Kutokana na taarifa ya uwepo wa huduma ya uwezeshaji kwa njia ya mikopo ambayo imekuwa ikitangazwa kupitia kurasa mbalimbali kupitia Facebook
Ofisi ya Waziri Mkuu taarifa inayokanusha uhalali wa kurasa hizo ambapo imesema:
Kumekuwepo na taarifa za uwepo wa ukurasa wa Facebook unaojitambulisha kwa jina la "Huduma ya Uwezeshaji", unaotangaza utoaji wa mikopo kwa madai ya "kupata mkopo ndani ya dakika tano" pamoja na mikopo yenye riba ya asilimia tano kwa mwezi.
Ukurasa huo unaendelea kuwadanganya wananchi kwa kutumia picha za viongozi wa Serikali bila idhini yoyote ili kuonekana kuwa rasmi na wa kuaminika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, wananchi wanaojaza fomu kupitia ukurasa huo hutakiwa kulipa kiasi cha hadi shilingi 120,000/= kama "akiba ya mkopo" kabla ya kupewa mkopo wa shilingi milioni moja (1,000,000/=).
Hata hivyo, baada ya kufanya malipo hayo, waombaji hawapati mkopo wowote na namba za mawasiliano zinazotolewa huwa hazipatikani. Hii ni mbinu ya kitapeli inayofahamika kama "ada ya awali", ambayo imekuwa ikitumika kuwaibia wananchi wengi.
Ofisi hiyo inautaarifu umma kuwa ukurasa huo hauna uhusiano wowote na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, hahusiki kwa namna yoyote na maudhui ya ukurasa huo wala matangazo yake.
Ofisi ya Waziri Mkuu inaonya kuwa watu wanaotumia picha za viongozi wa Serikali kwa madhumuni ya udanganyifu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Serikali ina mifumo rasmi na ya kisheria ya utoaji wa mikopo na uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwemo kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC),
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana pamoja na asilimia kumi (10%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri zinazotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Huduma hizo hutolewa kupitia taratibu rasmi za Serikali bila kutozwa ada yoyote ya awali.
Pia Tulia Akson mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pamoja na taasisi yake amekuwa aikihusishwa na mikopo hiyo, mnamo Agosti 16, 2025 Taasisi ya Tulia Trust
ilikanusha na kueleza kuwa ilipokea taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi waliodanganywa na matapeli wanaotumia jina la Tulia Trust kuomba pesa kwa ahadi ya kuwapatia mikopo, jambo ambalo ni uongo na udanganyifu wa wazi.