Kabla ya kuongeza nguvu, kumbuka...
Takribani miaka mitatu imepita toka kilipotokea kisa hiki:
Mkazi mmoja wa mji wa Matola mkoani Mbeya, alilazwa kwenye hospitali ya mkoa huo baada ya kuubonda na jiwe uume wake kwa kile alichokielezea baadaye kuwa ni kujikinga na maambukizi ya gonjwa la ukimwi.
Kisa cha mkazi huyo, ambaye ni kijana aliyekuwa chini ya miaka 35, kiliripotiwa na magazeti kadhaa nchini baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo kuwaelezea waandishi wa habari katika mkutano wake wa kawaida wa kuelezea matukio yaliyotokea mkoani mwake.
Baada ya kuripotiwa kwa kisa hiki, mjadala ukaanza, kila mtu aliyesikia au kusoma habari hiyo kwenye magazeti akaanza kusema lake, wapo waliosema kuwa kijana huyo aliyekuwa akitibiwa na madaktari, alikuwa mjinga na wapo waliosema kuwa alichofanya kilikuwa sahihi.
Waliosema kuwa alikuwa mjinga walikuwa na hoja zao, wengi walisema iwapo kama alikuwa anaogopa kuambukizwa Ukimwi basi si bora angetumia kondomu au angeoa mwanamke mmoja muaminifu au angeacha tu kushiriki tendo la ngono.
Kinyume na alichofanya kijana huyo wa Mbeya, katika hali ya kawaida, wanaume wengi wenye umri kama wake siku hizi wamekuwa wakihangaika na jambo moja kubwa, kutafuta dawa za kuongeza nguvu za kiume ili kukiongezea heshima kiungo kile.
``Yaani mie nijifyeke mwenyewe, haiwezekani!`` anasema Suleiman Bundara mkazi wa Magomeni Jijini Dar es Salaam na kujigamba; ``mimi nafikiria kuongeza makali kwa viagra, sio kujifyeka.``
Ni kweli, sio Bw. Bundara peke yake, wapo watu wengi duniani wa aina yake, ambao hata bila ya kuwa na matatizo ya nguvu za kiume, wanapenda kutumia dawa za kuongeza nguvu hizo.
Jaribu kuangalia karibu katika kila gazeti utakalo soma, ni nadra sana kukosa tangazo dogo la biashara lililotolewa na mganga wa kienyeji anayejigamba kuwa anazo dawa za kuongeza nguvu za kiume, na matangazo hayo hayaishii magazetini tu, bali hata redioni pia yapo.
Dawa zinazoongelewa hupewa majina mengi ya `kusisimua`, lengo kubwa likiwa ni kuwavuta wateja `kuingia` ili washawishike kuzijaribu, ndio biashara ilivyo.
Wingi huu wa matangazo umeanza kuonekana katika miaka ya hivi karibuni, na kadiri siku zinavyozidi ndivyo idadi ya waganga wanaojigamba kuwa na dawa hizo inavyozidi kushamiri, kuna waganga wenye dawa za Kiswahili, Kiarabu na za Kichina ndio usiseme!
Wingi wa matangazo hayo unaashiria jambo moja, kuwa lipo tatizo kubwa la wanaume kupungukiwa nguvu hizo, na ingawa hakuna utafiti wa kitaalamu uliofanywa rasmi, lakini inaonyesha kuwa tatizo hilo kwa sasa ni kubwa sana na si Tanzania tu, bali ni dunia nzima.
Kutokana na hali hiyo ndipo waganga wa kienyeji pamoja na makampuni mengi makubwa duniani hujaribu kuelekeza nguvu zao katika kufanya utafiti wa kutengeneza dawa za kusaidia watu wenye tatizo hilo, na bahati nzuri kwa makampuni na waganga hao ni kwamba inaonekana kama biashara inawaendea vizuri.
Kwa mujibu wa utafiti wa taasisi moja ya biashara ya dawa za aina hiyo nchini Uingereza, imebainika kuwa asilimia 46 ya wanaume nchini humo hutumia dawa hizo, hata hivyo wengi wao huzitumia bila ya kupata ushauri wa daktari na maduka mengi ya dawa yametozwa faini kwa kuwauzia dawa hizo bila ya kuwa na vyeti vya daktari.
Kupungua kwa nguvu za kiume, ambalo ni suala linalotokana na sababu zaidi ya moja, kumekuwa kukiwafanya wanaume wengi kuishi katika maisha na hali ya usononekaji na wengi wamekumbwa na umauti kutokana na hali hiyo ya kuishi na sononi kwa muda mrefu.
Sababu za kupungua kwa nguvu za kiume zipo nyingi, lakini wataalamu wa masuala ya saikolojia wanaamini kuwa mara nyingi suala hilo, hasa kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 45, linatokea kwa msongo wa akili kuliko ufanyaji kazi wa misuli ya mwili.
``Watu wengi wanaofikiri kuwa wamepungukiwa na nguvu hizo huwa hawako hivyo,`` inasema sehemu moja ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Havard, nchini Marekani na kufafanua kuwa:
``Tatizo la watu hao huwa ni kushiriki tendo hilo kwa wakati usio muafaka kwao, wanashiri wakati bado hawajajitayarisha kiakili au wanapokuwa wamejitayarisha, basi `njiani` hukutana na wenzi ambao hawaafiki mwelekeo wa `safari` yao``.
Wataalamu wa masuala ya vyakula nao wanaeleza kuwa tatizo hilo huwapata wanaume wengi kwa sababu ya utumiaji wa vyakula vyenye kuongeza kiwango kikubwa cha mafuta mwilini ambao hawashiriki katika mazoezi ya viungo ambayo huifanya misuli ya damu mwilini kutokufanya kazi vizuri na hivyo kusababisha matatizo mengi ya mwili kushindwa kufanya kazi zake vizuri.
Katika nchi zilizoendelea kama Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya, matumizi ya dawa hizi hutolewa kwa watu baada ya kuandikiwa cheti na daktari, na watu wenye matatizo ya msukumo wa ndamu (BP), mara nyingi wamekuwa wakishauriwa kutotumia dawa hizo kwa sababu ni hatari kwa maisha yao.
Hii ni kwa sababu dawa nyingi, kama Viagra, Ciallis, Levitra, Yohimbine na nyingine mbali ya kuwa na nafasi ya kusababisha magonjwa ya moyo, kwa watu wasiokuwa nayo, pia yana madhara mengine kama vile kusababisha upofu na kuleta hali ya mwili kuwa na kitetemeshi.
Madhara mengine ya dawa hizo ni pamoja na kumsababishia mtumiaji hali ya kuumwa na kichwa mara kwa mara, macho kuwa mekundu, kuziba kwa hewa puani na maumivu ya tumbo pamoja na kuharisha .
Haya ni aina ya madhara yanayotokana na dawa za kizungu, ambazo kabla ya kuingia madukani kufanyiwa utafiti wa kina kuangalia madhara yake kwa watumiaji, na ingawa hayo yote yanafanyika lakini bado athari zake kwa watumiaji zinaonekana.
Hapa ndipo panapozusha hofu juu ya dawa hizi nyingine `za kienyeji zinazotengenezwa na waganga na kuuzwa bila ya kufanyiwa utafiti wa kina, ni wazi kama kanuni za kiafya zinavyosema, kuwa kila dawa ina madhara yake, lakini je ni nani anapima madhara mabaya yatokanayo na dawa hizi za kienyeji zinazouzwa kama njugu?
Ukiacha madhara yatokanayo na dawa hizo, pia wanaume wengi hukumbwa na tatizo hili la kupungukiwa nguvu kwa sababu ya uvutaji wa sigara kwa wingi, utafiti mbalimbali wa kitabibu duniani unaonyesha kuwa matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku huwasababishia wanaume upungufu wa nguvu hizo.
Ni kweli kwamba tatizo la wanaume wengi kupungukiwa nguvu za kiume limekuwa kubwa duniani, lakini utumiaji wa dawa za kuongeza nguvu hizo haupaswi kufanyika kiholela kwa kuzingatia kuwa matatizo yake kiafya ni makubwa kuliko faraja ya muda mfupi anayopata mtumiaji.