Zakumi, inaelekea umesoma Katiba moja tu (ya chama kimoja , kabla ya 1992), au umesahau moja ya Katiba (ya awali) ama hujasoma zote mbili (ya chama kimoja na ya vyama vingi - 1992). Nakushauri ujaribu kutafuta muda uzisome zote mbili halafu uje kujenga hoja hapa.
Mimi sioni lolote linalohusiana na mwongozo wa Nyerere katika utawala wa nchi yetu tangu tuvunje Azimio la Arusha na maazimio mengine yote, tangu turekebishe Muungano (kikatiba), tangu tubadilishe mwelekeo wa kiuchumi wa Taifa na tangu tuanze sera mpya za ubinafsishaji, biashara huria na kuingia kichwa kichwa kwenye globalization (bila kuielewa kwa kina na kuiandalia makao yake katika jamii yetu).
Zakumi, nchi hii haiyumbi kwa kuwa Nyerere aliamua hivyo. Nchi hii ilikuwa imara wakati wake. Sheria zilikuwa msumeno, viongozi walikuwa waadilifu zaidi na wananchi walikuwa na usawa wa wastani kuliko sasa. Sera zozote zilizokuwepo zilitekelezwa bila kujali eneo, rangi ya watu, uwezo n.k. WaTanzania walikuwa waTanzania wa kweli japo masikini.
Hivi sasa tumebadili mwelekeo kiasi kwamba, ili tuweze kurudi hadi pale alipotuachia Nyerere, tunahitaji kupigania uhuru upya. Na ni baada ya kufanya hivyo ndipo tunaweza kujiendeleza tena na kufika kwenye ustaarabu tunaoutaka. Kuna njia panda ambayo tulikosea kuchagua upande wa kupita na sasa tumepotea. Lakini tatizo letu si kukosea njia tuliyopita baada ya kufika njia panda, bali ni kuendelea kujidai hatujapotea na kuendelea na safari yetu hadi tutakapopotea zaidi na kushindwa kurudi tulipotoka.
Hilo ndilo linalotia hofu kuu.