, Seta, Namataba na Lugazi ambayo ni miji midogo inayofanana sana na miji ya Tanzania kama Muleba na Biharamulo.
Humo ndani ya basi maelezo ya vita yalishamiri sana kiasi cha kunitia hofu. Baadhi ya Waganda waliokuwa wakiongea niliwasikia wakisema majeshi ya Amin yanakaribia kuuteka mkoa mzima wa Kagera na kuufanya uwe sehemu ya Uganda. Maneno hayo yalinikera sana lakini sikuwa na la kufanya bali kushughulikia namna nitakavyotoka aslama katika nchi hiyo.
Baada ya mwendo wa takriban saa nne tukafika Jinja ambapo baadhi ya abiria waliteremka na wengine wakaingia. Mji wa Jinja ni mkubwa kidogo, unafanana sana na mji wa Morogoro na hata jinsi viwanda vilivyozunguka kando ya mji huo vinafanya ufanane zaidi na Morogoro ingawa kwa kweli Jinja ina viwanda ni vingi zaidi na pia ni maarufu duniani kutokana na maporomoko ya Owen ambayo hutoa umeme mwingi.
Hekaheka za hapo stendi ya basi ya Jinja zilikuwa kubwa kuliko zile nilizoziona katika stendi ya basi iliyokuwa karibu na soko la Nakawa jijini Kampala. Labda kwa sababu mji wa Jinja una sifa ya kuwa na viwanda vingi vikubwa, hoteli nyingi nzuri na watalii wengi ambao hufika katika mji huo kuangalia chanzo cha mto Nile. Mto Nile huanzia Jinja hadi katika Bahari ya Mediterania.
Mbali ya mabasi mengi hapo stendi kulikuwa na pikipiki kubwa nyingi ambazo abiria tuliyekaa naye kiti kimoja aliniambia kwamba pikipiki hizo ni za kukodi ziendazo Tororo na Kampala. Aidha, aliniambia pikipiki hizo ambazo hukodishwa na watu wenye safari za haraka zinajulikana sana nchini humo kwa jina la bodaboda. Abiria huyo ambaye alikuwa akiongea kwa ufasaha Kiingereza aliniambia mbali ya kuwepo hizo bodaboda pia kuna teksi ambazo huziita special hire zinazotumiwa sana na watu wenye uwezo kifedha.
Tuliondoka Jinja saa sita kamili mchana na baada ya kutoka mjini tukaanza kupita maeneo yenye viwanda mbalimbali na mashamba makubwa ya miwa utafikiri Kilombero. Mbali na mashamba hayo ya miwa, tuliyapita mashamba mazuri ya pamba ambayo kwa kweli yalivutia macho sana.
Baadaye tukaingia mji mdogo unaoitwa Iganga ambao naweza kuufananisha na mji wa Korogwe wa mkoani Tanga. Hapo tulisimama kwa dakika kama kumi hivi na baadaye safari ya Tororo mji wa mpakani ikaanza. Kabla ya kufika Tororo tulivuka daraja kubwa kama lile la Wami katika barabara ya Chalinze hadi Segera.
Daraja hilo niliambiwa ni la mkono wa tano wa mto mkubwa unaoitwa Kyoga. Kilomita chache baada ya kuvuka daraja hilo niliona kwa mbali mbele yetu milima mkubwa niliambiwa inaitwa Elgon, iliyopo nchini Kenya.
Moyoni shauku ya kufika Tororo iliongezeka sana, lakini tulipofika karibu na bao kubwa lililoandikwa “Tororo welcomes you” lenye kuonesha tunaingia Tororo tukasimamishwa na askari wa jeshi la Idi Amin Dada ambao walitisha sana kutokana na jinsi walivyovaa kivita huku kila mmoja akiwa na bunduki.
Askari hao waliokuwa kama 18 au 20 hivi walionesha hawana mchezo hata kidogo. Kando ya barabara kulikuwa na magari mawili ya dereva, lori moja aina ya Tata na Landrover mbili. Kiongozi wa askari hao aliyekuwa na cheo cha luteni kanali aliamuru abiria wote tuteremke na basi lipekuliwe.
Tukiwa nje ya basi hilo kila mmoja wetu alitakiwa aoneshe kitambulisho au hati ya kusafiria. Hali hiyo ilinifanya nijisikie kutaka kujisaidia haja ndogo na tumbo la kuharisha ghafla. Mate yalinikauka na mwili ukaanza kufa ganzi. Nilifikiria nitimue mbio lakini nilijua haitanisaidia kitu kwa sababu bunduki zote za askari hao zitaelekezwa kwangu, kwa hiyo nitapoteza maisha.
Ilipofikia zamu yangu kujieleza nikajipa moyo na kueleza kwamba mimi ni Mtanzania ninayeishi nchini Kenya, nilikuja Uganda kufanya biashara ya mitumba ya nguo lakini nilipokuwa Jinja niliibiwa begi langu ambalo lilikuwa na hati zangu mbalimbali na pasipoti.
“Wewe huna kitambulisho chochote?” aliuliza kwa ukali luteni aliyenihoji. “Umetoka wapi? Uliingia lini Uganda?” alizidi kuniuliza luteni huyo lakini kabla sijajibu nilivutwa na askari mwingine mwenye cheo cha kapteni aliyekuwa amesimama kando akisimamia utekelezaji wa ukaguzi huo. “Tumbukiza kwenye gari” alitoa amri kapteni huyo kwa askari wa chini yake. Nilichukuliwa kikuku na kuingizwa kwenye lori aina ya Tata ambamo niliwakuta watu kama 10 hivi ndani ya lori hilo.
Ndugu wasomaji wa gazeti la Raia Mwema na kwa kweli uwasilishaji huu wa kitabu cha MATEKA MPAKANI kilichoandikwa na kachero Frowin Kagaueka, kuwaenzi wenzake wawili waliouawa na majasusi wa State Research Bureau (SRB) chini ya utawala wa Idi Amin wa Uganda, tunaishia hapa kuhusu yaliyomo kwenye kitabu hicho ambacho kitachapwa na kusambazwa kwa ajili ya kuuzwa hivi karibuni. Tunamshukuru Frowin Kageuka kwa kuruhusu wasomaji wa Raia Mwema kusoma sehemu ya kitabu hicho kupitia gazeti hili kabla ya kitabu husika kuchapwa na kusambazwa. Kwa maswali na mawasiliano zaidi kuhusu kitabu hicho mnaweza kuwasiliana moja kwa moja na mtunzi kwa namba ya simu 0715 411113 – Mhariri Raia mwema(nimecopy huko)